Obama Alikuwa Akikoroma Sana, Michelle Alikuwa Akichonga Sana

Friday, September 25, 2009 / Posted by ishak /


Ndoa ya rais wa Marekani, Barack Obama na mkewe Michelle iliwahi kupitia misukosuko mikubwa ambayo ilitishia kuvunjika kwake. Miongoni mwa vitu vilivyokuwa vikisababisha kutokuelewana ni Obama kuvuta sana sigara na kukoroma sana usiku wakati Obama alikuwa akichukizwa na tabia ya Michelle kumsema sema sana kila wakati.
Wakati Obama alikuwa hapendi jinsi Michelle alivyokuwa akichonga sana na kumkosoa mara kwa mara, Michelle alikuwa akichukizwa na tabia ya Obama kukoroma sana wakati wa kulala na kuvuta sana sigara kiasi cha kwamba alikuwa akinuka sigara muda wote.

Mwaka 2007 wakati akifanya mahojiano na jarida la Glamour la Marekani, Michelle alisema kuwa Obama alikuwa ananuka sana sigara na kukoroma sana kiasi cha kwamba watoto wao walikuwa hawataki kulala naye.

Michelle pia alikuwa akichukizwa sana na Obama kujihusisha zaidi na siasa kuliko kuiangalia familia yake.

Mara kwa mara Michelle alimwambia Obama "Unajifikiria mwenyewe tu, sikuwahi kufikiria kwamba nitakuja kuilea familia peke yangu, sikuolewa kwaajili hii".

Michelle pia aliwahi kumwambia Obama wakati huo wakiwa na mtoto mmoja kwamba baada ya miaka minane ya ndoa yao, siku za ndoa yao zilikuwa zikihesabika na wakati wowote ingevunjika.

Kwa upande wake Obama alimwambia bibi yake Madelyn 'Toot' Dunham, ambaye alimlea alipokuwa Hawaii kwamba "Nampenda sana Michelle, lakini ni mkali sana na wakati wote ana hasira".

Maisha ya Obama na mkewe yameongelewa kwenye kitabu cha "Barack And Michelle: The Love Story " cha mwandishi wa habari wa Marekani na mtunzi wa vitabu, Christopher Andersen, ambacho kimeingia madukani wiki hii.

Historia ya Obama inaanzia Honolulu, Hawaii alikozaliwa kutokana na mama Mmarekani na baba 'Cha Pombe' (Mlevi sana) toka Kenya aliyekuwa mwanafunzi nchini Marekani.

Obama alilelewa na mama yake nchini Marekani na Indonesia wakati huo baba yake alirudi Kenya na kuoa mke mwingine.

Obama Alikutana na Michelle Robinson baada ya kumaliza mwaka wake wa kwanza kwenye chuo cha Harvard Law School, na kwenda kufanya field yake wakati wa likizo kwenye kampuni kubwa ya sheria inayoitwa Sidley Austin.

Michelle ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni hiyo ndiye aliyepewa majukumu ya kumsimamia Obama wakati wa field yake kwenye kampuni hiyo.

Obama alivutiwa na Michelle baada ya kutambulishwa na alimwambia rafiki yake baadae kwamba "Michelle ni mrembo sana, nitatumia uchawi wangu wote kumnasa".

Ili kumwingiza kwenye mitego yake, Obama alianza kumtumia Michelle maua na barua za kimapenzi pamoja kumpigia simu mara kwa mara mpaka alipokubali mwaliko wake baada ya kumsikia akitoa hotuba kwenye mkutano wa vijana weusi wa Marekani.

Hatimaye Obama alifanikiwa kumnasa Michelle na alifunga naye ndoa ilipofika oktoba 3 mwaka 1992.

Ndani ya miaka minne ya ndoa yao huku Obama akiwa amejikita zaidi kwenye siasa na kuchaguliwa kuwa seneta wa jimbo la Illinois, matatizo yalianza kujitokeza kwenye ndoa yao.

Michelle alikuwa akichukizwa na tabia ya Obama kutofanya usafi na kutozihifadhi vizuri soksi na chupi zake kwani baada ya kuzivua alikuwa akizitelekeza kwenye sakafu.

Michelle alichukizwa pia na tabia ya Obama kutofanya kazi yoyote ya nyumbani na kuacha mataulo yaliyolowa kwenye sakafu bafuni na pia kuacha vyombo vichafu kwenye sinki baada ya kula.

Hakuna kitu ambacho Michelle alikuwa akikichukia zaidi kama uvutaji wa sigara wa kupindukia wa Obama. Michelle alikuwa akilalamika nyumba yao ilikuwa ikinuka sigara na mazulia yao yote yalikuwa na matobo kutokana na moto wa sigara.

Wakati Michelle alikuwa akiingia kulala saa nne usiku ili awahi kuamka kuwahi kwenye kazi yake aliyokuwa akilipwa pesa nyingi sana, Obama alikuwa akiingia kitandani kulala mida ya saa nane usiku.

Mbali na kuingia kitandani kulala mida hiyo, Obama alikuwa akimsumbua Michelle kwa kukoroma sana.

Kuzaliwa kwa binti yao wa kwanza Malia, julai 4 mwaka 1998 hakukusaidia kuiimarisha ndoa hiyo badala yake kuliifanya ndoa hiyo iwe hatarini.

Obama alikuwa akitumia siku nne hadi tano akiwa mji mwingine kwenye bunge la Seneti na hali hiyo ilimfanya Michelle ajihisi ametelekezwa.

Michelle alifikiria kwamba Obama alikuwa akipoteza muda kwenye siasa badala ya kufanya kazi kama mwanasheria na kulipwa pesa nyingi zaidi.

Misuko suko kwenye ndoa ya Obama ilipungua wakati binti yake wa pili Natasha ambaye anajulikana zaidi kama Sasha alipopata ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo (Meningitis) mwaka 2001 wakati huo akiwa na umri wa miezi mitatu.

Sasha aliwahishwa hospitali na ilimbidi Obama na mkewe wapokezane kukaa naye hospitali kwa masaa 72 wakati alipolazwa kwa matibabu zaidi.

Baada ya hapo utulivu ulirudi kwenye ndoa yao na mambo yote yalikaa sawa baada ya Obama kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani.

Hatimaye mwezi novemba mwaka jana katika mji wa Chicago familia ya Obama ilitambulishwa rasmi kuwa familia namba moja ya Marekani.

"Nisingesimama hapa bila ya msaada wa rafiki yangu wa miaka 16, nguzo ya familia yangu, mke wangu Michelle Obama" alisema Obama.

Hivi sasa familia ya Obama imesahau yaliyopita na imekuwa ikitolewa mifano kama mojawapo ya familia bora duniani.

0 comments:

Post a Comment