Miujiza ya Kijana Aliyefariki Yawapagawisha Wengi

Wednesday, December 23, 2009 / Posted by ishak /


Mamia ya watu wanamiminika kwenye nyumba ya kijana mmoja nchini Australia ambaye muda mfupi baada ya kufariki kuta za nyumba yake zimeanza kutoa mafuta ya ajabu ambayo yanadaiwa kuwatibu watu magonjwa yao.
Wazazi wa kijana Mike Tannous aliyefariki miaka mitatu iliyopita wanadai kuwa kijana wao amechaguliwa na mungu kuwa mtawa wa kwanza wa kiume wa Australia.

Mike alifariki mwezi septemba mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 17 kutokana na ajali ya gari lakini wiki chache baadae kuta za chumba chake zilianza kutoa mafuta ya ajabu ambayo yanadaiwa kuwatibu mamia ya watu magonjwa yao.

Wazazi wake Mike, George na Lina wanaoishi katika kitongoji cha Guildford katika jiji la Sydney wamedai kuwa kijana wao ni mjumbe wa mungu na ameishawatibu watu wengi sana kwa miujiza yake.

Mafuta yanayomiminika kwenye kuta za nyumba yake yamefanyiwa uchunguzi wa kisayansi na wataalamu mbali mbali lakini bado hayajagundulika ni mafuta ya aina gani.

Mamia ya watu wamekuwa wakimiminika kwenye nyumba yao kuyaona na kusali wakiomba yawatibu magonjwa yao.
“Mtoto wetu ni mtawa, anazungumza nasi na anazungumza na watu kwa njia hii”, alisema baba wa kijana huyo.

“Mwaka jana mwanamke mmoja anayeishi karibu na nyumba yetu aliambiwa na madaktari hataweza kupata mtoto wa tatu kwa njia yoyote ile, alikuja hapa na kuanza kusali… mwezi mmoja baadae alirudi na boksi la biskuti akitamba kuwa amepata ujauzito”, alisema shangazi yake Mike, Susan Sawan.

Mamia ya watu wamekuwa wakimiminika kila siku kwenye nyumba hiyo na hivi sasa si kuta za chumba chake pekee zinazovuja mafuta bali kuta zote za nyumba hiyo ya vyumba vitatu mpaka kwenye picha ya Mike ukutani.

“Mwishoni mwa wiki watu huja toka sehemu mbali mbali na kutufanya tufunge mtaa, wanataka kushuhudia miujiza”, alisema baba wa kijana huyo aliyefariki.

Kutokana na habari za miujiza ya tiba ya mafuta ya kuta za nyumba hiyo kusambaa, mamia ya watu kutokana nchi mbali mbali duniani nao wamekuwa wakimiminika Austalia kushuhudia mafuta hayo.

Wazazi wa Mike wamesema kuwa wao hawakusanyi mchango wowote toka kwa watu wanaofika kwenye nyumba yao wanachopenda wao ni kuona watu wakipatiwa tiba kutokana na miujiza ya mtoto wao.

Familia hiyo imekuwa ikiwajibu watu wasioamini wanaotilishia shaka miujiza ya mafuta hayo kwa kuwaambia “Njoo na ushuhudie mwenyewe”.

source.nifamishe.com

0 comments:

Post a Comment