Adhana Inapopigwa Kanisani Kuwaita Waislamu..

Friday, January 29, 2010 / Posted by ishak /


Sauti kubwa ya adhana ikitoka kanisani iliwashangaza watu wengi katika mji wa Mainz nchini Ujerumani waliokuwa hawajui nia ya msanii wa Ujerumani ambaye alitumia adhana na kengele ya kanisani kuwakusanyisha waislamu na wakristo.
Katika kuleta amani na upendo baina ya waislamu na wakristo, msanii wa Ujerumani, Miriam Kilali alitumia staili ya aina yake kuwavuta watu kwa kupiga adhana ndani ya kanisa kuwaita waislamu na kutumia kengele kuwaita wakristo.

Miriam mwenye umri wa miaka 44 alirekodi adhana kwenye radio na kwenda kuipiga kwenye spika kubwa ndani ya kanisa na kuwafanya watu wengi wapita njia na wakazi wa maeneo ya karibu na kanisa hilo wabaki wakishangaa imekuwaje adhana inasikika kutokea kanisani.

Adhana ya kwanza ilisikika leo ijumaa saa nane mchana kwa saa za Ujerumani kabla ya kufuatiwa na milio ya kengele inayotumika siku zote kuwaita watu kanisani.

Adhana ilisikika leo kwa takribani dakika sita toka kwenye kanisa la St Anthony Chapel katika mji wa Mainz na itasikika tena siku ya jumamosi saa nne asubuhi, saa nane mchana na saa 11 jioni.

"Hii haikubaliki", alilalamika mwanamama mmoja wa kijerumani ambaye hakutaka kutaja jina lake.

"Wamechukua kila kitu chetu... zamani tulikuwa nchi ya kikatoliki", aliendelea kulalama mwanamama huyo.

"Najihisi kama nipo nyumbani vile ninaposikia adhana kama hii", alisema Mturuki Asil Yenertürk (52) akikumbushia adhana nchini Uturuki.

Naye mjerumani Johanna Demhardt mwenye umri wa miaka 70 alisema kuwa adhana hiyo imemkumbusha ziara yake nchini Singapore na aliendelea kusema kuwa si sahihi kwa adhana kusikika katika mitaa ya Mainz.

Naye Miriam muandaaji wa adhana hiyo kanisani alisema kuwa aliamua kufanya hivyo ili kujenga uhusiano mwema kati ya waislamu na wakristo.

"Mijadala mizito ya kujengwa misikiti barani ulaya, kuwakataza wanawake kuvaa hijab, kuwahusisha waislamu na ugaidi ni mojawapo ya mambo yanayoongeza chuki kati ya waislamu na wakristo", alisema Miriam.

Miriam alisema kuwa aliamua kutumia adhana na kengele kwa wakati mmoja ili kuwaunganisha waislamu na wakristo kwa kutumia maonyesho ya sanaa yanayoendelea kwenye kanisa hilo.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment