Jambazi Lasalimisha Silaha Kigoma, Laachiwa Huru

Friday, January 29, 2010 / Posted by ishak /


Jeshi la polisi mkoani Kigoma limemwachia huru kwa msamaha maalumu mkazi mmoja wa kijiji cha Nyamidaho wilayani Kasulu aliyesalimisha kwa serikali ya kijiji, silaha ya kivita aliyokuwa akiitumia kwa ujambazi.
Kamanda wa polisi mkoani Kigoma kamishina msaidizi wa polisi George Mayunga amemtaja mtu huyo kuwa ni Nathan Morton aliyekuwa akitajwa kuimiliki silaha hiyo kinyume cha sheria.

Kamanda Mayunga ameeleza kuwa, Morton amejisalimisha kwa mwenyekiti wa kijiji Bw. Henriko Kimorimori baada ya ushawishi mkubwa uliomtaka kujisalimisha kabla ya jeshi la polisi kufanya msako.

Amebainisha kuwa bunduki iliyokamatwa ni SMG yenye namba za usajili 109484 na kwamba jeshi la polisi kwa kutambua umuhimu wa mtu kusalimisha mwenyewe limempa msamaha na kipindi cha matazamio.

Aidha katika tukio hilo lililotokea ijumaa iliyopita, serikali ya kata ya Nyamidaho imeagizwa kuunda timu maalumu itakayofuatilia mwenendo wa maisha ya Bw. Nathan Morton ili kuhakiki kama hajihusishi na uharifu zaidi.

Kufuatia tukio hilo mkuu wa polisi mkoa wa Kigoma George Mayunga ametangaza rasmi kutoa msamaha kwa jambazi atakayesalimisha silaha kwa hiyari katika kipindi cha mwezi mmoja.

Amesema endapo mmiliki haramu wa silaha atajisalimisha jeshi la polisi halitamchukulia hatua yoyote zaidi ya kumpa ushauri nasaha wa kubadili tabia na kuacha uhalifu.

Hata hivyo kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma amesisitiza kuwa operesheni kamambe inaendelea ili kuhakikisha wamiliki wa silaha na watekelezaji wa vitendo vya ujambazi wanakamatwa na kufikishwa katika mkondo wa sheria.

Na katika tukio jingine lisilo la kawaida, mkazi mmoja wa manspaa ya kigoma Ujiji Bw. Hassan Baguma anashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kukamatwa wakati akifanya shambulio la hatari kwa kuwakata kwa panga mkewe, shemejiwe na mama mkwe wake.

Tukio hilo limetokea jumanne wiki hii katika mtaa wa hali ya hewa mjini Kigoma umbali wa mita 200 toka makao makuu ya polisi Kigoma wakati Bw. Hassan alipofika ukweni kwake na kuanza kuwashambulia wana ndugu hao kwa mapanga na kuwajeruhi vibaya.

Kamanda George Mayunga amewataja waliojeruhiwa kuwa ni mke wa mtuhumiwa Bi.Mwamini Francis, Shemejie aliyetambuliwa kwa jina la Emanuel Baguma na mama mkwe wake ajulikanaye kwa jina la Asia Francis.

Majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Kigoma Maweni ambako wanaendelea kupata matibabu.

Chanzo cha Bw. Hassan kuwacharanga mapanga wanandugu hao kinatajwa kuwa ugomvi wa ndoa baina yake na mkewe Bi. Mwamini ambaye mumewe anamtuhumu kumfilisi na kisha kumkimbia na kuambatana na wanaume wengine kwa ushawishi wa mama yake na ndugu wengine.

source nifahamishe