Abby Sykes aamua kuja kivingine

Sunday, February 28, 2010 / Posted by ishak /

JE, unamfahamu mwanamuziki mkongwe Ibrahim Abdulwaheed Sykes maarufu kama Abby Sykes?

Hili si jina geni miongoni mwa wanamuziki nchini, lakini kama hulifahamu sina shaka jina la msanii wa muziki wa kizazi kipya Dully Sykes utakuwa unalifahamu vyema.

Ni kwamba Ibrahim Abdulwaheed Sykes au Abby Sykes kwa wasiomfahamu ndio baba mzazi wa msanii Dully Sykes.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, msanii huyo alisema alianza kujifunza muziki mwaka 1966, kwa kutoroka usiku nyumbani na kwenda disko na kwamba kutokana na kupenda sana muziki ndipo akatumia gita la baba yake mdogo kujifunza.

Anasema baada ya kuanza kuimba kwenye majukwaa, ndipo akakutana na Adamu Kingoni, akiwa kiongozi wa bendi ya Rifters.

Sykes anasema familia yao iliwahi kuunda kundi maarufu lililojulikana kama Shery Merry Marcas, ambalo liliundwa na baba zake kama Abdulwaheed Sykes, Ally Sykes, Balozi Sykes.

Anasema ilipofika mwaka 1970, ndipo akajiunga na bendi hiyo ya Rifters akiwa mpiga gita. Baada ya kukaa muda mrefu katika bendi hiyo, akaamua kujitoa na kujiunga na bendi nyingine ya Kenya iliyoitwa Hold Banjo.

Anasema kipindi hicho alikuwa akipiga karibuni vifaa vyote vya muziki, huku akijifunza kuimba kwa kusikiliza nyimbo za wanamuziki maarufu wa nje akiwemo kama James Brown.

Anasema mwaka 1978 akajipanga na kutoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa Mimi na Wewe na kwamba albamu hiyo aliweza kupata fedha kidogo, lakini zaidi fedha zao ilikuwa kwenye matamasha.

Anasema kutokana na kuona muziki haulipi vizuri aliungana na rafiki zake na kuomba kazi katika Meli ya mv Oman. Anasema kipindi hicho, mtu huwezi kuonekana bora, au mjanja bila kuwa baharia au mfanyakazi wa bandari.

Akaamua kuachana na kazi ya muziki, na kuungana na wenzake katika kazi ya ubaharia na kuendelea kujifunza vitu vingi kutoka nchi mbalimbali.

Baada ya safari ya kwanza ya miezi minane kurudi, aliamua kuachana na meli hiyo, na kujiunga na meli nyingine ya Youcht kwa miezi minane mingine.

Akiwa Baharia anasema aliona vitendo vingi vya kiovu vilivyoendelea baharini, lakini kubwa ambalo anashindwa kulisahau, anasema siku moja, wakiwa kwenye safari za nchi ya mashariki ya mbali wakiwa katikati ya maji aliona wamekamatwa Watanzania wanne na Wakenya saba.

Anasema baada ya kufikishwa kwa mkubwa, walitupwa baharini. Hapo ndipo roho ilipomuuma kuona ndugu zake wa Kitanzania na wale Wakenya wakiliwa na papa mbele ya macho yao.

Msanii huyo anasema kuwa alipata taarifa kuwa kuna Mkenya mmoja alipona katika sakata hilo na hadi hii leo akikumbuka wenzake hulia na kuchanganyikiwa. Mwaka 1980 akaamua kuachana na kazi hiyo ya ubaharia na kurudia kazi yake ya muziki.

Mwanamuziki huyo anasema yote hayo yameshapita na hivi sasa amerudi, kama zamani na anatarajia kufanya mapinduzi makubwa ya muziki.

Anasema amejiandaa kuibuka na bendi itakayoundwa na yeye, mwanawe na kuwa ameshajiandaa kutoa albamu yake ya pili ukiachilia ile ya zamani ya mwaka 1978 ya Mimi na Wewe.

Albamu hiyo amerekodia studio ya Dhahabu Record inayomilikiwa na Dully Sykes. Tayari ameshakamilisha kurekodi nyimbo kadhaa na kuzitaja kuwa ni Mchumba Mzuri, Famili Song, Only You, Lalaa akiwashirikisha mwanaye Dully Sykes na Mr Blue.

Anasema mtu ambaye anapenda sana kazi zake, na pindi akiwa sawa basi atamshirikisha katika albamu hiyo ni msanii David Nyika ‘Daz Baba’.

Mkali huyo ana nyimbo kwenye albamu moja ya wanamuziki mchanganyiko ya Urithi, ama Baba na Mwana, ambayo ni ya wasanii maarufu walioimba na watoto zao, kama Nguza Vicking na Papi Kocha, Zahir Ally na Banana Zoro, yeye akiimba wimbo wa Malaika.

source habarileo

0 comments:

Post a Comment