Tunastahili Kuadhibiwa Baada ya Kuzini'

Monday, February 22, 2010 / Posted by ishak /


Wanawake watatu wa nchini Malaysia ambao walicharazwa bakora kwa kufanya mapenzi kabla ya kuolewa wamesema kuwa walistahili adhabu waliyopewa ili kuwawezesha kutubu madhambi yao.
Wanawake watatu ambao wamekuwa wanawake wa kwanza kucharazwa bakora nchini Malaysia kutokana na kufanya zinaa, wamesema kuwa walistahili adhabu waliyopewa.

Wanawake hao walicharazwa bakora wiki iliyopita baada ya kuhukumiwa na mahakama ya sheria za kiislamu kwa kufanya mapenzi kabla ya ndoa.

Kucharazwa bakora kwa wanawake hao kulisababisha hasira za makundi ya kutetea wanawake lakini wanawake hao wamejitokeza na kuzitetea adhabu walizopewa wakisema kuwa walistahili adhabu hizo kwa kosa kubwa la zinaa walilofanya.

Wanawake hao watatu wenye umri kati ya miaka 17 na 25 walijipeleka wenyewe kwenye mahakama za sheria za kiislamu wakisema kuwa wanajisikia vibaya baada ya kufanya mapenzi na wapenzi wao kabla ya kuoana na kupelekea wapate ujauzito.

Mmoja wa wanawake hao ambaye ana umri wa miaka 17 aliwaambia waandishi wa habari kuwa alijisalimisha mwenyewe kwenye mamlaka za kiislamu baada ya kufariki kwa mtoto aliyemzaa kabla ya muda wake wa kuzaliwa kufika. Hivi sasa mwanamke huyo anatumikia kifungo cha miezi sita jela.

"Najua nimefanya dhambi, nastahili kuadhibiwa, najua kucharazwa bakora ni mateso makubwa lakini nimeona kuwa ni njia bora ya mimi kutubu madhambi yangu na kurudi kwenye njia sahihi", alisema mwanamke huyo.

Mwanamke huyo tayari ameishafunga ndoa na mpenzi wake ambaye naye alicharazwa bakora na kisha kutumikia kifungo jela kwa kufanya kosa hilo la zinaa kabla ya ndoa.

Wanawake wengine wawili ambao wote wana mtoto mmoja mmoja, nao wanatarajia kufunga ndoa na wapenzi wao pindi watakapotoka jela.

Wanaume zao nao walicharazwa bakora na kutupwa jela kwa kosa hilo hilo la kufanya mapenzi kabla ya ndoa.

Wanawake wote watatu wanawashauri watu wengine wasifanye makosa ya kufanya zinaa na ambao wameishatenda dhambi hiyo wajitokeze kutubu dhambi zao.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment