Uingereza Kuzibania Viza Za Wanafunzi

Monday, February 08, 2010 / Posted by ishak /


Serikali ya Uingereza imetangaza mpango wake wa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopewa viza za kusoma nchini humo.
Serikali ya Uingereza imetangaza kuweka sheria na masharti magumu katika utolewaji wa viza za uanafunzi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza, Alan Johnson amesema kuwa masharti magumu yameongezwa katika maombi ya viza za uanafunzi kwa wanafunzi toka nchi zote duniani.

Mojawapo ya masharti yaliyoongezwa katika uombaji wa viza za uanafunzi ni kwa mwanafunzi anayeomba viza kutakiwa awe anaongea kiingereza fasaha.

Miongoni mwa sheria ziliongezwa ni kama vile kuwazuia wanafunzi wenye viza za muda mfupi kuwaleta Uingereza jamaa zao kama vitegemezi (dependant) wao.

Sheria mpya zimewekwa kufuatia waziri mkuu wa Uingereza kutaka masharti ya utolewaji wa viza yaangaliwe upya kufuatia tukio la mwanafunzi wa Nigeria aliyemaliza masomo yake nchini Uingereza kujaribu kuilipua ndege ya Marekani bila mafanikio.

Sababu kubwa ya kuwekwa kwa sheria hizi ni kupunguza idadi ya wanafunzi toka barani Afrika na Asia ambao hujishughulisha zaidi na kufanya kazi kuliko masomo yao.

Awali mwaka mmoja uliopita Uingereza iliongeza ugumu katika utolewaji wa viza za wanafunzi kwa kuwataka wanafunzi watoe vithibitisho vya kuweza kujilipia ada yote ya masomo yao na pia kuwa na uwezo wa kifedha kukimu gharama za maisha yao nchini Uingereza.

Wiki iliyopita, Uingereza ilisimamisha kwa muda kupokea maombi ya viza za wanafunzi kutoka maeneo ya kaskazini mwa India, Nepal na Bangladesh. Hatua hiyo ilitokana na idadi kubwa kuliko kawaida ya maombi ya viza za uanafunzi toka maeneo hayo.

Wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza imesema kuwa kutokana na masharti mapya ya utolewaji wa viza za wanafunzi, idadi ya wanafunzi watakaopewa viza itapungua sana lakini hata hivyo wizara hiyo ilikataa kutoa tathmini zao.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment