Ajali Ya Ndege Yaizuia The Cranes Kutua Mwanza

Wednesday, March 03, 2010 / Posted by ishak /


TIMU ya soka ya taifa ya Uganda, The Uganda Cranes, jana ilishindwa kuwasili jijini Mwanza kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa jijini humo kutokana na ajali ya Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku, katika ajali hiyo, watu wote waliokuwamo katika ndege hiyo wakati ikijiandaa kutua ikitokea Dar es Salaam, wamenusurika lakini uwanja ukifungwa kwa sababu za kiusalama zaidi.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737 yenye namba SH-Mvz, ilipata ajali hiyo jana majira ya saa 1:45 asubuhi; wakati ikitua tairi zake mbili zilipasuka na kusababisha kuacha njia yake huku injini moja ya kushoto ikiingiliwa maji.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, wakati ndege hiyo ikitua uwanjani hapo kulikuwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha ghafla kilisikika kishindo kikubwa kilichowashtua.

Akizungumza na gazeti moja la kila siku, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, alisema kutokana na kufungwa kwa uwanja huo kwa siku ya jana, Uganda Cranes walishindwa kuwasili kama ilivyokuwa imepangwa.

Mwakalebela alisema baada ya ajali hiyo, TFF iliwasiliana na Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) wakiwataka kusitisha safari yao kwa jana ili kuepuka usumbufu hadi leo tayari kwa mechi ya kirafiki itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa CCM- Kirumba.

Alisema pamoja na tatizo hilo, maandalizi ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na kusema vijana wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo.

Mwakalebela alisema mechi hiyo ni muhimu zaidi kwa Stars kwa ajili ya kujiandaa na kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani (CHAN).

Stars itaanza kampeni yake dhidi ya Somalia, mechi itakayopigwa Machi 13 kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment