Madhara ya Mabomu ya Marekani, Watoto wa Ajabu Wazaliwa Iraq

Friday, March 05, 2010 / Posted by ishak /


Madhara ya mabomu ya Marekani nchini Iraq yanajidhirisha kwa idadi kubwa ya watoto wenye vilema na maumbile ya ajabu ajabu kama vile watoto wenye vichwa vitatu kuzaliwa nchini Iraq na kuwafanya maafisa wa Iraq wawashauri wanawake wafunge kizazi.
Marekani inahisiwa kuwa ilitumia mabomu ya kikemikali katika mashambulizi yake ya mabomu nchini Iraq mwaka 2004, hii inatokana na idadi kubwa sana ya watoto wanaozaliwa wakiwa na maumbile ya ajabu ajabu.

Katika mji wa Fallujah ambapo ndipo mabomu mengi ya Marekani yalidondoshwa kuung'oa upinzani wa majeshi ya Saddam, idadi kubwa sana ya watoto wenye matatizo mbali mbali wamekuwa wakizaliwa kiasi cha kuwafanya madaktari wawashauri wanawake wa Fallujah wasizae.

Baadhi ya watoto wamekuwa wakizaliwa wakiwa na matatizo ya akili, wengine matatizo ya moyo huku wengine wakiwa na maumbile yasiyo ya kawaida.

Mwandishi wa BBC, John Simpson, aliyetoa ripoti yake toka Fallujah alikiri kushuhudia idadi kubwa ya watoto wenye maumbile ya ajabu.

Mmoja wa watoto hao alikuwa na vichwa vitatu wakati mwingine alikuwa na jicho moja huku watoto wengi wakiwa na maumbile ya kutisha zaidi.

Idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na matatizo ya moyo, ubongo au kupooza upande mmoja ni wengi sana kiasi cha kwamba madaktari wanasema kuwa kila siku watoto watatu wanazaliwa mjini Fallujah wakiwa na kasoro kwenye maumbile yao.

Maafisa wa Iraq wanawashauri wanawake wa Fallujah kuziacha ndoto zao za kuwa na watoto kwani watoto watakaozaliwa watakuwa na maumbile ya ajabu.

Majeshi ya Marekani yaliumiminia mabomu makubwa mji wa Fallujah kiasi cha kwamba nusu ya nyumba zote za Fallujah na misikiti ilibomolewa.

Marekani ilikiri kutumia mabomu hatari ya phosphorus ambayo yamepigwa marufuku duniani kutumika kwenye vita kutokana na uharibifu mkubwa unaotokana na mabomu hayo.

Majeshi ya Marekani yalianza mashambulizi yake mjini Fallujah kuanzia novemba 7 mwaka 2004 na baada ya siku 9 walitangaza kuuteka mji huo.

Wanajeshi 51 wa Marekani walifariki kwenye mashambulizi hayo wakati wanamgambo wa Iraq 1,400 waliuliwa kwenye mashambulizi hayo.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment