Mtikila atakwenda jela endapo atashindwa kulipa deni

Monday, March 08, 2010 / Posted by ishak /

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala ya jijini Dar es Salaam, imeamuru kunadiwa kwa mali za Mchungaji Mtikila ili kuweza kulipa deni linalomkabili kinyume na hapo atakwnda jela.
Uamuzi huo wa Mahakama umekuja baada ya ombi la kumtaka mchungaji kufungwa jela baada ya kushindwa kulipa deni la silingi milioni 8 analodaiwa.

Hivyo mahakama imeamuru kudainiwa kwa mali zake ili kuweza kufidia kulipa deni hilo na endapo itashindikana ombi la kufungwa kwake litazingatiwa.

Awali Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliamua nyumba ya mchungaji huyo iliyopo Mikocheni jijini Dar es salaam iuzwe ili kufidia deni hilo, lakini Hakimu Hakimu Afumwisye Kibona alisitisha uamuzi huo na kuagiza mali zake nyingine ziuzwe kufanikisha malipo ya deni hilo.

Mtikila na mwenzake Mariam Issa wanadaiwa zaidi ya Shilingi milioni 8 na Pascazia Matete ambaye alidai aliwakopesha kwa ajili ya kufanyia biashara.

Matete alishinda kesi namba 78 ya mwaka 2008 aliyoifungua katika Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo mbele ya Hakimu Benjamin Mwakasonda.

Akitoa amri hiyo, Hakimu Kibona alisisitiza kuwa iwapo ombi hilo la kutafuta mali mbadala za Mtikila ziuzwe kwa ajili ya kulipa deni hilo halitafanikiwa, ombi la kumfunga jela litafuatia.

Uamuzi huo wa kumfunga au kutomfunga utatolewa Machi 18, mwaka huu na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Joyce Minde.

Awali baada ya Matete kushinda kesi hiyo kutokana na Mtikila kutohudhuria Mahakamani mara kwa mara, aliiomba mahakama iamuru nyumba ya Mtikila yenye namba MKC/MCB 1135 iliyo kwenye kiwanja namba 237, Kitalu C Mikocheni iuzwe ili alipwe deni lake.

Hata hivyo, ombi la kuuza nyumba hiyo lilishindikana baada ya kampuni ya kimataifa ya Cielmac kuwasilisha pingamizi ikieleza kuwa ilishanunua nyumba hiyo kwenye mnada uliofanywa na benki ya NBC kupitia kampuni ya Comrade Auction Mart $ Court Brokes baada ya Mtikila kushindwa kurejesha mkopo wa Sh15 milioni aliouchukua katika benki hiyo.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment