Mwanamke Afungwa Jela ya Wanaume Kwa Miezi Sita

Wednesday, March 24, 2010 / Posted by ishak /


Skendo limeikumba kitengo cha kurekebisha tabia cha Afrika Kusini ambapo mwanamke aliyakamatwa kwa makosa ya ujambazi anadaiwa kufungwa kwenye jela ya wanaume kwa kipindi cha miezi sita na kupelekea mwanamke huyo abakwe na kulawitiwa na wafungwa wa kiume.
Denise Wilson au maarufu kwa jina la Abbah wa mji wa Isipingo nchini Afrika Kusini amekifungulia mashtaka kitengo cha kurekebisha tabia cha Afrika Kusini kwa kumweka kwenye jela ya wanaume kwa miezi sita wakati alipokuwa akisubiria kufikishwa mahakamani kwa makosa ya ujambazi, kujaribu kuua na kuteka watu.

Denise anadai fidia ya rand 100,000 kwa madhila aliyoyapata wakati alipokuwa kwenye jela ya wanaume.

Katika nyaraka za mahakama, Denise alisema kuwa alikamatwa septemba 24 mwaka 2002 na kupelekwa kwenye jela ya wanaume.

Alisema kuwa kitendo chake cha kupinga kuwekwa jela moja na wanaume kilisababisha avuliwe nguo mbele ya wanaume huku akizomewa na kuchekwa.

Wakati wa kipindi chake cha miezi sita kwenye jela ya wanaume, Denise anadai kuwa walinzi wa jela walikuwa wakimlazimisha afanye matendo ya ngono bila ya idhini yake.

Alidai pia kuwa wafungwa wa kiume walikuwa wakimpapasa mara kwa mara kwenye sehemu zake za siri bila ya idhini yake.

Denise pia hakusita kusema kuwa alibakwa na kulawitiwa katika kipindi cha miezi sita kwenye jela ya wanaume.

Alisema kuwa ingawa maafisa wa jela walikuwa wakijua kuwa yeye ni mwanamke, waliendelea kumweka jela moja pamoja na wanaume.

Alisema kuwa hata daktari wa wilaya alipomfanyia uchunguzi wa kuthibitisha jinsia yake, aliendelea kuwekwa kwenye jela hiyo.

Kitengo cha kurekebisha tabia cha Afrika Kusini kimeamua kukaa kimya kikisubiria kesi hiyo ianze kusikilizwa mahakamani.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment