Serikali yaamuru umeme upitishwe Kanisa la Kakobe

Monday, March 08, 2010 / Posted by ishak /

HATIMAYE Serikali imeamua kupitisha waya za umeme wa msongo wa kilovolti 132 karibu na Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Serikali imetoa amri hiyo bila kupingwa baada ya kuridhika na taarifa iliyotolewa na kitengo cha utoaji ushauri cha Chuo Kikuu (BICO).

Jana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja,akizungumza na waandishi wa habari alisema utekelezaji wa mradi huo unatakiwa kufanyika mara moja kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi, kwani ni kwa ajili ya manufaa na ustawi wa taifa.

Alisema serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuridhika na utafiti uliofanywa na wataalamu washauri wa BICO, TANESCO na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) umehakikishia serikali kuwa umeme huo hauna madhara kwa wananchi.

“Hivyo TANESCO inatakiwa kuendelea na zoezi la upitishaji wa nguzo za umeme katika eneo hilo” alisema Waziri.
Awali alisema kuwa kuna taarifa zilidai kuwa vipimo vya kupitihsa umeme huio kanisani hapo vilikosewa lakini iliundwa tume kuthibitisha hilo.

Hata hivyo alisema baada ya uchunguzi ilibaini hakuna vipimo vilivyokosewa na maamuzi yalithibitishwa na pande zote mbili kuthibitisha hilo.

Hivyo baada ya kuafikiana na uamuzi huo, Kakobe aliiomba serikali kufikiria kubadilisha laini na kuziweka katikati ya barabara ya Sam Nujoma kwa kuwa bado anaamini kuwepo kwa madhara ya mitambo yake ya televisheni.

Hata hivyo, Waziri Ngeleja alisema serikali haitaweza kupitisha laini hiyo katikati ya badabara, kwani sehemu hiyo kumesimikwa taa za barabarani na pia inakusudiwa kutumika kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi.

Aliongeza kuwa serikali haiwezi kubadili usanifu wa mradi huo kwa vile hakuna uhakika endapo maombi hayo ya kujenga kituo cha televisheni yatakidhi vigezo vyote ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa masafa.

“Kwa kweli serikali haiwezi kufanya kazi kwa kuhisi, kwani TCRA imethibitisha haijawahi kupokea wala kufanya mchakato wa maombi kutoka kwa kanisa hilo,” alisema Ngeleja.

Alisema BICO katika taarifa yake imeitaka TANESCO kutumia mbinu bora za ujenzi wa laini ya msongo huo, ili kuepukana na kona kali kwenye waya na kutounganisha waya sehemu yoyote kati ya nguzo namba 18 na 19 ambazo ziko kwenye eneo la karibu na kanisa hilo.

Katika taarifa hiyo ya Waziri iliongeza kuwa serikali imetumia shilingi milioni 25 kwa ajili ya kumlipa mshauri mtaalam BICO hadi kukamilika kwa ripoti hiyo ambayo imeweza kuondoa utata uliokuwepo kuhusiana na madai ya kuwepo kwa madhara.

Alisema mradi huo utahakikishwa unamalizika haraka iwezekana kwa kuwa kwa kiasi kikubwa utapunguza kukatika katika kwa umeme kunakosababishwa na uhaba pamoja na uchakavu wa njia za kusafirishia umeme.

Alisema mradi huo unatakwia ukamilike kabla ya Machi 15 mwaka huu, na kusema mrdi huo ukienda kinyume na hapo serikali inaweza ikapata hasara na wafadhili wanaweza wakahitaji fedha zao.

Mgogoro huo ambao ulidumu kwa takribani zaidi ya miezi miwili baina ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kanisa hilo linaloongozwa na Askofu Zakaria Kakobe kubisha kupitisha mradi huo kanisani hapo wka madai unamuathiri.

Na aliamua kutengeneza fulana maalum zinazovaliwa na waumini wa kanisa lake huku wakipiga kambi kanisani hapo kwa saa 24 kwa ajili ya kulinda kukabiliana na wafanyakazi wa TANESCO watakaokwenda kupitisha nguzo hapo.

Katika lindo hilo wafanyakazi wawili wa Tanesco waliweza kujeruhiwa walipofika kanisani hapo kuweka nguzo kupitihsa umeme huo.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment