'Sigara Zimeniua'

Wednesday, March 03, 2010 / Posted by ishak /


Mvuta sigara aliyeteseka miaka mingi kutokana na magonjwa yaliyotokana na uvutaji sigara ametimiziwa matakwa yake kuwa atakapofariki jeneza lake na kaburi lake liweke maneno yanayosema 'Sigara Zimeniua'.
Jeneza la mzee Albert Whittamore lilizungushwa katika mitaa ya mji wake nchini Uingereza huku likiwa limewekewa maneno 'Sigara Zimeniua'.

Mzee Albert aliyefariki mwishoni mwa mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 85, aliacha wosia kuwa atakapofariki kaburi na jeneza lake liwekewe maneno hayo ili kuwaonya vijana wasije wakapoteza maisha yao kama alivyopoteza ya kwake kutokana na magonjwa yaliyotokana na uvutaji sigara.

Mzee Albert aliteseka miaka mingi sana kutokana na matatizo ya mapafu, ugonjwa uliotokana na uvutaji wake uliokithiri wa sigara enzi za ujana wake.

Bango lilitengenezwa na kuwekewa maandishi ya 'Sigara Zimeniua' kabla ya jeneza lake kuzungushwa kwenye mitaa kadhaa ya mji wa Dover uliopo kilomita 160 toka jijini London.

Kwenye kaburi lake nako kuliwekewa bango kama hilo ambalo inasemekana litakaa hapo kwa muda wa wiki moja.

Mzee Albert kabla ya kufariki alikuwa akiwausia vijana kuhusiana na madhara yanayotokana na uvutaji wa sigara.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment