Sugu Awatuhumu Wamarekani Na Ikulu Dar Kwa Kumuingiza Mjini

Wednesday, March 03, 2010 / Posted by ishak /


MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Mbilinyi a.k.a Mr. II au Sugu ameituhumu taasisi moja ya Marekani na Ofisi ya Rais (Ikulu) ya Tanzania kwa kupora haki yake ya kuandaa tamasha la uzinduzi wa mradi wa kampeni ya kuzuia malaria mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku, Sugu alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, tayari amewasilisha malalamiko yake makao makuu ya taasisi hiyo, New York, Marekani kwa kosa la kwenda kinyume na makubaliano ya awali.

Kampeni hiyo ambayo ilizinduliwa Februari 13 kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Jakaya Kikwete, inalenga kuhamasisha jamii kupambana na malaria.

Sugu alisema kilichotokea ni kudhulumiwa wazo lake na Wamarekani hao ambao wameshirikiana na mkurugenzi na maofisa wengine (majina tunayo) wa Tanzania.

Alisema, baada ya kukutana na mmoja wa maofisa hao waliweza kujenga urafiki na alipomtaarifu kuhusu mpango wa asasi yao kutaka kuja nchini kuendesha kampeni kubwa ya kutokomeza malaria, hivyo yeye akamshauri atumie muziki wa Bongo Flava na wasanii wake kufikisha ujumbe.

“Kabla ya hapo, siyo huyu ofisa wala mtu yeyote kutoka kwenye asasi hiyo kule Marekani aliyekuwa akijua lolote kuhusu muziki wa Bongo Flava,” alisema Sugu.

Alisema aliandika mchanganuo na mpango mzima wa namna watakavyotekeleza na kupitishwa na bodi ya asasi hiyo yenye maskani yake Marekani.

Sugu amesema, akiwa katika matayarisho hayo mwaka jana, alilazimika kusitisha masomo yake ya elimu ya juu kwenye chuo alichokitaja kwa jina la Springfield, Massachussetts ili apate muda wa kushughulikia kampeni hiyo ya kutokomeza malaria.

“Kilichotushangaza sisi, baada ya mchakato wote kukamilika na wazo letu kukubalika na bodi ya asasi hiyo kwa miaka miwili, ghafla ulipofika muda muafaka wa kutekeleza mradi huu na kufanya uzinduzi tukajikuta tumeenguliwa,” alisema Sugu.

Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mkurugenzi mmoja wa Tanzania House of Talent (THT), Rugemalira Mutahaba, alisema hawahusiki kwa lolote kuhusu mradi huo ila yeye alihusika kwa kutoa wasanii, vyombo vya muziki na kusema asihusishwe kwa lolote.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment