Maiti za Watu Kuuzwa Kwenye Supermarket Ujerumani

Saturday, April 24, 2010 / Posted by ishak /


Yule daktari bingwa wa mifupa wa Ujerumani ambaye mwaka jana aliandaa maonyesho ya maiti zikifanya mapenzi, ameamua kufungua supermarket ambapo atauza vipande vya miili ya watu.
Baada ya kuandaa maonyesho mwaka jana akizionyesha maiti katika hali mbalimbali za kujamiiana, Dr. Gunther von Hagens wa nchini Ujerumani ameamua kuwauzia watu maiti za watu alizo nazo.

Hagens anafungua supermarket ya maiti za binadamu mjini Guben, Brandenburg, ambayo imepangwa kufunguliwa rasmi mei 28 mwaka huu.

Fuvu la binadamu likiwa limening'inizwa kwenye chuma litauzwa euro 1,200.

Hagens pia ana mpango wa kufungua tovuti ya duka hilo ili aweze pia kufanya mauzo online.

Hagens ambaye anajulikana zaidi kama "Dr Death" (Dokta Kifo), ni mtaalamu maarufu wa elimu ya mwili na viungo vya binadamu na wanyama (Anatomy).

Hagens anatumia njia aliyoigundua yeye mwenyewe inayojulikana kitaalamu kama "plastination" ambapo maiti hutolewa ngozi yote na kisha majimaji yote kwenye maiti kukaushwa.

Hagens hutumia plastiki zilizotengenezwa kwa madini ya silicon kuziweka maiti hizo katika maumbile mbali mbali kuonyesha maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Hagens alisema kuwa maiti anazozitumia kwenye kazi zake ni za watu waliojitolea miili yao kwake kabla hawajafariki. Hagens aliongeza zaidi kuwa yeye mwenyewe ameishajitolea maiti yake itumike namna hiyo akishafariki.

Mwaka jana Hagens aliingia kwenye mzozo mkubwa wakati alipofungua maonyesho mjini Berlin akiyaweka maumbile ya maiti katika staili mbalimbali za kujamiiana.

Miaka miwili iliyopita Hagens alijaribu kufungua duka la kuuza vipande vya miili ya watu lakini alilazimika kuahirisha mpango wake kutokana na upinzani mkubwa toka kwa makanisa na watu mbalimbali.

Safari hii Hagens amesema ameweka nia ya kweli ya kufungua supermarket hiyo ya maiti za binadamu na amesema hatauahirisha mpango wake kwa sababu yoyote ile.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment