Aunguzwa Vibaya Mkono na Mama wa Kambo Kwa Kudokoa Samaki

Tuesday, May 18, 2010 / Posted by ishak /


Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka saba wa wilaya ya Tarime mkoani Mara ameunguzwa vibaya vidole vyote vya mkono wake na mama yake wa kambo baada ya kudokoa samaki aliporudi kutoka shule akiwa na njaa
Polisi wilayani Tarime wamemtaja mtoto huyo kuwa ni Matiko Mwita anayesoma shule ya msingi ya Abainano.

"Mama yake wa kambo alikasirika na kuunguza mkono wake wa kulia kwa moto wa mkaa sababu ikiwa ni kitendo cha mtoto huyo kula kipande cha samaki aliporudi toka shuleni", alisema kamanda msaidizi wa polisi wilaya ya Tarime, Constantine Masawe.

"Nilikuja toka shule na kukuta samaki na ugali lakini mama yangu wa kambo aliponikuta nakula alinuuliza kwanini nakula chakula na ndipo alipoanza kuniunguza na moto mkononi", alisema mtoto Matiko.

Matiko aliungua vibaya vidole vyote vitano vya mkono wake wa kulia kufuatia kitendo hicho cha mama yake wa kambo.

Polisi wanamtafuta mwanamke huyo ambaye alikimbia pamoja na mumewe baada ya suala hilo kufikishwa polisi.

Kamanda Masawe alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Pili Mwita mkazi wa kijiji cha Motana wilayani Tarime mkoani Mara.

"Tunamtafuta pia mumewe kwasababu hakutoa taarifa yoyote polisi mpaka mwalimu wake alipomleta mtoto huyo kituo cha polisi".

Mtoto Matiko baada ya kupatiwa matibabu amepelekwa kwenye kituo cha kulea watoto yatima kilichopo kwenye kijiji cha Gamasara nje kidogo ya Tarime.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment