Mwanafunzi Ajaribu Kuulipua Ubalozi wa Marekani Dar

Wednesday, May 19, 2010 / Posted by ishak /


Mwanafunzi wa shule ya msingi ya Mtambani jijini Dar es Salaam anashikiliwa na polisi baada ya kujaribu kuulipua ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizopatikana zimesema kuwa mwanafunzi huyo ambaye jina lake limewekwa kapuni, anashikiliwa na polisi na kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kujaribu kuulipua ubalozi wa Marekani kwa kutumia bomu la mafuta ya taa.

Mwanafunzi huyo alikuwa na mpango wa kulilipua tanki la mafuta ya dizeli la ubalozi huo ambalo wakati wa tukio lilikuwa na zaidi ya lita 1,000.

Mwanafunzi huyo ambaye umri wake unakadiriwa kuwa kati ya miaka 15 na 17 alikamatwa ndani ya ubalozi huo akiwa na dumu lake la lita tano la mafuta ya taa, utambi na kiberiti.

Mwanafunzi huyo aliingia kwenye ubalozi huo jumapili iliyopita nyakati za usiku kwa kupitia mojawapo ya mageti ya ubalozi huo ambapo walinzi wake walikuwa wamepiga mbonji.

Kelele za koki la tanki la mafuta la ubalozi huo wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akilifungua ndizo zilizowazindua walinzi hao toka usingizini na kumnasa mwanafunzi huyo akiwa kwenye harakati za kulifungua tanki hilo ili alipige moto lilipuke.

Kijana huyo alipohojiwa na walinzi waliomkamata alikiri kutaka kusababisha mlipuko mkubwa ambao ungesababisha uharibifu mkubwa wa mali na kuhatarisha maisha ya watu.

Mwanafunzi huyo alisema kuwa yeye na wenzake walivutiwa na mafunzo ya Al-Qaeda waliyopewa kwa njia ya Video na walitaka kuyafanyia majaribio kabla ya siku ambayo ilipangwa wafanye shambulio kwenye ubalozi huo.

Ubalozi wa Marekani, Dar umethibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini haukutoa taarifa zaidi kwa kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment