Rais wa Nigeria Afariki Dunia

Wednesday, May 05, 2010 / Posted by ishak /


Rais wa Nigeria, Alhaji Umaru Yar'Adua ambaye kiti chake cha urais kimekuwa kikikaliwa na makamu wake kwa miezi kadhaa sasa baada ya rais huyo kuugua ugonjwa wa moyo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 58.
Kwa mujibu wa msemaji wa rais huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake wakati akiongea na shirika la habari la BBC, alisema kwamba rais Yar'Adua amefariki dunia jana jumatano ingawa serikali ya Nigeria bado haijatoa taarifa rasmi.

Rais Yar'Adua alichaguliwa kuwa rais mwaka 2007 lakini kutokana na matatizo ya moyo na figo hajaonekana kwa wananchi wake kwa miezi kadhaa.

Baada ya rais huyo kuugua muda mrefu huku akipatiwa matibabu nchini Saudi Arabia, hatimaye makamu wa rais, Goodluck Jonathan aliteuliwa kushikilia nafasi yake mpaka rais huyo atakapopona.

Taarifa zinasema kuwa rais huyo aliiaga dunia jana jumatano kwenye villa lake nchini Nigeria kwenye majira ya kati ya saa tatu na saa nne usiku kwa saa za Tanzania.

Yar'Adua alienda Jeddah, Saudi Arabia kwaajili ya matibabu mwezi Novemba mwaka jana na alitumia miezi mingi sana huko kiasi cha wapinzani wake na viongozi wa zamani wa Nigeria kumshauri ajiuzulu.

Wakati huo Yar'Adua alimkabidhi mikoba ya urais makamu wake, Goodluck Jonathan lakini hata aliporudi toka Saudi Arabia mwezi februari mwaka huu, Goodluck Jonathan aliendelea kukikalia kiti cha urais.

Taarifa zinasema kuwa baada ya kufariki kwa rais Yar'Adua, makamu wake wa rais ataapishwa rasmi kuwa rais katika siku zijazo.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment