Apanga Kumuua Osama Bin Laden kwa Jambia

Wednesday, June 16, 2010 / Posted by ishak /


Raia mmoja wa Marekani alijaribu kufanya kile ambacho serikali yake imeshindwa kukifanya kwa miaka kadhaa kwa kuamua kwenda peke yake nchini Afghanistan kumsaka na kumuua Osama bin Laden akiwa na bastola, panga na jambia.
Mmarekani Gary Brooks Faulkner mwenye umri wa miaka 52 ametiwa mbaroni nchini Pakistan akiwa kwenye misheni yake ya kumsaka na kumuua kiongozi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden.

Faulkner alitiwa mbaroni jumapili jioni akiwa kwenye harakati za kuvuka mpaka wa Pakistan kuingia Afghanistan ili kukamilisha nia yake ya kumuua Osama ambaye inasemekana amejificha kwenye milima iliyopo kwenye mpaka wa Afghanistan na Pakistan.

Alikamatwa akiwa na bastola moja, panga, jambia na vifaa vya kumwezesha kuona nyakati za usiku. Pia alikuwa na kitabu alichoandika mistari aliyoinukuu toka kwenye biblia.

Faulkner ambaye amebatizwa jina la "American Ninja" na magazeti ya Marekani anasumbuliwa na matatizo ya figo na shinikizo la damu, alikuwa amebeba dawa zake wakati wa safari yake hiyo ya kumsaka Osama.

Faulkner aliwasili nchini Pakistan juni 2 mwaka huu kama mtalii toka California, Marekani. Alipewa mlinzi wa kuongozana naye wakati wa utalii wake lakini alitoweka ghafla jumatatu ya wiki iliyopita na kuwafanya polisi waanze msako wa kumtafuta.

Alikutwa kwenye misitu iliyopo kilomita chache toka mpakani karibu na mji wa Nuristan wa nchini Afghanistan ambao unasemekana ni ngome ya Taliban nchini Afghanistan.

Faulkner aliwaambia polisi kuwa alikuwa kwenye misheni ya kumsaka na kumuua Osama bin Laden.

Alipoulizwa kama anafikiria ana uwezo wa kumkamata Osama, Faulkner aliwaambia polisi "Mungu yuko pamoja nami, nina imani nitamuua Osama bin Laden".

Faulkner aliwaambia polisi kuwa aliamua kwenda mwenyewe kumuua Osama baada ya kuchukizwa na shambulizi la kigaidi la septemba 11, 2001.

Serikali ya Marekani imekuwa ikimsaka Osama bin Laden kwa matukio ya kigaidi duniani na kichwa cha Osama bin Laden kimetengewa zawadi ya dola milioni 25 kwa mtu atakayetoa taarifa za kufanikisha kukamatwa kwake.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment