Mke Amuua Mume Kwasababu ya Kombe la Dunia

Saturday, June 19, 2010 / Posted by ishak /

Kombe la dunia linaloendelea nchini Afrika Kusini limekuwa sababu ya kifo cha mwanaume mmoja nchini humo ambaye alifariki baada ya kupigwa na mkewe na watoto wake wakati alipolazimisha kuangalia mechi kwenye TV wakati mkewe na watoto wake walitaka kuangalia nyimbo za dini.
David Makoeya mwenye umri wa miaka 61 hakutaka kuikosa mechi ya jumapili iliyopita kati ya Ujerumani na Australia.

Mke wake na watoto wake wao walitaka kuangalia programu ya nyimbo za dini za kikristo kwenye luninga.

Polisi wanasema kuwa Makoeya alikuwa akigombania remote control na familia yake ili aweze kuangalia mechi ya kombe la dunia.

Familia yake walikataa kubadilisha channel ya mambo ya dini waliyokuwa wakiiangalia na hapo ndipo mzozo ulipoanzia.

"Alisema, Hapana nataka kuangalia mpira", msemaji wa polisi Mothemane Malefo alisema.

Huku akiwa na hasira, Makoeya alinyanyuka na kuelekea kwenye TV ili aweze kubadilisha channel lakini hakufika mbali kwani mkewe na watoto wake walianza kumshushia kipigo.

Mke wa Makoeya mwenye umri wa miaka 68, Francina, akishirikiana na mtoto wake wa kiume Collin mwenye umri wa miaka 36 na binti yake Lebogang mwenye umri wa miaka 23 walimshushia kipigo cha nguvu baba yao.

"Inaonekana walikipigiza kichwa chake kwenye ukuta, walipiga simu polisi baada ya kumjeruhi vibaya sana... wakati polisi wanafika eneo la tukio, Makoeya alikuwa ameishafariki", alisema Malefo.

Mke wa Makoeya na wanae ambao wanaishi kwenye kijiji cha Makweya, walitiwa mbaroni jumapili usiku.

Binti yake aliachiwa kwa dhamana ya dola 200 wakati mkewe na mtoto wake wa kiume wanaendelea kunyea debe rumande.

Ndugu wa familia hiyo wamesikitishwa na kifo cha Makoeya wakisema kuwa Makoeya hakuwa mtu mwenye vurugu alikuwa mtulivu na mwenye furaha kwa familia yake.

Kifo cha Makoeya kimetokea ikiwa ni siku chache baada ya watoto wawili kufariki nchini Uganda kutokana na moto baada ya wazazi wao kuwaacha wakiwa wamelala na kwenda kuangalia mechi ya kombe la dunia.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment