Miaka 25 Jela Kwa Kuiba Chakula Kanisani

Friday, August 20, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mmoja wa nchini Marekani ambaye alihukumiwa kwenda jela miaka 25 baada ya kujaribu kuiba chakula kanisani, ametoka jela jana baada ya kutumikia miaka 13 jela.
Gregory Taylor, alijaribu kuganga njaa yake kwa kuzamia kwenye jiko la kanisa kwa nia ya kuiba chakula, kitendo chake hicho kiliyafanya maisha yake yaende mrama.

Taylor alikamatwa ndani ya jiko la kanisa na kufunguliwa mashtaka ya wizi ambapo alihukumiwa kwenda jela miaka 25.

Baada ya kutumikia miaka 13 jela, Taylor ameachiwa huru jana baada ya mahakama kuona kuwa adhabu aliyopewa ilikuwa kubwa sana kuliko kosa lenyewe.

Taylor alitupwa jela mwaka 1997 baada ya hakimu wa California kuitumia sheria inayosema kuwa mtuhumiwa anayekamatwa baada ya kufanya uhalifu mara tatu basi atupwe jela kuanzia miaka 25.

Kabla ya tukio la kujaribu kuiba chakula kanisani, Taylor alikuwa akikabiliwa na tuhuma za makosa mawili ya wizi, kosa la kwanza lilikuwa ni kumchomolea mtu pochi lake na kosa la pili lilikuwa ni kujaribu kumpora mtu mali zake.

Taylor alitoka kwenye jela ya wanaume ya mjini Los Angeles jana asubuhi na kulakiwa na ndugu na marafiki.

Taylor aliwaambia waandishi wa habari kuwa sasa amebadilika na anamshukuru mungu kwa kumpa chansi ya pili.

Alisema kuwa ana mpango wa kufanya kazi kwenye mgahawa wa kaka yake ili aweze kuwasaidia watu wengine wanaotafuta chansi ya pili katika maisha.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment