Msiba Juu ya Msiba

Monday, August 23, 2010 / Posted by ishak /


Baba na mama mmoja wa nchini Ufaransa walipigwa na mshtuko wa ghafla wakati walipofika makaburini kwaajili ya mazishi ya ndugu yao na bila kutarajia kuliona kaburi la mtoto wao waliyekuwa wakijua yuko hai na mwenye afya njema.
Kwa mujibu wa gazeti la La Voix du Nord la nchini Ufaransa, Josiane Vermeersch na mkewe Elie Langlet walifika kwenye makaburi ya Hellemmes mjini Lille kaskazini mwa Ufaransa kwaajili ya mazishi ya kaka yake Ellie.

Lakini wakati wakiondoka makaburini baada ya mazishi, mmoja wa wanafamilia aliona bango juu la kaburi likiwa na jina la mtoto wao likisomeka "Olivier Langlet, 1968-2010".

Kwa mshangao mkubwa wanafamilia waliwasiliana na uongozi wa makaburi hayo ili kujua undani wa suala hilo.

Uchunguzi wa haraka haraka wa kaburi hilo ulithibitisha kuwa marehemu alikuwa ni mtoto wa kiume wa familia hiyo ambaye alikuwa akiishi umbali wa kilomita tano tu toka nyumbani kwa baba na mama yake. Taarifa zaidi zilisema kuwa alikutwa amefariki nyumbani kwake kutokana na maradhi.

Josiane na mkewe waliviambia vyombo vya habari kuwa walikuwa wakijua mtoto wao yu hai na mwenye afya njema na walijaribu kumtafuta bila mafanikio kumpa taarifa ya msiba wa mjomba wake.

"Hatukuamini macho yetu baada ya kuona kaburi lake, ghafla tulianza kuangua kilio", walisema wanafamilia hao.

Familia hiyo ilisema kuwa haikupewa taarifa ya kifo cha mtoto wao ambaye alizikwa kinyemela bila ndugu zake kujulishwa.

Vyombo vya habari vya Ufaransa, vimelaani uzembe uliofanyika wa kutoijulisha familia yake hasa zama hizi za teknolojia ambapo njia za mawasiliano zimekuwa nyingi sana.

"Alienda kumzika kaka yake akakutana na kaburi la mtoto wake", lilisema gazeti moja la nchini humo kuelezea tukio hilo ambalo limezua mjadala mrefu.

Polisi wa Ufaransa wanachunguza kwanini polisi na maafisa wa mazishi hawakuwapa taarifa wazazi na ndugu wa marehemu kabla ya kumzika mtoto wao.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment