Aichana Quran na Biblia na Kuzivutia Sigara Kurasa Zake

Wednesday, September 15, 2010 / Posted by ishak /



Mwanasheria mmoja wa nchini Australia amezua balaa jingine baada ya kuzichana kurasa za kwenye msahafu na biblia na kuzitumia kurasa hizo kuvutia sigara.
Siku chache baada ya mchungaji wa Marekani kuzua mtafaruku duniani baada ya kutishia kuichoma moto Quran, mwanasheria mmoja wa nchini Australia amezua mtafaruku mwingine kwa kuzichana kurasa za kwenye msahafu na kwenye biblia na kisha kuzitumia kurasa hizo kuvutia sigara.

Mwanasheria huyo aliyejulikana kwa jina la Alex Stewart, aliandaa video ya dakika 12 ambayo aliiweka kwenye YouTube akiwa ameshikilia msahafu na biblia kabla ya kunyofoa kurasa kwenye vitabu hivyo vitakatifu na kuzitumia kuvutia sigara.

Stewart ambaye hana dini alisema katika video hiyo "Hivi ni vitabu tu kama vitabu vingine".

Video yake ilifutwa kwenye YouTube muda mfupi baada ya kuwekwa baada ya watu kuanza kuilaani video hiyo.

Stewart ambaye anafanya kazi kwenye chuo kikuu cha Queensland University of Technology amesimamishwa kazi kwa muda na chuo hicho ambacho kimesema kuwa kimesikitishwa sana na kitendo chake.

"Chuo kikuu kimesikitishwa sana na hakijafurahia kitendo kama hiki kutokea", alisema makamu mkuu wa chuo hicho Peter Coaldrake.

Kitendo cha Stewart kimefuatia tukio la mchungaji Terry Jones wa Florida, Marekani kutishia kuchoma moto misahafu 200 siku ya septemba 11.

Aliahirisha azma yake hiyo kutokana na vitisho toka kwa waislamu na shinikizo kubwa toka kwa serikali ya Marekani.

Hata hivyo wachungaji wawili wa jimbo la Tennessee nchini Marekani, mchungaji Bob Old na msaidizi wake Danny Allen waliichoma moto Quran na kitabu chenye maandishi ya "Muhammad" kwenye ukurasa wake wa mbele.

Mjini Washington, mwanaume mmoja aliichana Quran mbele ya jengo la ikulu ya Marekani na kukiweka kipande cha ukurasa alichokinyofoa kwenye mfuko wa plastiki.

Tukio hilo lilishuhudiwa na watalii waliokuwa maeneo hayo pamoja na polisi wanaolinda usalama eneo hilo ambao hawakuchukua hatua yoyote ili kuepuka kuingilia haki za watu za uhuru wa kujieleza.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment