Kitabu cha Mafunzo ya Wizi

Tuesday, November 30, 2010 / Posted by ishak /


Mwizi wa nchini Japan ambaye kutokana na kufanya wizi kwa mwaka alikuwa akijiingizia kiasi cha pesa sawa na Tsh. Milioni 540 ametoa kitabu cha kuelezea jinsi ya kuiba kwenye majumba ya watu bila kugundulika, kitabu hicho kimekuwa gumzo nchini Japan na kinanuliwa kwa wingi.
Mwizi wa nchini Japan, Hajime Karasuyama kutokana na utaalamu wake wa kuiba kwenye majumba ya watu, ametoa kitabu kinachoelezea jinsi ya kuiba kwa ustadi mkubwa bila ya kugundulika.

Kitabu chake kinachoenda kwa jina la "Kazi: Mwizi, Kipato Kwa mwaka: Yen Milioni 30", kimekuwa gumzo nchini Japan na kimekuwa kikinunuliwa kama njugu.

Wachapishaji wa kitabu hicho Futabasha Publishing wamesema kuwa nakala za mwanzo za kitabu hicho zipatazo 10,000 zimenunuliwa zote ndani ya siku 10 baada ya kitabu hicho kuzinduliwa.

Katika kitabu hicho, Karasuyama anaelezea jinsi ya kufungua vitasa vya milango ya aina yoyote ile kwa muda mfupi na bila ya ufunguo na jinsi ya kuvunja madirisha ya vioo bila ya kusababisha kelele.

Karasuyama ameelezea pia jinsi alivyokuwa akitumia lensi kuangalia ndani ya nyumba kwa kupitia kwenye tundu la funguo.

Mbali ya wizi wa majumbani, Karasuyama pia amelezea pia njia za kufanya utapeli na kuwaacha watu kwenye mataa.

Karasuyama alisema kuwa kutokana na wizi alikuwa akijiingizia kitita kinono kwa mwaka zaidi ya Tsh. Milioni 540.

"Tunapoingia ndani ya nyumba, sisi wezi huwa tunajua wapi watu huficha pesa zao", alisema Karasuyama alipokuwa akiongea na jarida la Shukan Taishu kuhusiana na kitabu chake ambacho kimeambatanisha maneno ya "Usijaribu kuniiga" kwenye ukurasa wake wa kwanza.

Wachapishaji wa kitabu hicho kinachouzwa Yen 1,200 sawa na Tsh. 20,000 wamekanusha madai kuwa kuchapishwa kwa kitabu hicho kutapelekea baadhi ya watu kugeuka wezi kwa kuiga staili za wizi za Karasuyama.

Wachapishaji hao wamesema kuwa kitabu cha Karasuyama kitawawezesha watu kujifunza njia zinazotumiwa na wezi hivyo kuweza kuzilinda vyema nyumba zao.

source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment