Thamani ya Shilingi ya Tanzania yapanda

Sunday, December 19, 2010 / Posted by ishak /


Thamani ya Shilingi ya Tanzania imepanda mfululizo kwa muda wote wa wiki mbili zilizopita tokea Desemba 3 Mwaka huu ukilinganisha na Dola ya Kimarekani.
Kwa mujibu wa takwimu zinazotolewa kila siku na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kiwango cha kubadilisha fedha Desemba 2, kilikuwa Shilingi 1,487.55 kwa Dola moja, lakini Desemba 3, kilishuka na kufikia Shilingi1,485.23 upungufu wa shilingi 2.32.
Hadi kufikia Desemba 10, Dola ilibadilishwa kwa shilingi 1,477.22, pungufu kwa shilingi 8.01 ikilinganishwa na kiwango cha ubadilishanaji wa shilingi kwa dola wa Desemba 3 uliokuwa shilingi 1,485.23.
Kuanzia Desemba 13 hadi jana thamani ya Shilingi ilipanda kwa kasi kubwa ambapo Desemba 13 dola ya Kimarekani ilibadilishwa kwa Shilingi1,466.23, Desemba 14 ilibadilishwa kwa Shilingi 1,455.72, Desemba 15 ilibadilishwa kwa Shilingi 1,443.39 na jana dola ilibadilishwa kwa Shilingi1,432.42.
Hivyo takwimu hizi za Bot zinamaanisha kuwa thamani ya fedha yetu imeimarika ukilinganisha na dola ya Kimarekani kwa kipindi hiki cha wiki mbili zilizopita.
Kupanda huku kwa thamani ya shilingi mfululizo unakinzana na namna ilivyoporomoka kwa haraka mwanzoni mwa Agosti wakati harakati za uchaguzi zilipoanza hadi kura zilipopigwa na kuendelea hivyo hadi mwanzoni mwa mwezi huu.

source nipashe

0 comments:

Post a Comment