11 Wafariki Wakisherehekea Mwaka Mpya Nigeria

Saturday, January 01, 2011 / Posted by ishak / comments (0)


Zaidi ya watu 11 wamefariki dunia nchini Nigeria kufuatia bomu kubwa lililolipuka kwenye baa wakati watu wakisherehekea mwaka mpya.
Zaidi ya watu 11 wamefariki dunia kufuatia bomu kubwa lililolipuka kwenye baa iliyopo karibu na kambi ya jeshi iliyopo karibu na ikulu mjini Abuja.

Eneo hilo lilikuwa likisemekana kuwa ndilo lenye usalama kuliko maeneo yote ya mji wa Abuja.

Wakati wa krismasi wiki iliyopita zaidi ya watu 80 walifariki dunia nchini Nigeria kutokana na milipuko ya mabomu katika mji wa Jos ambao umekumbwa na chuki ya kidini kati ya waislamu na wakristo.

Katika bomu lililotokea mkesha wa mwaka mpya, inakadariwa kuwa watu 30 wamepoteza maisha yao ingawa taarifa ya polisi ilithibitisha vifo vya watu 11.

Bomu hilo lilitokea muda mfupi kabla ya mwaka mpya wakati watu wakiwa wanajiburudisha baa wakisubiri kusherehekea mwaka mpya 2011.

Waziri wa ulinzi wa Nigeria amewataka watu wadumishe utulivu wakati uchunguzi mkali ukiendelea kuhusiana na milipuko ya mabomu ambayo imekuwa ikiiandama Nigeria siku za karibuni.

source nifahamishe

Auanza Mwaka Mpya Vibaya Kwa Operesheni ya Kuongeza Makalio

Saturday, January 01, 2011 / Posted by ishak / comments (0)


Mwanamke mmoja wa nchini Marekani ambaye alitaka kuingia mwaka 2011 akiwa mrembo zaidi na mwenye makalio makubwa amefariki dunia masaa matatu baada ya kufanyiwa operesheni ya kuongeza makalio.
Mwaka 2011 umeanza vibaya kwa bwana Osvaldo Vargas mkazi wa Florida, Marekani, Amempoteza mke wake ambaye operesheni ya kuongeza urembo na makalio ili aonekane mrembo zaidi mwaka 2011 ilimalizika vibaya na kupelekea kifo chake.

Lidvian Zelaya mwenye umri wa miaka 35 alitaka kuingia mwaka 2011 akiwa mrembo zaidi kwa kuamua kufanya operesheni ya kutoa nyama nyama na mafuta toka kwenye tumbo lake na kuzihamishia kwenye makalio yake ili kuyafanya yawe makubwa zaidi.

Masaa matatu baada ya operesheni hiyo, Lidvian aliwahishwa hospitali akiwa amezidiwa sana na wakati mume wake anawasili hospitali Lidvian alikuwa ameishafariki dunia.

"Amefariki akitafuta urembo, kwangu mimi alikuwa tayari ni mrembo", alisema mume wa Lidvian kwa huzuni.

"Alikuwa ni mrembo, mwenye furaha na aliyependa kudansi, nataka kujua nini kimetokea", alisema bwana Oswaldo wakati akiongea na waandishi wa habari.

"Hatumlaumu yeyote lakini tunataka kujua nini kimesababisha kifo chake", alisema Oswaldo akiwa pamoja na mwanasheria wake.

Lidvian alifanyiwa operesheni kwenye kliniki ya Strax Rejuvenation, ya Florida, hata hivyo kliniki hiyo imesema kuwa sheria zinawabana kusema chochote kuhusiana na kifo cha Lidvian.

source nifahamishe

Babu wa Miaka 83 Amuua Mkewe Kwa Kumshindilia Bisibisi Kichwani

Wednesday, December 29, 2010 / Posted by ishak / comments (0)

Babu mwanablogu mzee wa nchini Taiwan mwenye umri wa miaka 83 amemuua mkewe mwenye umri wa miaka 80 kwa kumshindilia bisibisi kichwani na kisha kuweka maelezo jinsi alivyofanya mauaji hayo kwenye blogu yake.
Babu Wang Ching-hsi mwenye umri wa miaka 83 wa nchini Taiwan kutokana na huruma yake aliamua kuyamaliza maisha ya mkewe mgonjwa wa kansa kwa kuizamisha bisibisi kwenye kichwa chake.

Kabla ya kufanya mauaji hayo, Babu Wang aliandika kwenye blogu yake kuwa hali ya mkewe imezidi kuwa mbaya na amepoteza hamu ya kuendelea kuishi duniani.

Babu Wang alimpa mkewe dawa za usingi na alipopitiwa na usingizi alimuua kwa kuizamisha bisibisi kwenye fuvu lake la kichwa.

Kwa mujibu wa magazeti ya Taiwan, Wang alipiga simu polisi kuwapa taarifa kuwa amemuua mkewe na alikaa nje ya nyumba yake akiwasubiri polisi wafike.

"Kwanini nimemuua mke wangu?, majibu yote yapo kwenye blogu yangu", alisema Wang akiwaambia waandishi wa habari wakati akiingizwa kwenye karandinga la polisi.

Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa, Wang alikubaliana na mkewe miaka kumi iliyopita kuwa kila mmoja wao afariki kwa amani muda utakapofika.

Katika makubaliano hayo, Wang alimwambia mkewe, "Muda utakapofika nitakuua".

Kumekuwa na mjadala mkubwa nchini Taiwan kuhusiana na haki ya mtu aliyechoka kuishi kusitisha maisha yake.

Mwezi juni mwaka huu, baraza la kutunga sheria la Taiwan lilipitisha sheria ya kuwaruhusu wagonjwa na ndugu wa mgonjwa aliyekuwa mahututi kwa magonjwa yaliyofikia kikomo, kusitisha kuwapa dawa au huduma za kurefusha maisha yao ili kuwaepusha na mateso wanayopata.


source nifahamishe

Jela Miaka Mitano Kwa Kusoma Email ya Mkewe

Wednesday, December 29, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mwanaume mmoja wa nchini Marekani ambaye alifungua email ya mkewe na kugundua kuwa mkewe alikuwa akifanya mapenzi nje ya ndoa, anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela.
Leon Walker mwenye umri wa miaka 33 mkazi wa Michigan nchini Marekani anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela kwa kufungua na kusoma email za mkewe.

Leon alifungua email ya mkewe, Clara Walker, kwa kutumia kompyuta waliyokuwa wakiitumia pamoja nyumbani kwao.

Kwa kutumia password yake, Leon alifungua akaunti ya Gmail ya mkewe na alisoma email zake ambapo aligundua kuwa mkewe alikuwa akitembea nje ya ndoa.

Mkewe alikasirika baada ya siri hiyo kufichuka na aliamua kufungua kesi ya madai ya talaka ambapo pia alimfungulia Leon mashtaka ya kusoma email zake.

"Hii ni kesi ya kustaajabisha, hakuna sheria inayoweka wazi suala kama hili", alisema mwanasheria Frederick Lane.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hii ni mara ya kwanza sheria dhidi ya wizi wa nyaraka za siri kwenye masuala ya kibiashara inatumika kwenye masuala ya kifamilia.

Baadhi ya wanasheria wanasema kuwa huenda Leon akahukumiwa kwenda jela miaka mitano iwapo atapatikana na hatia ya kutumia password ya mkewe kusoma email zake.

Leon akiongea na waandishi wa habari alisema kuwa alichungulia email za mkewe ili aweze kujua chanzo cha mkewe kuwatelekeza watoto wao.

Kesi ya Leon itaanza kusikilizwa februari 7 mwakani.

source nifahamishe