Binti wa Osama bin Laden Akiri Baba Yake Ameuliwa

Thursday, May 05, 2011 / Posted by ishak /


Osama bin Laden

Mtoto wa kike wa Osama bin Laden amesema kuwa baba yake alikamatwa akiwa hai kabla ya kuuliwa kwa kupigwa risasi mbele yake na wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani.
Televisheni ya Al-Arabiya iliwanukuu maafisa usalama wa ngazi za juu wa Pakistan wakisema kuwa binti huyo wa Osama mwenye umri wa miaka 12, aliwaambia kuwa baba yake aliuliwa mbele ya familia yake na kisha mwili wake kuburuzwa hadi kwenye helikopta ya Marekani.

Mwili wa mtoto wa kiume wa Osama nao ulichukuliwa na wanajeshi wa Marekani na kupakizwa kwenye helikopta.

Televisheni ya Al-Arabiya iliwanukuu maafisa usalama wa Pakistan wakisema kuwa watoto sita wa Osama bin Laden, mmoja wa wake zake na mwanamke mmoja toka Yemen ambaye inasemekana alikuwa daktari wake walisafirishwa hadi kwenye mji wa Rawalpindi karibu na mji wa Islamabad, kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya jeshi.

"Hivi sasa wanapatiwa matibabu kwenye hospitali ya jeshi ya Rawalpindi" alisema mmoja wa Maafisa usalama wa Pakistan na kuongeza kuwa mke wa Osama bin Laden aliwaambia kuwa wamekuwa wakiishi Abbottabad kwenye nyumba hiyo kwa miezi sita sasa.

Afisa mwingine wa ngazi za juu wa Pakistan alisema kuwa baadhi ya taarifa zilizotolewa na Marekani kuhusiana na kukamatwa na kuuliwa kwa Osama hazina ukweli ndani yake.

"Hakuna hata risasi moja iliyopigwa toka kwenye nyumba ya Osama, ndege yao ya kivita ilipata matatizo ya kiufundi angani na ilianguka kwenye eneo la tukio".

Maafisa usalama wa Pakistan walisema kuwa hawakukuta silaha yoyote wala mabomu wakati walipofanya msako wa nguvu ndani ya nyumba ya Osama baada ya maiti yake kuchukuliwa na Marekani.

Uchunguzi wa kwanza ulifanyika jumatatu na jumanne walirudia kufanya msako kwenye nyumba hiyo yenye vyumba 13. Walichokuta ndani ya nyumba ya Osama ni nyati wawili, ng'ombe mmoja na kuku wapatao 150.

"Kulikuwa hakuna handaki wala sehemu maalumu ya kujificha ndani ya nyumba hiyo, ndio maana sielewi kwanini mtu anayetafutwa kuliko watu wote duniani alienda kuishi pale", alisema afisa huyo wa Usalama wa Pakistan.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment