Wanajeshi Wa Kikosi Kilichomuua Osama bin Laden Wauliwa

Wednesday, August 10, 2011 / Posted by ishak /

NewsImages/5870762.jpg

Wanajeshi wa Marekani wapatao 22 toka kikosi cha Seal Team Six kilichotumika kumuua Osama bin Laden wamefariki dunia baada helikopta waliyokuwemo kutunguliwa na makombora ya Taliban nchini Afghanistan.
Jeshi la Marekani limepata pigo kubwa sana la mwaka baada ya kupoteza jumla ya wanajeshi 31 wakiwemo wanajeshi 22 toka kikosi maalumu cha Seal Team Six ambacho wanajeshi wake walitumika katika shambulio la kumuua kiongozi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden.

Seal Team Six ni kikosi maalumu cha makomandoo wa Marekani ambacho ndicho kilichotumika kuivamia nyumba ya Osama bin Laden nchini Pakistan na kumuua kiongozi huyo wa Al-Qaeda.

Taarifa iliyotolewa ilisema kwamba helikopta ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa imewabeba wanajeshi 31 wa Marekani pamoja na makomandoo saba wa Afghanistan ilitunguliwa na makombora ya wanamgambo wa Taliban.

Kuuliwa kwa wanajeshi wengi wa Marekani ndani ya siku moja ni pigo kubwa sana kwa jeshi la Marekani katika vita hivyo vya Afghanistan ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa takribani miaka 10 sasa.

Mmoja wa maafisa wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba helikopta hiyo ya kijeshi ya Marekani ilitunguliwa na Taliban kwenye mji wa Wardak usiku wa siku ya ijumaa.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba helikopta hiyo ilitunguliwa wakati ilipokuwa ikifanya shambulizi kwenye maeneo yanayotawaliwa na Taliban kwenye mji wa Wardak.

"Tulikuwa nyumbani usiku wakati tulipoona helikopta ikitua juu ya paa la jumba la kamanda wa Taliban na mara risasi zilianza kuvurumishwa toka pande zote mbili", alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Mohammad Saber.

Saber aliongeza kuwa helikopta hiyo iliamua kuondoka toka eneo hilo lakini ghafla ilidondoka chini na kulipuka.

Msemaji wa Taliban, Zabiullah Mujahid alisema kwamba wanamgambo wa Taliban ndio waliyoiangusha helikopta hiyo kwa kombora.

Pia Mujahid alibainisha kuwa wanamgambo wanane wa Taliban waliuliwa wakati wa shambulio hilo.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment