MAZINGIRA USIYOTAKIWA KABISA KUANZISHA UHUSIANO KIMAPENZI

Tuesday, June 07, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Wengi kati ya watu ambao hukumbwa na majuto ya “ningejua nisingemkubali” ni wale wanaoanzisha uhusiano wa kimapenzi kwenye mazingita yasiyostahili.
Wataalamu wa mapenzi wanasema, penzi sahihi lazima liambatane na wakati muafaka wa kufanya hivyo. Ukikosea katika kupima mazingira unakuwa kwenye asilimia 80 za kuchagua mtu asiyekufaa maishani mwako.
Leo kwa kutambua umuhimu wa mada hii nimeona niwaletee mazingira ambayo hayafai mtu kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, lengo langu likiwa ni kuweka umakini katika kuchagua na kuondoa, kupunguza majuto ya kuumizwa na mapenzi.


KWENYE MGOGORO
Uchunguzi unaonesha kuwa asilimia 60 -70 ya wapenzi huanzisha uhusiano mpya wa kimapenzi nyakati za migogoro baina ya wapendanao kwa lengo la kupoza maumivu.
Msomaji wangu, ni jambo la hatari sana kuanzisha uhusiano kwenye mazingira ya mgogoro kwani utakapofanya hivyo utapoteza umakini na hivyo kujikuta ukijiingiza kwenye uhusiano usiokuwa na faida ya baadaye kwako.

UKIWA NA HISIA KALI
Kama binadamu kamili kuna wakati tunakuwa kwenye msukumo mkubwa wa hisia za kimapenzi, kila umuonaye anaweza kukushawishi si kwa sababu anakufaa lakini njaa ya penzi isiyohitaji kuchagua itakuwa inakusukuma kujishibisha hata kwa maganda.
Epuka kabisa kusukumwa na mhemko wa mwili, usikubali kuwa mtumwa wa hisia kwani utajikuta umempa penzi mtu ambaye hata wenzako watashangaa jinsi ulivyoangukia pua.

UNAPOKUWA UMELEWA
Mazingira ya ulevi ni hatari sana, watu wengi hufanya ngono zembe bila kuangalia madhara yake wakati wakiwa wamelewa. Nashauri kwamba, unapokwenda baa jambo la kwanza kabisa unalotakiwa kulihifadhi kwenye akili yako ni kutojiingiza kwenye uhusiano mpya wa kimapenzi.

Katika maisha yangu ya ushauri nimekutana na watu wengi sana wakikiri kuambukizwa magonjwa ya zinaa walipokuwa wamelewa.
Nakushauri msomaji wangu kwamba, usikubaliane kabisa ulevi ukuingize kwenye masuala la kimapenzi. Acha starehe ya pombe pekee ikifurahishe, ukitaka vyote utaamka umefanya jambo la ajabu litakalokuhuzunisha maisha yako yote.

SIKU ZA UPWEKE
Nafahamu kuwa, harakati za kimaisha huwatengenisha wapenzi na kujikuta wakiwa wapweke kwa muda. Kipindi hiki kinaweza kuwa cha mwenza kwenda masomoni au safari ya kikazi. Ni kipindi cha kujaribiwa imani.

Jambo baya kabisa ni kuona, eti wapenzi waliotenganishwa na changamoto za kimaisha kujiona wapweke na kuamua kutafuta wachezaji wa nje wawasaidie kumaliza upweke.
Wapenzi wengi walijikuta kwenye majuto baada ya kujiingiza kwenye uhusiano na watu ambao kimsingi hawaendani nao ila kwa lengo moja tu la kuwaondolea upweke, matokeo yake kufumaniwa na jamii kuwashangaa kwa kutokuwa wavumilivu.

MSUKUMO WA MKUMBO
Ninaposema msukumo wa mkumbo namaanisha nyakati ambazo rafiki zako watakupitia kwenda disko, mkifika huko bila kupanga kila mtu anakuwa na wake, wewe unajikuta peke yako unalazimika kumkubali aliyebaki nawe kwa lengo la kuogopa kuonekana huna mtu wa kujirusha naye. Baadaye unajikuta kwenye majuto makubwa.


source globalpublishers