
Mwanamke wa nchini Marekani ambaye alitandikwa risasi ya kifua baada ya kujifanya amefariki, alinusurika maisha yake kutokana na matiti ya bandia aliyoyapandikiza kwa operesheni miaka kadhaa iliyopita.
Lydia Carranza alikuwa kazini kwake kwenye zahanati ya meno mjini California wakati mume wa mfanyakazi mwenzake alipovamia kwenye zahanati hiyo.
Mwanaume huyo alikuwa amebeba bunduki na alifika kwenye zahanati hiyo akiwa na lengo moja tu la kumuua mkewe ambaye alikuwa akidai talaka.
Kaka wa mke wa mwanaume huyo ambaye naye anafanya kazi kwenye zahanati hiyo aliingilia kati akitaka kusuluhisha mambo lakini alitandikwa risasi ya tumbo na mwanaume huyo.
Baada ya hapo mwanaume huyo alimgeukia mkewe na kuanza kumpiga risasi kadhaa mpaka alipohakikisha amemuua.
Ndipo sasa zamu ilipomuangukia Coranza na wafanyakazi wenzake. Coranza alitandikwa risasi kwenye mkono wake wa kulia, alipojifanya amefariki mwanaume huyo alimsogelea na kumtandika risasi nyingine ya kifua.
Coranza ambaye ni mama wa watoto watatu alinusurika maisha yake kutokana na matiti ya bandia ya silicone aliyojipandikiza miaka kadhaa iliyopita kuhimili kishindo kikubwa cha risasi hiyo.
Miaka michache iliyopita Coranza alifanya operesheni ya kuongeza ukubwa wa matiti yake kutoka saizi B hadi saizi D.
"Ana bahati sana, risasi ilibakia milimita chache sana kuufikia moyo wake na ogani zake muhimu, kama angekuwa hajafanya operesheni ya kuongeza matiti, tusingekuwa tunaongea hivi sasa", alisema Dr. Ashkan Ghavami wa zahanati hiyo alipokuwa akiongea na gazeti la Los Angeles Times.
Jaime Paredes, mwanaume aliyefanya mashambulizi hayo ya risasi alikamatwa na anasubiria kupandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka mbali mbali yakiwemo mashtaka ya mauaji ya mkewe.
source nifahamishe

Rais Barack Obama wa Marekani ametakiwa aache kuvuta sigara na daktari wake.
Rais Obama ametakiwa na daktari wake aache kabisa kuvuta sigara kwaajili ya afya yake mwenyewe.
Obama aliambiwa hivyo baada ya vipimo vya kwanza vya afya yake tangia alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani kuonyesha kuwa ana afya njema sana na yupo fiti kulitumikia taifa lake.
Daktari binafsi wa Obama, Jeffery Kuhlman alisema kuwa vipimo vya afya ya Obama vimeonyesha kuwa Obama atakuwa mwenye afya njema kipindi chote cha urais wake.
Dr. Kuhlman alimshauri Obama aendelee na jitihada zake za kujizuia kuvuta sigara ili aiche kabisa tabia ya kuvuta sigara.
Rais Obama mwenye umri wa miaka 48, amekuwa akijitahidi kujizuia kuvuta sigara mbele za watu na amesema kuwa siku hizi huwa havuti sigara mbele ya familia yake.
Enzi zake kabla ya urais, Obama alikuwa mvutaji mkubwa sana wa sigara na kuna wakati Michelle Obama alinukuliwa na jarida moja la Marekani akielezea kukerwa na uvutaji sigara wa Obama.
Rais Obama alimuahidi mkewe kuwa akishinda urais ataacha kabisa kuvuta sigara lakini alikiri kuwa amekuwa akivuta sigara siku moja moja tangia alipoingia ndani ya ikulu ya Marekani.
Mwaka jana rais Obama alisema kuwa amefanikiwa kujizuia kuvuta sigara kwa asilimia 95.
source nifahamishe
Ajali Ya Ndege Yaizuia The Cranes Kutua Mwanza

TIMU ya soka ya taifa ya Uganda, The Uganda Cranes, jana ilishindwa kuwasili jijini Mwanza kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa jijini humo kutokana na ajali ya Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku, katika ajali hiyo, watu wote waliokuwamo katika ndege hiyo wakati ikijiandaa kutua ikitokea Dar es Salaam, wamenusurika lakini uwanja ukifungwa kwa sababu za kiusalama zaidi.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737 yenye namba SH-Mvz, ilipata ajali hiyo jana majira ya saa 1:45 asubuhi; wakati ikitua tairi zake mbili zilipasuka na kusababisha kuacha njia yake huku injini moja ya kushoto ikiingiliwa maji.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, wakati ndege hiyo ikitua uwanjani hapo kulikuwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha ghafla kilisikika kishindo kikubwa kilichowashtua.
Akizungumza na gazeti moja la kila siku, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, alisema kutokana na kufungwa kwa uwanja huo kwa siku ya jana, Uganda Cranes walishindwa kuwasili kama ilivyokuwa imepangwa.
Mwakalebela alisema baada ya ajali hiyo, TFF iliwasiliana na Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) wakiwataka kusitisha safari yao kwa jana ili kuepuka usumbufu hadi leo tayari kwa mechi ya kirafiki itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa CCM- Kirumba.
Alisema pamoja na tatizo hilo, maandalizi ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na kusema vijana wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, wamejiandaa vizuri kwa mechi hiyo.
Mwakalebela alisema mechi hiyo ni muhimu zaidi kwa Stars kwa ajili ya kujiandaa na kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani (CHAN).
Stars itaanza kampeni yake dhidi ya Somalia, mechi itakayopigwa Machi 13 kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam.
source nifahamishe
Ahadi nyingine ya kurudi umeme Zanzibar yatolewa
MEDAIWA jana kuwa huduma ya umeme visiwani Zanzibar inatarajiwa kurudi Machi 9 baada ya kukamilika kazi za utengenezaji wa kituo cha kupokea umeme kilichopo Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi
Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Hassan Ali Mbarouk, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na kukamilika kwa matengenezo cha Fumba huduma hiyo itarejea punde na kuwaahidi wananchi wasiwe na wasiwasi huduma hiyo itarejea siku hiyo.
Alisema kazi iliyobakia ni kuunganisha waya za umeme kutoka nchi kavu na baharini na kazi hiyo ya kuunganishwa kwa waya kutoka katika vituo vya Fumba hadi Ras Kiromoni Tanzania Bara itachukua muda wa siku tatu.
Alisema hadi Jumapili ijayo kazi ya matengenezo itakuwa imemalizika na matarajio Machi 8 kutafanyika vipimo vya majaribio na Machi 9 ndiyo huduma hiyo inatarajiwa kuwashwa na kurudi rasmi kwa umeme visiwani humo.
Pia aliweza kuwaambia waandishi wa habari kuwa kuchelewa kwa huduma hiyo kumesababishwa na mafuta yaliyokuwemo ndani ya waya zinazoleta umeme kutokuwa safi na kulazimika kusafishwa kwa muda wa siku tatu.
Wakazi wa visiwani humo wamekosa huduma hiyo ya umeme tangu Desemba mwaka jana, baada ya kutokea hitilafu katika kituo cha kupokea umeme huo kutoka Ras Kiromoni hadi Fumba mjini Unguja
source nifahamishe
BASI moja la abiria la kampuni ya Abood jana liliteketea kwa moto lote katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo.
Basi hilo likiwa kituoni hapo lilianza kuweaka moto ghafla na kupelekea mali zote vikiwemo na viti kuteketea kwa moto huo.
Ilidaiwa kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotoka katika gari hilo.
Hata hivyo kikosi cha zima moto kilichelkewa kufika eneo la tukio na kukut gari hilo liko katika hatua za mwisho kuteketea
Basi hilo leo lilikuwa linatarajiwa lifanye safari zake kuelekee mkoani Tunduma.
source nifahamishe
Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limesema haifahamiki huduma ya umeme itarejea lini visiwani humu kwa vile mafundi kutoka ulaya wanaendelea na matengenezo katika kituo cha Fumba Zanzibar na Ras Kilomoni, Tanzania bara.
Hayo yameelezwa na meneja wa shirika hilo, Hassan Ali Mbarouk, alipokuwa akizungumza na Nipashe baada ya kutakiwa kueleza ni lini huduma ya umeme inatarajia kurudi. Zanzibar iliingia gizani tangu Desemba 10 mwaka jana.
Awali Waziri wa Maji, Nishati na ardhi Mansour Yusuf Himid, alitangaza kuwa huduma ya umeme Zanzibar ilitarajia kurejea Februari 20 kufuatia kuwasili kwa mafundi toka Afrika Kusini na Ulaya.
Meneja huyo wa Zeco alisema jana kazi ya matengenezo katika kituo cha Ras Kilomoni Tanzania bara imeshafanyika kwa asilimia 98 tangu walipoanza matengenezo hayo.
“Mafundi bado wanaendelea na matengenezo na ni mapema kueleza lini umeme utarejea na kabla ya kufanya hivyo ni lazima nishauriane na wakubwa wangu,” alisema meneja huyo na kuongeza kuwa kazi ya matengenezo inandelea vizuri.
Meneja huyo alisema kazi iliyobakia katika kituo cha Ras Kilomoni Tanzania bara ni kuunganisha bomba maalum katika kituo hicho kinachopokea umeme toka Kidatu kabla ya kusafirishwa Zanzibar kupitia waya uliotandikwa chini ya bahari.
Aidha, alisema kwamba katika kituo cha Fumba, mafundi toka Ulaya na wazalendo wanaendelea kukamilisha kazi ya kuweka viunganishi katika waya huo na kazi hiyo inaendelea vizuri tangu vifaa vilivyokuwa vikisubiriwa kuwasili Zanzibar.
“Lakini siwezi kusema kazi zilizobakia zitakamilika lini na kurejeshwa kwa umeme ispokuwa kazi inaendelea vizuri na karibu vifaa vyote vilivyokuwa vinasubiriwa vimewasili Zanzibar,” alisema meneja huyo.
Hata hivyo habari zilizopatikana toka katika vyanzo vya kuaminika ndani ya shirika hilo, zinaeleza kuwa huenda huduma ya umeme Zanzibar ikarejea Machi 3, mwaka huu.
Meneja huyo aliwataka wananchi waendelee kuwa na subira na baada ya kukamilika kwa matengenezo shirika litawatangazia siku ya kurejea huduma hiyo.
Waya unaopokea umeme toka Tanzania Bara uliozikwa chini ya bahari tayari umemaliza muda wake wa matumizi wa miaka 30 na hiyo ni mara ya 3 kulipuka na kusababisha wananchi kukosa huduma ya umeme.
Waya huo unauwezo wa kupokea megawati 45 za umeme wakati matumizi ya umeme yamefikia megawati 43.7.
Tangu kukosekana kwa huduma ya umeme shirika hilo limekuwa likipata hasara ya sh bilioni 2.2 kila mwezi na viwanda vingi vimelazimika kufungwa kutokana na tatizo la umeme pamoja na baadhi ya hoteli za kitalii Zanzibar.
Awali SMZ ilitangaza huduma ya umeme Zanzibar ingetarajia kurejea leo lakini hali imekuwa tofauti.
Kukosekana kwa huduma ya umeme kumesababisha sherehe za kuzaliwa mtume Mohammed kushindwa kufanyika juzi usiku katika viwanja vya Mnazi Mmoja kama ilivyozoeleka na badala yake zilifanyika kuanzia saa 10 jioni katika msikiti wa mwembe shauri na kuongozwa na Rais wa Zanzibar alhaji Amani Abeid Karume.
Mei Mwaka 2008 wananchi wa Zanzibar walilazimika kukaa bila umeme kwa muda wa mwezi mmoja baada ya waya unaopokea umeme kulipuka katika kituo cha Fumba na serikali kulazimika kuagiza wataalamu kutoka Afrika Kusini na Norway.
source ippmedia
JE, unamfahamu mwanamuziki mkongwe Ibrahim Abdulwaheed Sykes maarufu kama Abby Sykes?
Hili si jina geni miongoni mwa wanamuziki nchini, lakini kama hulifahamu sina shaka jina la msanii wa muziki wa kizazi kipya Dully Sykes utakuwa unalifahamu vyema.
Ni kwamba Ibrahim Abdulwaheed Sykes au Abby Sykes kwa wasiomfahamu ndio baba mzazi wa msanii Dully Sykes.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, msanii huyo alisema alianza kujifunza muziki mwaka 1966, kwa kutoroka usiku nyumbani na kwenda disko na kwamba kutokana na kupenda sana muziki ndipo akatumia gita la baba yake mdogo kujifunza.
Anasema baada ya kuanza kuimba kwenye majukwaa, ndipo akakutana na Adamu Kingoni, akiwa kiongozi wa bendi ya Rifters.
Sykes anasema familia yao iliwahi kuunda kundi maarufu lililojulikana kama Shery Merry Marcas, ambalo liliundwa na baba zake kama Abdulwaheed Sykes, Ally Sykes, Balozi Sykes.
Anasema ilipofika mwaka 1970, ndipo akajiunga na bendi hiyo ya Rifters akiwa mpiga gita. Baada ya kukaa muda mrefu katika bendi hiyo, akaamua kujitoa na kujiunga na bendi nyingine ya Kenya iliyoitwa Hold Banjo.
Anasema kipindi hicho alikuwa akipiga karibuni vifaa vyote vya muziki, huku akijifunza kuimba kwa kusikiliza nyimbo za wanamuziki maarufu wa nje akiwemo kama James Brown.
Anasema mwaka 1978 akajipanga na kutoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa Mimi na Wewe na kwamba albamu hiyo aliweza kupata fedha kidogo, lakini zaidi fedha zao ilikuwa kwenye matamasha.
Anasema kutokana na kuona muziki haulipi vizuri aliungana na rafiki zake na kuomba kazi katika Meli ya mv Oman. Anasema kipindi hicho, mtu huwezi kuonekana bora, au mjanja bila kuwa baharia au mfanyakazi wa bandari.
Akaamua kuachana na kazi ya muziki, na kuungana na wenzake katika kazi ya ubaharia na kuendelea kujifunza vitu vingi kutoka nchi mbalimbali.
Baada ya safari ya kwanza ya miezi minane kurudi, aliamua kuachana na meli hiyo, na kujiunga na meli nyingine ya Youcht kwa miezi minane mingine.
Akiwa Baharia anasema aliona vitendo vingi vya kiovu vilivyoendelea baharini, lakini kubwa ambalo anashindwa kulisahau, anasema siku moja, wakiwa kwenye safari za nchi ya mashariki ya mbali wakiwa katikati ya maji aliona wamekamatwa Watanzania wanne na Wakenya saba.
Anasema baada ya kufikishwa kwa mkubwa, walitupwa baharini. Hapo ndipo roho ilipomuuma kuona ndugu zake wa Kitanzania na wale Wakenya wakiliwa na papa mbele ya macho yao.
Msanii huyo anasema kuwa alipata taarifa kuwa kuna Mkenya mmoja alipona katika sakata hilo na hadi hii leo akikumbuka wenzake hulia na kuchanganyikiwa. Mwaka 1980 akaamua kuachana na kazi hiyo ya ubaharia na kurudia kazi yake ya muziki.
Mwanamuziki huyo anasema yote hayo yameshapita na hivi sasa amerudi, kama zamani na anatarajia kufanya mapinduzi makubwa ya muziki.
Anasema amejiandaa kuibuka na bendi itakayoundwa na yeye, mwanawe na kuwa ameshajiandaa kutoa albamu yake ya pili ukiachilia ile ya zamani ya mwaka 1978 ya Mimi na Wewe.
Albamu hiyo amerekodia studio ya Dhahabu Record inayomilikiwa na Dully Sykes. Tayari ameshakamilisha kurekodi nyimbo kadhaa na kuzitaja kuwa ni Mchumba Mzuri, Famili Song, Only You, Lalaa akiwashirikisha mwanaye Dully Sykes na Mr Blue.
Anasema mtu ambaye anapenda sana kazi zake, na pindi akiwa sawa basi atamshirikisha katika albamu hiyo ni msanii David Nyika ‘Daz Baba’.
Mkali huyo ana nyimbo kwenye albamu moja ya wanamuziki mchanganyiko ya Urithi, ama Baba na Mwana, ambayo ni ya wasanii maarufu walioimba na watoto zao, kama Nguza Vicking na Papi Kocha, Zahir Ally na Banana Zoro, yeye akiimba wimbo wa Malaika.
source habarileo
