Watu Wafupi Wako Kwenye Hatari ya Kufa Kwa Magonjwa ya Moyo

Tuesday, June 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Utafiti uliofanywa kwa miaka 50 ukiwashirikisha watu milioni 3 umeonyesha ufupi ni tatizo na watu wafupi wako kwenye hatari ya kufariki kwa magonjwa ya moyo kulinganisha na watu warefu.
Baada ya miaka 50 ya utafiti wanasayansi wamegundua kuwa ufupi wa mtu ni mojawapo ya sababu zinazochangia watu kupata magonjwa ya moyo.

Utafiti huo ulionyesha kuwa watu wafupi wako kwenye hatari ya asilimia 50 zaidi ya watu warefu kupata magonjwa ya moyo.

Kwa wastani mtu alihesabika mfupi akiwa na urefu wa sentimeta 160.5 wakati mtu alihesabika mrefu alipokuwa na urefu wa sentimeta 173.9.

Utafiti huo ulionyesha usahihi kwa jinsia zote za kike na kiume ingawa kipimo cha urefu wa mwanaume na mwanamke kilikuwa tofauti.

Wanaume wafupi walitajwa kuwa na urefu chini ya sentimeta 165.4 wakati wanaume warefu walikuwa na urefu kuanzia sentimeta 177.5.

Wanawake wafupi walihesabika kuwa na urefu chini ya sentimeta 153 wakati wanawake warefu walikuwa na urefu wa sentimeta 166.4.

Kwa kuwa watu wafupi huwa na mishipa midogo ya damu ya coronary artery, hali hiyo huchangia kuwafanya wawe kwenye nafasi kubwa ya kukumbwa na matatizo ya msukumo wa damu mwilini.

Matokeo ya utafiti huu yalitolewa kwenye jarida la European Heart Journal baada ya kuwashirikisha jumla ya watu milioni 3.

Dr Tuula Paajanen, wa chuo kikuu cha Tampere nchini Finland, aliyeongoza utafiti huo alisema kuwa kwa miaka mingi kumekuwa na mjadala mrefu kuhusiana na urefu wa mtu kuwa mojawapo ya sababu za kupata magonjwa ya moyo.

Dr Paajanen alisema kuwa matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa ufupi wa mtu ni sababu inayojitegemea ya mtu kupata magonjwa ya moyo.

Dr Paajanen alisema kuwa mbali ya unene, uzee na kiwango kikubwa cha kolestro, ufupi nao inabidi uongezwe katika sababu zinazochangia matatizo ya moyo.


source nifahamishe

Imamu Mwanamke Anapowasalisha Wanaume

Sunday, June 13, 2010 / Posted by ishak / comments (0)



Mwanamama wa Kanada Raheel Raza kama ilivyotarajiwa jana aliweka rekodi kwa kuwa mwanamke wa kwanza wa kiislamu nchini Uingereza kusalisha sala ya ijumaa. Raheel aliwaambia waumini waliokuwepo msikitini kuwa si dhambi katika uislamu mwanamke kusalisha wanaume.
Mwandishi wa habari wa Kanada ambaye pia mwanaharakati wa kupigania usawa wa kijinsia katika dini ya kiislamu, Raheel Raza jana aliweka rekodi ya kuwa imamu mwanamke wa kwanza nchini Uingereza.

"Nilikuwa mwanamke wa kwanza kuwa imamu nchini Kanada, mwanamke kusalisha wanaume si dhambi, hata mtume wetu ametoa ruhusa ingawa baadhi ya maimamu wanakubali na wengine wanaona si sahihi ni makosa", alisema Rahel.

"Mimi kabla ya kutoa uamuzi wangu nilifanya utafiti na nimegundua kuwa ni sahihi na hamna kosa lolote".

"Nimetumiwa email nyingi za vitisho vya kuuliwa ili nisirudie tena kuwa imamu, hata hivyo mimi uimamu sio kazi yangu, nimekuja hapa baada ya kuitwa na watu", alisema Rahel.

Naye kiongozi wa kituo cha waislamu cha Oxford, Dr. Taj Hargey, ambaye ndiye aliyemualika Rahel kuja kusalisha katika kituo chao, alisema kuwa wanawake kuongoza misikiti si suala la kujadili.

"Hakuna aya katika Quran inayokataza wanawake kusalisha au kuongoza misikiti, katika uislamu wanaume na wanawake ni sawa. Kama katika misikiti hakuna usawa wa jinsia basi katika jamii pia hakutakuwa na usawa", alisema.

"Huenda ikawa ni vigumu kuwa na imamu mwanamke nchini Saudi Arabia au Pakistan lakini haimanishi kuwa ni makosa kuwepo sehemu zingine", aliongeza Dr. Taj Hargey.

Dr. Taj Hargey alisema kuwa sala ya jana haikukumbana na vipingamizi vyovyote hivyo inamaanisha kuwa watu wanaanza kuelewa na kukubali taratibu taratibu.

"Inabidi turudie kufanya hivi mara nyingi ili watu wazoee", alisema Dr. Taj Hargey

source nifahamishe

Hatimaye Sio Mungu Tena..

Sunday, June 13, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mtoto aliyezaliwa nchini India akiwa na mikono minne na miguu minne ambaye alikuwa akiabudiwa kama mungu amepoteza uungu wake baada ya kufanyiwa operesheni kuondoa mikono na miguu iliyozidi.
Deepak Paswan, 7, alizaliwa katika sehemu za watu masikini nchini India akiwa ameungana na pacha wake kwenye tumbo. Alikuwa na miguu minne na mikono minne lakini kichwa kimoja.

Waumini wa dini ya Hindu katika kijiji chake kilichopo kwenye jimbo la Bihar walikuwa wakimtembelea nyumbani kwake wakimuabudu kama Mungu wa Kihindu anayeitwa Vishnu.

Familia yake haikufurahia jinsi mamia ya watu walivyokuwa wakienda nyumbani kwao kwaajili ya kumuabudu mtoto huyo na waliomba msaada kwa watu ili mtoto huyo afanyiwe upasuaji.

Hatimaye maombi yao yalikubaliwa mei 30 mwaka huu na hospitali moja katika mji wa Bangalore ilikubali kulipa gharama zote za kumfanyia operesheni mtoto huyo.

Baada ya operesheni ngumu ya masaa manne, madaktari walifanikiwa kuondoa viungo vilivyozidi toka kwenye mwili wa mtoto huyo.

Deepak akitambulishwa mbele ya waandishi wa habari, alionekana kufurahia hali yake mpya ambayo imempotezea sifa yake ya uungu ambayo waumini wa Hindu walimpa.

"Siku zote tulitaka afanyiwe operesheni ili atenganishwe na pacha wake aliyejiunga tumboni mwake ili kuepuka watu kumfanya mtoto wetu chombo cha ibada", alisema baba wa mtoto huyo Viresh Paswan.

"Hatimaye ndoto yangu imetimia sasa tutafanya sherehe tutakaporudi kijijini kwetu", alisema Paswan.

source nifahamishe

Mtanzania auwawa........

Friday, June 11, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Takribani mwezi mmoja uliopita kulikuwa na tangazo kwenye blogs na hapa JF kwamba kuna dada yetu mmoja alipotea na akawa anatafutwa na ndugu zake.

Taarifa iliyotolewa kwenye local TV stations za Southern California zinasema kwamba mwili wa huyo dada ulipatikana jana nyuma ya nyumba aliyokuwa akiishi. Ulikuwa umefungwa kwenye mifuko ya plastic na blanket kama takataka.

Mume wa marehemu anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. Dada huyo alikuja kwa ajili ya kusomea kozi ya Uuguzi na alikuwa anasoma ili awe Registered Nurse. Ameacha watoto 2.

Lilian Mgonjwa alihojiwa na kituo cha TV kutoka makazi yake huko Long Beach. Kama kutakuwa na taarifa za ziada ninatumaini tutaendelea kujulishana

Amzalisha Binti Yake Watoto 7

Friday, June 11, 2010 / Posted by ishak / comments (0)



Mvuvi wa nchini Brazili ambaye alikuwa akimbaka mtoto wake kwa miaka 16 na kupelekea kuzaa naye watoto 7 ametiwa mbaroni.
Mvuvi toka maeneo ya watu masikini ya Maranhao nchini Brazili ambaye alikuwa akimwingilia kinguvu binti yake kwa miaka 16 ametiwa mbaroni.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Brazili la Estado, polisi walimtia mbaroni Jose Agostinho Bispo Perreira mwenye umri wa miaka 54 baada ya kupewa taarifa na mtu asiyejulikana juu ya mchezo wa mzee huo kula mayai yake mwenyewe.

Taarifa zinasema kuwa Perreira alianza mchezo wa kumuingilia binti yake tangia alipokuwa na umri wa miaka 12.

Taarifa zaidi zinasema kuwa Perreira alimfungia binti yake huyo kwenye kibanda kilichopo mbali na mji aliokuwa akiishi.

Polisi waliokuwa wakimfanyia uchunguzi Perreira wamegundua kuwa hivi sasa binti yake ana umri wa miaka 28, hajui kusoma wala kuandika na amezaa watoto saba na Perreira.

Mtoto mdogo kuliko wote ana umri wa miezi miwili wakati waliobakia wana umri wa miaka 4, 5, 7, 8 na 12.

Polisi wanasema kuwa Perreira alikuwa akiwagawa kwa familia zingine watoto aliozaa na binti.

Taarifa ya polisi ilisema kuwa mvuvi Perreira alianza kuishi na binti yake baada ya ndoa yake na mkewe kuvunjika.

Perreira alizaa watoto wanne na mkewe huyo. Watoto wake wawili wa kiume na mmoja wa kike walienda kuishi na mama yao mji mwingine.

Hawakuwa na taarifa kuwa baba yao alikuwa akimuingilia kwa nguvu mdogo wao na alizaa naye watoto saba.

source nifahamishe

Bakora 90 na Jela Miezi 4 Kwa Kubusiana Hadharani

Friday, June 11, 2010 / Posted by ishak / comments (0)

Mahakama nchini Saudi Arabia imemhukumu mwanaume aliyembusu mwanamke hadharani kucharazwa bakora 90 na kwenda jela miezi minne.
Mahakama mjini Riyadh, Saudi Arabia imemhukumu mwanaume aliyembusu mwanamke kwenye shopping mall kwenda jela miezi minne.

Mahakama pia imeamuru mwanaume huyo acharazwe bakora 90 kwa kitendo chake hicho.

Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la serikali la Al-Yom, polisi wa kidini wa Saudia walimtia mbaroni mwanaume huyo pamoja na wanawake wawili baada ya kuwaona wakifanya vitendo nje ya maadili mbele ya watu wengine.

Mwanaume huyo ambaye umri wake ni kwenye miaka ya 20, alionekana akiwa amekaa na mwanamke mmoja wakibusiana na kukumbatiana. Haikuelezewa mwanamke wa pili alikuwa akifanya nini wakati huo.

Majina ya wanawake hao na mwanaume huyo hayakutajwa.

Kwa mujibu wa sheria za kiislamu nchini Saudia, ni kosa mwanaume na mwanamke ambao hawana uhusiano wowote (hawajaoana) kuongozana barabarani achilia mbali kukaa pamoja na kuanza kubusiana.

Gazeti la Al-Yom liliripoti kuwa mwanaume huyo atacharazwa bakora 90 kwa mafungu matatu na pia amepigwa marufuku kuingia kwenye shopping mall yoyote nchini humo kwa miaka miwili.

Wanawake aliokamatwa nao watasomewa mashtaka yao katika mahakama nyingine.


source nifahamishe

Mwanamke Kusalisha Sala ya Ijumaa Uingereza Leo

Friday, June 11, 2010 / Posted by ishak / comments (0)



Kwa mara ya kwanza nchini Uingereza sala ya ijumaa ya waislamu itaongozwa na mwanamke anayepigania usawa wa kijinsia katika dini ya kiislamu.
Mwandishi wa habari wa Kanada, Raheel Raza mwenye umri wa miaka 60 atakuwa mwanamke wa kwanza nchini Uingereza kusalisha sala ya ijumaa.

Raheel ambaye alizaliwa muislamu, amekuwa akipigania usawa wa kijinsia katika dini ya kiislamu.

Raheel amealikwa mjini Oxford nchini Uingereza kusalisha sala ya ijumaa katika jumuiya inayoongozwa na kiongozi wa kituo cha waislamu mjini Oxford, Taj Hargey.

Kwa mujibu wa gazeti la Independent, Taj Hargey anadai kuwa yeye ni Imamu anayepigania sala zenye mchanganyiko wa jinsia na pia anapigania wanawake kuwa maimamu.

Raheel ambaye ni mkazi wa mji wa Toronto nchini Kanada, yeye anapigania usawa wa jinsia katika uislamu na anataka wanawake wapewe nafasi za uimamu na uongozi wa misikiti.

Miaka mitano iliyopita, Raheel alitumiwa vitisho vya kuuliwa baada ya kutoa khutba ya sala ya ijumaa ambayo wanawake na wanaume walichanganyika pamoja. Sala hiyo ilifanyika kwenye mojawapo ya vituo vya taasisi yake.

Raheel atakuwa mwanamke wa pili duniani kusalisha sala ya ijumaa lakini pia atakuwa mwanamke wa kwanza muislamu wa kuzaliwa kusalisha sala ya ijumaa.

Mwaka 2008, mwanamke wa kikristo wa Marekani aliyebadili dini kuwa muislamu na kujiita Amina Wadud aliongoza sala ya ijumaa nchini humo. Hata hivyo sala yake ilihudhuriwa na watu pungufu ya 40 kutokana na maandamano ya kumpinga yaliyofanywa na wanawake wa kiislamu.

Taj Hargey amedai kuwa sala ya leo ya ijumaa itakayoongozwa na mwanamama Raheel itahudhuriwa na watu zaidi ya 100 ambapo kama kawaida wanawake na wanaume watachanganyika na kuasali bega kwa bega.

source nifahamishe