'Yesu Alikuwa ni Muathirika wa Ukimwi'

Monday, September 06, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mchungaji wa kanisa moja nchini Afrika Kusini amezua zengwe kubwa nchini humo baada ya kudai kuwa Yesu alikuwa muathirika wa virusi vya HIV.
Mchungaji Xola Skosana wa kanisa la Way of Life Church la mjini Capetown, amesababisha mjadala mkubwa nchini humo baada ya kudai kuwa Yesu alikuwa muathirika wa virusi vya HIV vinavyosababisha ukimwi.

Mchungaji Skosana alisema kuwa aliamua kusema hivyo ili kuyafanya makanisa ya Afrika Kusini yaache kukaa kimya linapozungumziwa suala la kuongezeka kwa idadi ya waathirika wa ukimwi.

"Nikiwa kama mchungaji, nina jukumu la kuwajulisha watu juu ya Mungu ambaye huwajali watu na kuwatakia mema, sio ambaye huwadharau na kuwahukumu", alisema mchungaji huyo.

"Wanasema huwezi kumhusisha Yesu na Ukimwi", alisema mchungaji Skosana.

"Lakini Katika sehemu nyingi za Biblia, Yesu anajiweka kama mgonjwa na mtu wa hali ya chini, tukiwatembelea watu ambao ni wagonjwa tunakuwa tumemtembelea yeye, tukiwapuuza wagonjwa tunakuwa tumempuuza yeye", alisema mchungaji Skosana.

Mwezi uliopita, Skosana ambaye alipoteza ndugu zake wawili wa kike kutokana na ukimwi, alijipima ukimwi hadharani mbele ya wafuasi wake, wafuasi wake 100 nao walimuunga mkono na kuamua kujipima ukimwi hadharani.

Hatua yake hiyo ilipongezwa na taasisi za kupambambana na ukimwi nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo kauli yake hii imepelekea wakristo nchini Afrika Kusini kumtuhumu kuwa analichafua jina la Yesu.

Mchungaji Skosana, ameyataka makanisa nchini Afrika Kusini kuacha ukimya wao na kuanza kuwausia waumini wao juu ya ugonjwa wa ukimwi.

Kanisa katoliki nchini humo limejiweka mbali na mijadala ya ugonjwa wa ukimwi huku likiendelea kupinga matumizi ya kondomu.

Takribani watu 1,000 wanafariki kila siku kutokana na ukimwi nchini Afrika Kusini.

source nifahamishe