Sita Mbaroni Kwa Kuichoma Moto Quran Uingereza

Friday, September 24, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Polisi wa nchini Uingereza wamewatia mbaroni watu sita kwa kueneza chuki katika jamii kwa kuweka VIDEO kwenye YouTube wakionyesha jinsi wanavyoichoma moto Quran na kuipiga mateke.
Polisi wa nchini Uingereza wametoa taarifa wakisema kuwa wamewatia mbaroni watu 6 ambao waliweka video kwenye YouTube wakionyesha jinsi walivyoichoma moto misahafu na kuipiga mateke.

Taarifa ya polisi ilisema kuwa watu wawili walitiwa mbaroni septemba 15 na wengine wanne walitiwa mbaroni juzi jumatano. Wote wako nje kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.

"Walikamatwa kufuatia tukio la kuchoma moto misahafu miwili katika kitongoji cha Gateshead siku ya septemba 11", alisema msemaji wa polisi.

"Tukio hilo lilirekodiwa na baadae kuwekwa kwenye internet", iliendelea kusema taarifa ya polisi.

Video hiyo ya YouTube iliwaonyesha wanaume walioficha sura zao kwa vitambaa wakipiga kelele za "Septemba 11, siku ya kimataifa ya kuichoma moto Quran" wakitukana na pia wakiimba "Hii ni kwaajili ya vijana wetu waliopo Afghanistan".

Wanaume hao walichukua mafuta ya petroli na kuyamwaga kwenye misahafu miwili na kuichoma moto misahafu hiyo.

Waliendelea kuimba na kupiga kelele wakati misahafu hiyo ikiendelea kuungua kabla ya kuanza kuipiga mateke.

Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa kitongoji hicho ulitoa taarifa ya pamoja wakilaani kitendo hicho na kusema kuwa vitendo vilivyoonyeshwa kwenye video hiyo haviwakilishi mawazo ya jamii.

"Jamii yetu imeundwa kwa heshima kwa watu wote na tunaendelea kushirikiana na viongozi wa jumuiya, wakazi na watu wa imani zote ili kudumisha ushirikiano uliopo", ilisema taarifa hiyo.

Kutiwa mbaroni kwa wanaume hao kumekuja zikiwa hazijapita wiki mbili tangu mchngaji wa nchini Marekani, mchungaji Terry Jones alipoahirisha mpango wake wa kuichoma moto misahafu 200 katika kuadhimisha siku ya kuwakumbuka wahanga wa shambulizi la septemba 11, 2001.

source nifahamishe