Kitabu cha Katuni za Kumkashifu Mtume Kutolewa Mwezi Ujao

Friday, August 27, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mwandishi wa habari wa Denmark ambaye alisababisha mtafaruku duniani alipotoa katuni za kumkashifu mtume Muhammad (s.a.w) kwenye gazeti, ametangaza kuwa atatoa kitabu mwezi ujao chenye katuni hizo.
Mwandishi wa habari wa Denmark ambaye mwaka 2005 alichapisha katuni 12 za kumkashifu mtume Muhammad (s.a.w) kwenye gazeti, ametangaza kuwa kitabu kipya chenye katuni hizo kinatoka mwezi ujao.

Kitabu hicho kilichoandikwa na mhariri wa gazeti la Jyllands-Posten, Flemming Rose kitaingia madukani septemba 30 ikiwa ni miaka mitano tangu katuni hizo zilipochapishwa kwenye gazeti.

Kuchapishwa kwa katuni hizo kulisababisha mtafaruku duniani na kupelekea baadhi ya watu kufariki katika maeneo mbalimbali duniani.

Katika mahojiano na gazeti la Denmark la Politiken, Rose alisema kuwa hataki kuleta chokochoko lakini anataka watu wazifahamu katuni 12 pamoja na picha zingine ambazo zinadaiwa kuwa ni za uchochezi.

"Najua watu wengi hawaelewi nafikiria nini kuhusiana na katuni hizi, nataka nijielezee mwenyewe, sina chochote zaidi ya kutumia maneno kuelezea .. baada ya watu kukisoma kitabu nadhani wataelewa ukweli wa mambo. Maneno yajibiwe kwa maneno, hivyo ndivyo inavyotakiwa kwenye demokrasia", alisema Rose.

Rose ambaye alitumiwa vitisho vingi vya kuuliwa alipochapisha kwa mara ya kwanza katuni hizo, alisema kuwa anataka kuanzisha mjadala barani ulaya kuhusiana na jinsi watu wanavyotakiwa kuishi kwenye karne ya 21. "Mgogoro wa katuni umeonyesha tutegemee nini kwenye karne ya 21", alisema.

Naye msanii wa katuni wa Denmark, Kurt Westergaard, ambaye alichora katuni ya mtume iliyomuingiza matatani kwa kuchora katuni aliyodai ya mtume ikiwa na bomu kwenye kilemba, naye ametangaza kuchapisha kitabu cha katuni zake hizo ndani ya miezi michache ijayo.

Mwanzoni mwa mwezi huu gazeti la Jyllands-Posten lililochapisha katuni hizo lilitangaza kuwa limeweka fensi za umeme kwenye ofisi zake ili kujilinda na mashambulizi ya kigaidi.

source nifahamishe

Mwarabu Ampigilia Misumari 24 Hausigeli Wake

Friday, August 27, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mfanyakazi wa ndani toka nchini Sri Lanka aliyekuwa akifanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia, amerudi kwao akiwa na misumari 24 ndani ya mwili wake ambayo ilipigiliwa na bosi wake kila alipokuwa akilalamika kazi ngumu alizokuwa akipewa.
Picha za X-Ray zilionyesha misumari 24 ikiwa kwenye mwili wa bi L.T. Ariyawathi kwenye sehemu za kichwani, miguuni na mikononi.

Ariyawathi mwenye umri wa miaka 49, aliamua kurudi kwao Sri Lanka baada ya miezi mitano ya kufanya kazi nchini Saudi Arabia, atafanyiwa operesheni kesho kuiondoa misumari toka kwenye mwili wake.

Mfanyakazi huyo wa ndani aliliambia gazeti moja nchini humo kuwa bosi wake raia wa Saudi Arabia alikuwa akimpigilia misumari kama adhabu.

"Walikuwa hawaniruhusu nipumzike, mke wake alikuwa akiipasha moto misumari halafu yeye alikuwa akiipigilia kwenye mwili wangu", alisema Ariyawathi.

Prabath Gajadeera, mkurugenzi wa hospitali ya Kamburupitiya hospital nchini humo ambayo Ariyawathi anapatiwa matibabu alisema: "Picha za X-ray zimeonyesha kuwa misumari 24 na sindano zimo kwenye mwili wake, kuna msumari mmoja kwenye paji lake la uso".

Misumari hiyo yenye urefu wa sentimeta tano ilipigiliwa zaidi kwenye mikono, miguu na viganja vya miguu ya Ariyawathi.

"Hali yake inaendelea vizuri lakini tunampatia antibiotics na dawa za kutuliza maumivu".

Tukio hili limetishia uhusiano wa kisiasa kati ya Sri Lanka na Saudi Arabia.

Kuna raia wa Sri Lanka milioni 1.8 walioajiriwa nje ya nchi. Asilimia 70 kati yao ni wanawake.

Wengi wao hufanya kazi za ndani katika nchi za mashariki ya kati wakati wachache hufanya kazi nchini Singapore na Hong Kong.

source nifahamishe

Nyota wa Muziki Aliyewaambukiza Watu Ukimwi Anusurika Kwenda Jela

Friday, August 27, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Nyota wa muziki wa Pop wa Ujerumani ambaye huku akijua kuwa ameathirika, alifanya mapenzi na wanaume bila kutumia kinga na kupelekea kumuambukiza ukimwi mpenzi wake mmoja, amenusurika kwenda jela baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje cha miaka miwili
Mahakama ya mji wa Darmstadt nchini Ujerumani, imemhukumu kifungo cha nje cha miaka miwili, mwanamke nyota wa muziki wa pop wa nchini humo Nadja Benaissa kwa kosa la kumuambukiza ukimwi mpenzi wake.

Benaissa ambaye ni mmoja wa waimbaji wa kundi la muziki wa Pop la "No Angels", alipewa hukumu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kosa moja la kudhuru mwili.

Mwimbaji huyo maarufu wa nchini Ujerumani alikiri kufanya mapenzi na wanaume bila kutumia kinga bila ya kuwajulisha kuwa yeye ni muathirika.

Benaissa ambaye ni mjerumani mwenye asili ya Morocco, aliomba radhi mahakamani kwa kitendo chake hicho kwa kusema "Naomba radhi kwa moyo wangu wote, ningependa kuurudisha muda nyuma ili kuepuka vitendo nilivyofanya lakini siwezi kufanya hivyo".

Benaissa anadaiwa kufanya mapenzi na wanaume watatu kati ya mwaka 2000 na 2004 bila ya kuwataarifu kuwa yeye ni muathirika.

Benaissa alikuwa akijitambua fika kuwa yeye ni muathirika tangia mwaka 1999, nyaraka za mahakama zilisema.

Benaissa aligundulika ana ukimwi wakati wa ujauzito wake wakati alipokuwa na umri wa miaka 16.

Mmoja wa wanaume hao watatu ambaye ameishathibitishwa kuwa ameambukizwa virusi vya HIV vinavyosababisha ukimwi ndiye aliyemfikisha mahakamani Benaissa.

Kosa lililokuwa likimkabili Benaissa lingeweza kupelekea ahukumiwe kwenda jela miaka 10, lakini waendesha mashtaka walitaka ahukumiwe kifungo cha nje kwakuwa alikiri kosa lake na kuomba msamaha.

source nifahamishe

Miaka 20 Jela Kwa Kumtikisa Mtoto Wake Mchanga

Friday, August 27, 2010 / Posted by ishak / comments (0)

Mwanaume wa nchini Marekani ambaye alichoshwa na vilio vya mtoto wake mchanga na kuamua kumnyamazisha kwa kumtikisa kwa nguvu mtoto wake huyo na kupelekea kuharibika kwa ubongo wake, amehukumiwa kwenda jela miaka 20.
Gerardo Espinosa mhamiaji holela nchini Marekani toka Mexico, amehukumiwa kwenda jela miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kuuharibu ubongo wa mtoto wake mchanga kwa kumtikisa kwa nguvu wakati alipokuwa akilia.

Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa Espinosa mkazi wa Nevada hakutaka vilio vya mtoto wake mchanga wa kike viingilie uchezaji wake wa video game kwenye televisheni.

Ili kumnyamazisha mtoto wake, Espinosa ambaye ana umri wa miaka 19, alimtikisa kwa nguvu sana mtoto wake na kupelekea kuharibika kwa ubongo wake.

Kitendo cha Espinosa kilipelekea mtoto wake apate vilema vya maisha, akipoteza uwezo wa kuona na kusikia huku akitembea kwa tabu sana.

Akiongea wakati wa kutoa hukumu, jaji Patrick Flanagan alilaani kitendo cha Espinosa na kusema kuwa kama sheria zingeruhusu angemhukumu Espinosa kwenda jela maisha.

Espinosa alihukumiwa kwenda jela miaka 20 pamoja na kujitetea kuwa majeraha ya binti yake yalitokana na kuanguka chini kwa bahati mbaya.

Mtoto wake alikuwa na umri wa wiki 11 wakati tukio hilo lilipotokea.

source nifahamishe

Semenya Azua Tena Mjadala wa Jinsia Yake

Monday, August 23, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mjadala wa jinsia ya mwanariadha wa kike wa Afrika Kusini, Caster Semenya umeibuka tena baada ya Semenya kuwaburuza tena wenzake na kushinda mbio za mita 800 nchini Ujerumani na kuwaacha wanariadha wenzake wakilalamika wanashindana na mwanaume.
Baada ya kudaiwa hakukumbana na nyota wa riadha katika mbio zake za mita 800 nchini Finland, Caster Semenya amewadhihirishia watu kuwa yuko fiti kwa kuwaburuza vigogo wa mbio za wanawake za mita 800 nchini Ujerumani.

Katika mbio hizo zilizofanyika jana mjini Berlin, Semenya aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa dakika moja na sekunde 59.90.

Ushindi huo wa Semenya umeibua tena mjadala wa jinsia yake ambapo sasa baadhi ya wanariadha wenzake wameanza kulalamika kuwa wanashindana na mwanaume.

Mwanariadha wa Uingereza Jemma Simpson, ambaye alishika nafasi ya nne kwa kutumia sakika 2 na sekunde 0.57 alilalamika kuruhusiwa kwa Semenya kushiriki mbio za wanawake wakati kukiwa na mjadala wa jinsia yake.

"Wakati mwingine tunajizuia kutoa maoni yetu kuhusiana na jinsia ya Semenya lakini tunasikitishwa sana", alisema Simpson.

Naye mwanariadha wa Kanada, Diane Cummins ambaye alishika nafasi ya nane kwenye mbio hizo hakuficha hasira zake kwa kudai wanashindana na mwanaume.

Diane alisema kuwa wakiwa kama wanariadha wanashindwa kutoa maoni yao binafsi kuhusiana na Semenya kwakuwa wanapotamka yaliyo mioyoni mwao huonekana ni wanamichezo wabaya ambao wanatoa lawama baada ya kushindwa.

Mwanariadha wa Italia, Elisa Cusma Piccione, ambaye alishika nafasi ya tatu alikataa kutoa maelezo ya kauli yake aliyoitoa mwaka jana kuwa Semenya ni mwanaume.

Semenya kwa upande wake alisema kuwa ataanza maandalizi yake kujiandaa na mbio za jumuiya ya madola zitakazofanyika mwezi oktoba.

Semenya aliingia kwenye mbio za jana akiwa amefanya mazoezi kwa mwezi mmoja tu na hakufanya mazoezi ya kuongeza spidi yake.

Inatarajiwa kuwa kwenye mbio za mwezi oktoba atakuwa amerudia fomu yake ya zamani aliyokuwa nayo wakati anaweka rekodi ya dunia kwenye mbio za wanawake za mita 800.

source nifahamishe

Msiba Juu ya Msiba

Monday, August 23, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Baba na mama mmoja wa nchini Ufaransa walipigwa na mshtuko wa ghafla wakati walipofika makaburini kwaajili ya mazishi ya ndugu yao na bila kutarajia kuliona kaburi la mtoto wao waliyekuwa wakijua yuko hai na mwenye afya njema.
Kwa mujibu wa gazeti la La Voix du Nord la nchini Ufaransa, Josiane Vermeersch na mkewe Elie Langlet walifika kwenye makaburi ya Hellemmes mjini Lille kaskazini mwa Ufaransa kwaajili ya mazishi ya kaka yake Ellie.

Lakini wakati wakiondoka makaburini baada ya mazishi, mmoja wa wanafamilia aliona bango juu la kaburi likiwa na jina la mtoto wao likisomeka "Olivier Langlet, 1968-2010".

Kwa mshangao mkubwa wanafamilia waliwasiliana na uongozi wa makaburi hayo ili kujua undani wa suala hilo.

Uchunguzi wa haraka haraka wa kaburi hilo ulithibitisha kuwa marehemu alikuwa ni mtoto wa kiume wa familia hiyo ambaye alikuwa akiishi umbali wa kilomita tano tu toka nyumbani kwa baba na mama yake. Taarifa zaidi zilisema kuwa alikutwa amefariki nyumbani kwake kutokana na maradhi.

Josiane na mkewe waliviambia vyombo vya habari kuwa walikuwa wakijua mtoto wao yu hai na mwenye afya njema na walijaribu kumtafuta bila mafanikio kumpa taarifa ya msiba wa mjomba wake.

"Hatukuamini macho yetu baada ya kuona kaburi lake, ghafla tulianza kuangua kilio", walisema wanafamilia hao.

Familia hiyo ilisema kuwa haikupewa taarifa ya kifo cha mtoto wao ambaye alizikwa kinyemela bila ndugu zake kujulishwa.

Vyombo vya habari vya Ufaransa, vimelaani uzembe uliofanyika wa kutoijulisha familia yake hasa zama hizi za teknolojia ambapo njia za mawasiliano zimekuwa nyingi sana.

"Alienda kumzika kaka yake akakutana na kaburi la mtoto wake", lilisema gazeti moja la nchini humo kuelezea tukio hilo ambalo limezua mjadala mrefu.

Polisi wa Ufaransa wanachunguza kwanini polisi na maafisa wa mazishi hawakuwapa taarifa wazazi na ndugu wa marehemu kabla ya kumzika mtoto wao.

source nifahamishe