Maalim Seif ataka uchaguzi Zanzibar usogezwe mbele

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


KATIBU mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amependekeza uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka huu usogezwe mbele au Rais Amani Abeid Karume aongezewe muda ili kuweka misingi imara ya kuondoa siasa za chuki visiwani humu.

Hamad alitoa pendekezo hilo jana alipokuwa akiwasilisha mada kwenye kongamano la siku moja la kujadili maridhiano na mustakabali wa Zanzibar lililofanyika kwenye Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

Pendekezo hilo limekuja siku mbili baada ya Rais Amani Abeid Karume kueleza kwenye sherehe za Mapinduzi kuwa hakuna muhula wa tatu kwa urais wa Zanzibar katika hotuba iliyoonekana kama ya kuaga Wazanzibari.

Wakati Karume akionekana kukataa pendekezo hilo ambalo utekelezaji wake unahitaji mabadiliko ya kikatiba, Maalim Seif aliibuka na wazo tofauti katika kongamano hilo lililoandaliwa na chama chake na kushirikisha viongozi mbalimbali wa kisiasa, dini, wasomi na wataalamu wa ndani na nje ya nchi.

"Binafsi nimekuwa nikitafakari sana changamoto hizi na naamini tunapaswa kuzitafakari na kuzijadili kwa lengo la kuona tunazikabili vipi," alisema Seif ambaye aliwahi kuwa waziri kiongozi.

"Ni maoni yangu kuwa tukifanya haraka ya kukimbilia uchaguzi ambao nilishaeleza hapo awali kwamba umekuwa ndiyo chanzo cha kuvurugika kwa umoja wetu, kuna hatari ya kuyapoteza yote niliyoyaeleza.

"Hatuwezi kukwepa uchaguzi maana ndiyo njia ya kidemokrasia ya kuwapata viongozi wetu, lakini tumeshafanya chaguzi saba za vyama vingi Zanzibar, nne kabla ya Mapinduzi na tatu tangu 1992 na zote zimeshindwa kutupa umoja.

"Kwa Zanzibar, katika kipindi hiki, maridhiano ni muhimu zaidi kuliko uchaguzi. Tutapaswa kwenda katika uchaguzi, lakini naamini tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi baada ya kufanikiwa kujenga msingi madhubuti wa maridhiano."

Maalim Seifa alisema baada ya kutafakari kwa kina, ameamua kuungana na wananchi wa Zanzibar zikiwamo taasisi za kidini zinazotaka Rais Karume aongezewe muda au uchaguzi kusogezwa mbele.

Alisema hili litatoa fursa kwa Wazanzibari kuingia katika uchaguzi huo baadaye wakati ukiwa huru na salama zaidi bila matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza miaka ya nyuma.

"Natoa wito wa kuchukuliwa hatua ya kusogeza mbele kidogo uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka huu kwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja au miaka miwili ili kutoa nafasi kwa Rais Amani Karume kuchukua hatua zaidi za kukamilisha kazi njema aliyoianza," alisema.

"Naelewa mwenyewe juzi katika hotuba yake ya kilele cha sherehe za Mapinduzi, (Karume) alisema kwamba anakamilisha kipindi chake na katiba ya Zanzibar hairuhusu kipindi cha tatu. Nakubaliana naye na sipendekezi kuondolewa kwa ukomo wa vipindi viwili kwa mtu anayeshikilia madaraka ya urais wa Zanzibar.

"Ila, namwomba sana akubaliane na matakwa ya Wazanzibari walio wengi kama yalivyokwisha onyeshwa kupitia taarifa na kauli mbalimbali kwamba kipindi chake cha pili tukiongeze muda kidogo ili tusiipoteze fursa ya kihistoria ambayo ameianzisha yeye."

Maalim Seif ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa upande wa serikali na upinzani kulitafakari kwa kina jambo hilo na kuwapa Wazanzibari wanachokitaka.

"Nawaomba Wazanzibari tuungane pamoja kumtaka Rais Amani Karume aweke upande dhamira yake ambayo najua anaiamini sana ya kuondoka madarakani mwaka huu na badala yake akubaliane nasi juu ya haja ya kuendelea kuubeba mzigo huu tunaotaka kumtwisha na atuvushe pale ambapo waliomtangulia walishindwa," alisema.

Awali Maalim Seif alianza mada yake kwa kusema: "Mimi na Rais Karume tumekubaliana kuwa hakuna kurudi nyuma katika hatua tuliyoianzisha."

Alisema nia ni kuona kuwa wanaitumia fursa hiyo kuirudisha Zanzibar katika nafasi yake iliyokuwa nayo awali kwa kuwa Wazanzibari wamechoshwa na matatizo wanayoyapata katika kipindi chote kilichopita.

Kwa mujibu wa Maalim Seif ni muhimu kwa Zanzibar sasa sio uchaguzi bali kuondoa siasa za utengano, chuki, ubaguzi, uhasama, ugomvi na visasi na kuweka siasa za umoja, maelewano na mashirikiano.

Mada hiyo ya Maalim Seif iliungwa mkono na watu waliohudhuria kongamano hilo ambao walisema wataendelea kumshawishi Rais Karume kukubali kuendelea na wadhifa wake ili kutoa nafasi ya kurekebishwa baadhi ya kasoro kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Walisema hakuna haja ya kuingia katika uchaguzi wakati inafahamika kila uchaguzi unaofanyika Zanzibar hutawaliwa na vurugu na hatimaye wananchi kupoteza maisha au kujeruhiwa.

Naila Majid Jidawy, mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa katika vyama tofauti, alisema ipo haja ya kuongezwa muda kwa viongozi wawili Maalim Seif na Rais Karume ili wamalize tofauti zao na mambo waliyokubaliana ili Wazanzibari waingie katika uchaguzi wakiwa na hali ya usalama na amani.

"Maalim mada yake ni kubwa sana katika nchi maana anazungumzia usalama wa Wazanzibari, hazungumzi kama mgombea anataka kugombea kwa maana kwamba huu uchaguzi unaotaka kuja miezi tisa au kumi ijayo hautafanikiwa na hakuna njia ya kufanikiwa na sote tunajua," alisema.

"Kwa maoni yangu binafsi, nataka uchaguzi huu uahirishwe na yeye Maalim na Karume waendelee kwa sababu wao ndio walioyawaza haya na kuzungumza na wakatushushia sisi na wametupa maneno mazito haya ni makubwa sana."

Akichangia mada katika kongamano hilo, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa chuo kikuu cha Zanzibar, Zubeir Zubeir alisema iwapo uchaguzi utafanyika hivi sasa, kuna uwezekano wa kuwepo matatizo makubwa.

Aliwataka wanafunzi wenzake na viongozi wote kuunga mkono mazungumzo hayo ili kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa hakuna mtu mwenye hati miliki ya uongozi.

Katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Hamad Yussuf alisema mfumo uliopo ubadilishwe ili atakayekuja aje kukuta mfumo uliopo ambao utawarahisishia wananchi kufaidi matunda yaliyopo kwani kuongezewa muda kwa Rais Karume kunaweza kusababisha matatizo ya kikatiba.

"Rais ana miaka tisa sasa kwa hivyo ni kipndi cha kutosha kama alitaka kuweka mfumo au kuweka chochote. Kwa maoni yangu rais atumie miezi iliyobakia katika baraza la wawakilishi linalokuja ili kurestructure (kujenga upya)mifumo au na kufuta sheria kandamizi badala ya kusema tumuongezee muda," alisema.

Makamu mwenyekiti wa NLD, Mfaume Ali Hassan alisema uchaguzi unaokuja uongezwe muda kwa kuwa huenda watu wakaingia katika mapambano ya lazima.

Wakili maarufu, Awadh Ali Said alisema hakubaliani na maoni ya wengi ya kuongezewa muda Rais Karume akisema ni sawa na kuendeleza udikteta na kuwekeza kwa watu na sio kwa nchi.

source,mmwananchi.co.tz

Afungwa miaka 30 jela kesi ya wizi NBC Ubungo

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana iliwaachia huru washitakiwa tisa wa kesi ya kula njama na kuiba katika benki ya NBC Tawi la Ubungo,Dar es Salaam.

Mshitakiwa, Rashid Lembrisi, akihukumiwa kifungo cha miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya tuhuma hizo.

Walioachiwa huru ni Abdulrahman Dodo, Rahma Galos, Mashaka Mahengi, Philipo Mpoki, John Mdasha, Martine Mdasha, Jackson Sawangu, Lucas Aloyce na Ramadhan Abdulrahman.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi , Pelagia Khaday, ambaye hivi sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania.

Alitoa hukumu hiyo baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili za mashitaka na utetezi ambapo alibainisha kuwa Lembrisi alionekana kuhusika zaidi na tuhuma hizo.

Wakili wa Upande wa Utetezi Magafu alimuomba Jaji huyo kumpunguzia adhabu mtuhumiwa huyo kwa madai kuwa ni kijana anayetegemewa na familia yake.

Jaji Khaday alisema, angetoa hukumu hiyo kwa kuzingatia aina ya kosa, uzito wa kosa na mazingira yake.

Watuhumiwa hao walikuwa wakidaiwa kuwa Februari 2, 2006 katika benki ya NBC tawi la Ubungo kwa pamoja walitumia silaha kuiba Sh milioni 168.5, dola za Kimarekani 16,128, na euro 50 mali ya benki hiyo.

source.habarileo.co.tz

Kahaba Aishtaki Shule Yake Kwa Kumuachia Awe Kahaba

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Mwanamke mmoja wa nchini Uholanzi ameifikisha kizimbani shule yake kwa kushindwa kumlinda asiangukie kwenye ukahaba.
Maria Mosterd ameifikisha mahakamani shule yake katika mji wa Zwole akiidai fidia kwa kushindwa kumlinda asiangukie kwenye ukahaba.

Maria mwenye umri wa miaka 20 ameandika kitabu kuhusiana na shughuli yake ya ukahaba akisema kuwa wafanyabiashara wa ukahaba walikuwa wakimchukua mbele ya shule na kwenda kumfanyisha ngono na wanaume kwa malipo.

Mama yake Lucie Mosterd alisema :"hali hii hutokea kwenye shule nyingi na hakuna mtu anayewajibishwa".

Mahakama katika mji wa Zwolle ilikataa kuikubali kesi hiyo ikisema kuwa shule yake ilijaribu kuwasiliana bila mafanikio na mama yake kuhusiana na mabadiliko ya tabia ya binti yake.

Mahakama iliiambia pia familia ya Maria kuwa wazazi ndio wenye majukumu ya kuwalinda watoto wao.

Familia ya Maria imesema itakata rufaa kuhusiana na maamuzi hayo ya mahakama.


source.nifahamishe

Aozeshwa Kwa Baba Mkwe Wake Kwa Mahari ya Nguruwe

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Ni kawaida kwa mwanamke barani Afrika kuolewa kwa mahari ya ng'ombe na mbuzi lakini hali ilikuwa tofauti nchini New Zealand ambapo msichana mmoja alilazimishwa kuolewa na baba mkwe wake kwa mahari ya nguruwe mmoja aliyenona.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 alijikuta akiozeshwa kwa baba mkwe wake mtarajiwa na sio mpenzi wake kama alivyotegemea baada ya mzee huyo kutoa mahari ya nguruwe na jamvi moja la thamani kubwa.

Msichana huyo alikuwa akiishi na mama yake pamoja na baba yake wa kambo ambao wote wawili wametiwa mbaroni wakikabiliwa na makosa ya kumlazimisha msichana huyo kuolewa na mzee huyo na pia kumlazimisha kufanya mapenzi na mwanaume huyo ambaye ni baba wa mpenzi wake.

Kwa mujibu wa gazeti la Sunday Star-Times la New Zealand, mama wa msichana huyo anakabiliwa pia na mashtaka ya kumshambulia binti huyo mara mbili ili akubali kuolewa na mwanaume huyo ambaye angekuwa baba mkwe wake iwapo angeolewa na mpenzi wake.

Taarifa zaidi zilisema kwamba msichana huyo alikuwa hataki kuolewa na mzee huyo lakini kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya familia hizo mbili, alilazimishwa kukubali kuolewa.

Familia yake ilikabidhiwa mahari ya nguruwe mmoja mkubwa sana aliyenona pamoja na jamvi moja la gharama.

Usiku wa harusi yake, msichana huyo alikimbia na kwenda kwa mpenzi wake ambaye ni mtoto wa mzee huyo aliyeozeshwa kwake.

Alipogundulika amejificha kwa mpenzi wake, alifuatwa na kushambuliwa na kisha kutekwa na kurudishwa kwa mume wake ili aanze kumtumikia kama mke wake.

Mama wa msichana huyo na mumewe watapandishwa kizimbani baadae mwezi huu wakikabiliwa na mashtaka sita na iwapo watapatikana na hatia wanaweza kutupwa jela miaka 14.

source.nifahamishe

Haiti Yakumbwa na Tetemeko la Ardhi, Maelfu Wazikwa Hai

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 7.0 limeikumba haiti masaa machache yaliyopita na kupelekea maelfu ya watu kufunikwa na vifusi wakiwa hai.
Operesheni kubwa inaendelea kuwaokoa maelfu ya watu waliozikwa hai na vifusi vya majumba kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea nchini Haiti ambalo halijawahi kutokea katika visiwa vya Caribbean.

Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.0 lilibomoa hospitali na majumba katika mji mkuu wa Haiti wa Port-au-Prince na kusababisha maafa makubwa huku kila mtu aliyesalimika akihaha kumuokoa ndugu yake au ndugu zake waliofunikwa na vifusi.

Mamia ya watu wapo chini ya vifusi wakipiga kelele za kuomba msaada.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo lililotokea masaa machache yaliyopita alielezea jinsi alivyoiona miili ya watu ikiwa imezagaa katika mji huo ambao mawasiliano ya simu yamekatika.

Shuhuda huyo alisema kuwa maelfu ya watu wakiwa aidha wamefariki au majeruhi, walionekana mitaani ambapo barabara hazipitiki kutokana na vifusi vya majumba.

Matrekta yalionekana mitaani yakisaidia kufukua vifusi vya majumba mbali mbali yakiwemo makazi ya wanadiplomasia na wafanyakazi wa umoja wa mataifa.

Rais wa Marekani, Barack Obama ameelezea kusikitishwa kwake na maafa hayo na amesema kuwa Marekani iko tayari kutoa msaada.

"Maombi yangu na sala zangu ziwaendee wahanga wa tetemeko la ardhi, tunalifuatilia suala hili na tupo tayari kuwasaidia wananchi wa Haiti", alisema rais Obama.

ource.nifahamishe

Watatu wa familia moja wafukiwa na kifusi

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)

WATU watatu wa familia moja wamekufa kufuatiwa kufukiwa na kifusi na mwingine kusombwa na maji ya mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Arusha



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, amethibitisha matukio hayo na kusema vifo vya watu hao vimetokana na kufukiwa na vifusi na kuswombwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika wilaya za Longido na Arumeru mkoani humo.

Alisema mwili wa mtu mmoja uliokotwa ukiwa na majeraha unaosadikiwa kuwa kifo chake kilitokana na mvua hizo.

Kamanda Matei alisema watatu wengine wa familia moja walikutwa katika machimbo ya Moramu Mweupe wa Kujengea Nyumba, baba na watoto walikutwa wamekufa kufuatiwa kufumikwa na kifusi kilichosombwa na mvua na kuwafunuka.

Mvua hizo zimekuwa zikiathiri watu wengi katika mikoa tofauti tofauti na kusababisha vifo na nyumba kubomoka katika sehemu tofauti nchini

Kutuatia mvua hizo wilayani Kilosa mkoani Morogoro, wilaya hiyo imeendelea kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua zinazonyesha hivi sasa ambapo katika kitongoji cha Mateteni, Kijiji cha Mbiligili, jumla kaya 173 zenye watu 225 nyumba zao zimezungukwa na maji.

Hivi sasa watu hao wamehifadhiwa katika kambi iliyokuwa ya wakimbizi eneo la Shule ya Msingi Dakawa Centre baada ya kukumbwa na mafuriko na nyumba zao kuzingirwa na maji.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendegu, alisema mafuriko hayo yalianza kutokea usiku wa kuamkia Januari 12, mwaka huu baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mto Mkundi kujaa maji na kusambaa katika vijiji vilivyo jirani na mto huo.

Pinda atangaza mali zake

Friday, January 15, 2010 / Posted by ishak / comments (0)


WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda ametangaza mali zake alizonazo anazozimiliki mbele ya vyombo vya habari ofisini kwake jana.
Pinda alitangaza mali hizo zikiwemo na shilingi milioni 25 kwenye akaunti yake, nyumba tatu za kawaida moja ikiwa jijini Dar es Salaam, Mpanda na Dodoma na gari moja alilolinunua kwa mkopo.

Waziri Pinda aliamua kufanya hivyo ili kuweka bayana mali zake na kuonyesha mfano kwa viongozi wote nchini kufata kwa kuwa viongozi walitakiwa kuweka bayana mali zao ili kutekeleza sheria ya maadili ya uongozi.

"Hizo ndizo mali zangu nilizo nazo ndugu" alisema mbunge huyo wa Mpanda wakati akitangaza mali zake

Waziri mkuu aliyetambulika kwa jina la mtoto wa mkulima alitaja mali zake hizo na kusema haelewi yeye kwake utajiri ni nini na kusema mali hizo kwake anajiona ni tayari zimeshamtosheleza na wakati akianza kutaja mali zake hizo wka kujielezea mbele za wahariri alianza kwa kusema

"Nina nyumba Dodoma kutokana na utaratibu wa mikopo ya nyumba za serikali; nina nyumba Mpanda ambayo imepatikana kwa mpango wa kawaida tu, imetokana na visenti kidogo nikanunua pale ambapo bahati nzuri gharama za ujenzi hazikuwa kubwa sana, nikakikarabati kipo pale kipo Makanyagio pale."

"Haya! Ukitoka pale unataka niseme nini tena. Dar es Salaam sina nyumba ya kusema ya maana sana ukienda shambani Pugu kule kipo kinyumba kidogo hivyo inahitajika kazi ya ziada kuweza kufanya paonekane pa maana.

"Kijijini kwa baba yangu pale Kibaoni sina nyumba; pale mlipoona nimekaa na bibi tunapiga porojo, kile kijumba mimi na wadogo zangu tulimsaidia babu kwa ajili ya kumjengea babu yetu na pale ndipo nilipokuwa nafikia siku zote wakati wa likizo."

Pinda, ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 2000, alisema miaka yote alikuwa akifikia kwenye nyumba hiyo ambayo yeye ana chumba chake kimoja hali kadhalika babu yake.

Alisema baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu, alijikuta kwenye wakati mgumu sana kwa kuwa alitaka kuendelea kufikia kwenye nyumba hiyo, lakini watu wa usalama walimkataza.

"Baada ya hii maneno inayoitwa uwaziri mkuu, nilipoteuliwa nikataka nifikie pale katika ile nyumba, lakini nikaambiwa hapana; haiwezekani; hapafai; huwezi kufikia pale,"alisema.
Alisema hilo ndilo lilikuwa tatizo lake la kwanza kwa hiyo anajaribu kujenga tena kitu ambacho na yeye atapata mahala pa kufikia pamoja na wasaidizi wake kwenye eneo hilo.

"Nimegundua tatizo ni hawa wakubwa. Pale kijijini kwetu hakuna nyumba za wageni hatuna chochote mi nilidhani nikienda kule nikiachwa kwa babu na bibi, wao wataenda huko umbali wa kilomita wakatafute pa kupumzika, lakini wakasema no! no! no! haiwezekani, nikawaelewa," alisema.

Alisema ukiondoa nyumba hiyo, vitu vya maana zaidi hana labda gari la mkopo na ni gari la mbunge.
Pinda aliendelea kuwaambia wahariri kuwa

"Hivi ukifika hivi unahitaji nini cha zaidi tena? Kwa hiyo kipato kidogo unachokipata unaweza kukitumia kwa ajili ya huduma za watoto wako kusoma na kadhalika kwa sababu ni vitu viko nje ya taratibu za serikali. Kwa hiyo huwa najiona tu kwamba na mimi nina bahati tu kwamba Mungu alinifikisha hapa nilipofika na kunifikisha katika nafasi hii imenipa ahueni," alisema.

Alisema kama masuala hayo muhimu yanatimia, wajibu wake ni kujaribu kulipa fadhila kwa Watanzania kwa kufanya kila atakaloweza kuwatumikia vizuri zaidi.

"Kwa hiyo mimi nina hakika zaidi kuwa kwa nafasi kama niliyo nayo, naweza kuishi bila tamaa ya mambo mengine zaidi... mimi hata hisa sina, sijanunua hisa mahali popote, lakini huko tunakokwenda naweza nikatamani nikatafuta hata hisa hivi, kwa ajili labda ya sababu fulani fulani," alisema.


SOURCE.NIFAHAMISHE