Bikira Kuwa Sharti la Kuingia Shule za Sekondari

Friday, October 01, 2010 / Posted by ishak /

Wasichana waliopoteza bikira zao hawatapata nafasi za kujiunga na shule za sekondari za serikali nchini Indonesia iwapo muswada mpya wa sheria wa kuzuia vijana kuanza uzinzi mapema utapitishwa na bunge la nchi hiyo.
Muswada wa sheria umefikishwa bungeni nchini Indonesia ukitaka wasichana waliopoteza bikira zao wasiruhusiwe kujiunga na shule za sekondari nchini humo.

Muswada huo wa sheria umetolewa na mbunge wa jimbo la Jambi nchini humo Babang Bayu Suseno ambaye ameeleza kuwa muswada huo ukipitishwa kuwa sheria utasaidia kuzuia vijana kuanza uzinzi mapema.

Suseno alisema kuwa upatikanaji wa video na picha za ngono na ufahamu mdogo wa masuala ya dini umepelekea vijana kujihusisha na matendo ya ngono mapema.

Mbunge huyo ametaka wanafunzi wa kike wafanyiwe uchunguzi kuthibitisha bikira zao kabla ya kuruhusiwa kuingia shule za sekondari za serikali.

Hata hivyo muswada huo umekumbwa na upinzani mkubwa toka kwa wanasiasa na taasisi za kutetea haki za binadamu.

Imeelezwa kuwa kuwalazimisha wasichana kupima bikira zao itakuwa ni kuwabagua na ni kinyume cha haki za binadamu.

"Njia ya kuzuia uzinzi kwa vijana ni kwa kuwapa elimu ya masuala ya jinsia", alisema Seto Mulyadi, mkuu wa kitengo cha taifa cha kuwalinda watoto na kuongeza "Sio wasichana wote wanaoshiriki kwenye masuala ya ngono wanafanya hivyo kwa kupenda".

"Weka somo maalumu shuleni la kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kujilinda lakini sio kuwapima bikira", aliongeza Mulyadi.

Indonesia ni nchi yenye waislamu wengi kuliko wote duniani wapatao milioni 210. Wengi wao wana msimamo wa kati lakini wale wenye msimamo mkali wanahofia kuwa maendeleo ya kasi yanayoambatana na vijana kuiga umagharibi yanapelekea kupungua kwa msimamo wa kidini nchini humo.

Ili muswada huo upitishwe inabidi upewe sapoti ya gavana wa jimbo la Jambi pamoja na waziri wa masuala ya wanawake, lakini viongozi hao wawili ndio waliokuwa wa mwanzo kuupinga muswada huo.

source nifahamishe