Siri za Marekani Zaanikwa

Tuesday, November 30, 2010 / Posted by ishak /


Pamoja na serikali ya Marekani kuionya tovuti maarufu ya kutoboa siri zilizoficha ya WikiLeaks kutoziweka nyaraka zake za siri hadharani kwa kuwa maisha ya watu wengi yatakuwa hatarini, tovuti hiyo imezitoa nyaraka hizo za siri na kuiweka hadharani sura halisi ya Marekani.
Nyaraka za siri za Marekani zipatazo 250,000 zimeanza kuwekwa hadharani pamoja na serikali ya Marekani kuionya tovuti ya WikiLeaks kuwa inavunja sheria na inayaweka maisha ya watu wengi hatarini.

Tovuti ya WikiLeaks ambayo imebobea kwa kutoboa siri za ndani za masuala mbalimbali duniani ilikabiliwa na mashambulizi ya hackers ambao waliifanya tovuti hiyo ishindwe kupatikana online.

Hata hivyo nyaraka hizo za siri zimewekwa hadharani kama ilivyopangwa kwa kutumia magazeti ya The Guardian la Uingereza, gazeti la New York Times la Marekani, Der Spiegel la Ujerumani, El Pais la Hispania na gazeti la Le Monde la Ufaransa.

Nyaraka hizo za siri huenda zikaharibu uhusiano wa Marekani na baadhi ya viongozi wa nchi mbalimbali duniani ambao Marekani iliwapachika majina mbalimbali ya kuwakashifu.

Miongoni mwa nyaraka hizo za siri hizo ni mazungumzo ya siri kati ya Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia ambaye mara nyingi sana alikuwa akiishinikiza Marekani ipigane vita na Iran ili kuziteketeza silaha zake za nyuklia.

Taarifa hizo ziliendelea kusema kuwa Mfalme huyo wa Saudia aliishinikiza Marekani iiwekee Iran vikwazo vikali vya kiuchumi na kuwapiga marufuku viongozi wake kusafiri kimataifa.

Nyaraka hizo ziliendelea kusema kuwa Mfalme Abdullah aliungwa mkono na Mfalme wa Bahrain, Hamad ibn Isa Al Khalifa na Mtawala wa Abu Dhabi, Sheikh Mohammad bin Zayed ambao nao waliitaka Marekani iiteketeze Iran.

WikiLeaks pia ilitoa nyaraka ambazo zilisema kuwa Marekani kwa kuwatumia maafisa wake kinyume cha sheria iliwapeleleza viongozi wa baraza la Umoja wa Mataifa na hata kufikia kuchukua kwa siri alama za mboni ya jicho na alama za vidole za katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Marekani pia ilifuatilia simu walizokuwa wakipiga, fax, email na tovuti walizokuwa wakizitembelea.

Miongoni mwa majina ya kashfa waliyopachikwa viongozi wa serikali mbalimbali duniani, Marekani ilimuita Rais Mugabe wa Zimbabwe kuwa ni "Kichaa Mzee", kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi ameitwa "Mtu wa Ajabu Asiyeeleweka", wakati rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad amefananishwa na Hitler.

Nyaraka nyinginezo zilielezea jinsi Marekani ilivyokuwa ikizishinikiza baadhi ya nchi ziwachukue wafungwa wa kigaidi wa jela ya Guantanamo Bay. Nchi ya Slovenia ililazimishwa imchukue mfungwa mmoja wa Guantanamo Bay iwapo inataka kukutana na Rais Obama.

Nyaraka zaidi za siri zinazoonyesha jinsi Marekani ilivyokuwa ikivunja sheria za kimataifa zinaendelea kuchapishwa.

siurce nifahamishe