Babu wa Miaka 83 Amuua Mkewe Kwa Kumshindilia Bisibisi Kichwani

Wednesday, December 29, 2010 / Posted by ishak /

Babu mwanablogu mzee wa nchini Taiwan mwenye umri wa miaka 83 amemuua mkewe mwenye umri wa miaka 80 kwa kumshindilia bisibisi kichwani na kisha kuweka maelezo jinsi alivyofanya mauaji hayo kwenye blogu yake.
Babu Wang Ching-hsi mwenye umri wa miaka 83 wa nchini Taiwan kutokana na huruma yake aliamua kuyamaliza maisha ya mkewe mgonjwa wa kansa kwa kuizamisha bisibisi kwenye kichwa chake.

Kabla ya kufanya mauaji hayo, Babu Wang aliandika kwenye blogu yake kuwa hali ya mkewe imezidi kuwa mbaya na amepoteza hamu ya kuendelea kuishi duniani.

Babu Wang alimpa mkewe dawa za usingi na alipopitiwa na usingizi alimuua kwa kuizamisha bisibisi kwenye fuvu lake la kichwa.

Kwa mujibu wa magazeti ya Taiwan, Wang alipiga simu polisi kuwapa taarifa kuwa amemuua mkewe na alikaa nje ya nyumba yake akiwasubiri polisi wafike.

"Kwanini nimemuua mke wangu?, majibu yote yapo kwenye blogu yangu", alisema Wang akiwaambia waandishi wa habari wakati akiingizwa kwenye karandinga la polisi.

Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa, Wang alikubaliana na mkewe miaka kumi iliyopita kuwa kila mmoja wao afariki kwa amani muda utakapofika.

Katika makubaliano hayo, Wang alimwambia mkewe, "Muda utakapofika nitakuua".

Kumekuwa na mjadala mkubwa nchini Taiwan kuhusiana na haki ya mtu aliyechoka kuishi kusitisha maisha yake.

Mwezi juni mwaka huu, baraza la kutunga sheria la Taiwan lilipitisha sheria ya kuwaruhusu wagonjwa na ndugu wa mgonjwa aliyekuwa mahututi kwa magonjwa yaliyofikia kikomo, kusitisha kuwapa dawa au huduma za kurefusha maisha yao ili kuwaepusha na mateso wanayopata.


source nifahamishe