Maalim Seif ataka kusaidiwa mzigo

Sunday, December 12, 2010 / Posted by ishak /


KATIKA hali inayoashiria kuelemewa na mzigo wa majukumu, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amekiomba chama chake, kumtafuta mtu wa kumsaidia katika nafasi hiyo, wakati kikisubiri uchaguzi wake.

Rai hiyo imekuja huku Katibu Mkuu Msaidizi wa CUF, Juma Haji Duni, akiwa ameteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Utabibu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Uteuzi huo umefanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo mbele ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipimba katika kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, mtendaji huyo wa CUF pia alilitaka baraza kujipanga kwa uchaguzi mkuu ujao.

Maalim Seif alisema mtu atakayepata nafasi hiyo ya kumsaidia kwa muda lazima atambue kuwa nafasi hiyo itakuwa bado mikononi mwake (Seif) hadi atakapoyaachia rasmi majukumu ya umakamu wa Rais wa Zanzibar.

"Katibu mkuu atakayepata nafasi ya kuteuliwa, ajue yeye si Katibu Mkuu wa CUF, katibu mkuu nitabaki kuwa ni mimi hadi nitakapoiachia nafasi hii rasmi kwa kufuata utaratibu,"alisema Maalim Seif.

Alimuomba mwenyekiti kwa kushirikiana na baraza, kumsaidia katika kumtafuta au kumpendekeza mtu atakayemsaidia katika nafasi hiyo.

Katika kikao hicho, kiongozi huyo pia alimshukuru Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Dk Shein kwa kuweka uwiano mzuri katika uteuzi wa Baraza la Mawaziri na kwamba uteuzi huo, utaleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema CUF imepata mafanikio makubwa katika uteuzi huo kwa kuwa umepata nafasi ya kuongoza nchi na kwamba kwa sasa Zanzibar inaongozwa na vyama vya CCM na CUF tofauti na miaka ya nyuma ambapo nchi ilikuwa ikiongozwa na chama kimoja.

"Chama chetu ni miongoni mwa vyama viwili vinavyoongoza serikali, kwa hiyo tujivunie ushindi wetu kwani tumetimiza malengo ya CUF ya kushika madaraka ya nchi, tangu tukiunde tumejaribu mara tatu tukashindwa lakini mwaka huu tumeweza,"alisema.

Hata hivyo, alisema ushindi huo ni changamoto kwa CUF na kwamba wote waliopata uongozi wanapaswa kubeba majukumu na kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi bila kubagua.

Alisema uteuzi wa mawaziri nane kutoka chama hicho ni mkubwa sana hasa ikizingatiwa kuwa Rais Dk Shein, alikuwa na uwezo wa kufanya lolote katika uteuzi huo.

"Mimi ni Makamu wa Kwanza wa Rais, nitamsaidia Rais wangu kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na mawaziri wote bila kuangalia kama ni wa CCM au CUF, nina hakika sote kwa pamoja tutaleta mabadiloko,"alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF (Lipumba) alimpongeza Maalim Seif kwa kuonyesha ukomavu wa siasa wakati wa kusubiri matokeo ya kura na baada ya kutangazwa kwa kutoa hotuba ya kihistoria tofauti na matarajio ya watu weng.

Alisema baadhi ya waty walidhani kuwa kauli yake ingeleta maafa.

"Tunampongeza kwa kuhakikisha kuwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar yanakuwa mbele badala ya maslahi binafsi kuchukua nafasi. Pia tunampongeza Dk Shein kwa ushirikiano aliotuonyesha katika kuunda baraza lake la mawaziri," alisema.

Alifafanua kuwa mafanikio ya CUF ni matokeo ya maridhiano mazuri yaliyofanywa na Katibu mkuu wa chama na Rais mstaafu wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.


Alisema kuwa CUF imefungua njia, ili kwa pamoja wannchi wa Zanzibar, waweze kutatua matatizo yao na kuondokana na umaskini.

source mwananchi