Mfanyabiashara maarufu Zanzibar atinga kizimbani

Sunday, June 19, 2011 / Posted by ishak /

Mfanyabiashara maarufu mjini Zanzibar Suleyum Mbarak Salim (35) amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuiibia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Sh bilioni 2.7.
Mfanyabiashara huyo, maarufu kama Morgan alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu, Amisa Suleima Hemed wa Mahakama ya mkoa mjini Magharibi Unguja jana.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Maullid Mkame alisema mshtakiwa huyo anadaiwa kuiibia benki ya watu wa Zanzibar kati ya Machi 12 na Mei 11, 2009.
Alisema kwamba mstakiwa aliiba dola za Marekani 122,000 sawa na sh bilioni 2.7, ikiwa ni mali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kitendo ambacho ni kinyume na sheria namba 6 kifungu namba 124 (1) (4) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004. Mshtakiwa alikana shtaka hilo ambapo wakili anayemtetea Suleiman Salum aliomba mteja wake kupatiwa dhamana kwa vile shtaka alilofunguliwa ni miongoni mwa makosa yenye dhamana na haki yake kwa mujibu wa katiba.
Salum alisema kwamba mshtakiwa hajawahi kuhusishwa na mashtaka yoyote au kutiwa hatiani kwa kosa lolote na kuomba hakimu kumpatia dhamana mteja wake kwa vile ana mali zisizohamishika.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka, Maulid Makame alisema kwamba kwa muda mrefu, mshtakiwa huyo alikuwa akisakwa baada ya kuhusishwa na kesi namba 115 inayohusu wizi katika benki hiyo ya Zanzibar iliyofunguiliwa mwaka 2009 na kuwahusisha wafanyakazi wawili wa benki hiyo.
Alisema kitendo cha kumpa dhamana kinaweza kuathiri upelelezi hasa kwa kuzingatia uchunguzi wa suala hilo haujakamilika na mshtakiwa alikuwa anasakwa muda mrefu.
Hata hivyo, Hakimu Amisa alisema atatoa uamuzi juu ya ombi la dhamana Juni 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena katika mahakama ya Vuga mjini Zanzibar.



source ippmedia

0 comments:

Post a Comment