Zaidi ya watu 11 wamefariki dunia nchini Nigeria kufuatia bomu kubwa lililolipuka kwenye baa wakati watu wakisherehekea mwaka mpya.
Zaidi ya watu 11 wamefariki dunia kufuatia bomu kubwa lililolipuka kwenye baa iliyopo karibu na kambi ya jeshi iliyopo karibu na ikulu mjini Abuja.
Eneo hilo lilikuwa likisemekana kuwa ndilo lenye usalama kuliko maeneo yote ya mji wa Abuja.
Wakati wa krismasi wiki iliyopita zaidi ya watu 80 walifariki dunia nchini Nigeria kutokana na milipuko ya mabomu katika mji wa Jos ambao umekumbwa na chuki ya kidini kati ya waislamu na wakristo.
Katika bomu lililotokea mkesha wa mwaka mpya, inakadariwa kuwa watu 30 wamepoteza maisha yao ingawa taarifa ya polisi ilithibitisha vifo vya watu 11.
Bomu hilo lilitokea muda mfupi kabla ya mwaka mpya wakati watu wakiwa wanajiburudisha baa wakisubiri kusherehekea mwaka mpya 2011.
Waziri wa ulinzi wa Nigeria amewataka watu wadumishe utulivu wakati uchunguzi mkali ukiendelea kuhusiana na milipuko ya mabomu ambayo imekuwa ikiiandama Nigeria siku za karibuni.
source nifahamishe
11 Wafariki Wakisherehekea Mwaka Mpya Nigeria
Auanza Mwaka Mpya Vibaya Kwa Operesheni ya Kuongeza Makalio
Mwanamke mmoja wa nchini Marekani ambaye alitaka kuingia mwaka 2011 akiwa mrembo zaidi na mwenye makalio makubwa amefariki dunia masaa matatu baada ya kufanyiwa operesheni ya kuongeza makalio.
Mwaka 2011 umeanza vibaya kwa bwana Osvaldo Vargas mkazi wa Florida, Marekani, Amempoteza mke wake ambaye operesheni ya kuongeza urembo na makalio ili aonekane mrembo zaidi mwaka 2011 ilimalizika vibaya na kupelekea kifo chake.
Lidvian Zelaya mwenye umri wa miaka 35 alitaka kuingia mwaka 2011 akiwa mrembo zaidi kwa kuamua kufanya operesheni ya kutoa nyama nyama na mafuta toka kwenye tumbo lake na kuzihamishia kwenye makalio yake ili kuyafanya yawe makubwa zaidi.
Masaa matatu baada ya operesheni hiyo, Lidvian aliwahishwa hospitali akiwa amezidiwa sana na wakati mume wake anawasili hospitali Lidvian alikuwa ameishafariki dunia.
"Amefariki akitafuta urembo, kwangu mimi alikuwa tayari ni mrembo", alisema mume wa Lidvian kwa huzuni.
"Alikuwa ni mrembo, mwenye furaha na aliyependa kudansi, nataka kujua nini kimetokea", alisema bwana Oswaldo wakati akiongea na waandishi wa habari.
"Hatumlaumu yeyote lakini tunataka kujua nini kimesababisha kifo chake", alisema Oswaldo akiwa pamoja na mwanasheria wake.
Lidvian alifanyiwa operesheni kwenye kliniki ya Strax Rejuvenation, ya Florida, hata hivyo kliniki hiyo imesema kuwa sheria zinawabana kusema chochote kuhusiana na kifo cha Lidvian.
source nifahamishe
Babu wa Miaka 83 Amuua Mkewe Kwa Kumshindilia Bisibisi Kichwani
Babu mwanablogu mzee wa nchini Taiwan mwenye umri wa miaka 83 amemuua mkewe mwenye umri wa miaka 80 kwa kumshindilia bisibisi kichwani na kisha kuweka maelezo jinsi alivyofanya mauaji hayo kwenye blogu yake.
Babu Wang Ching-hsi mwenye umri wa miaka 83 wa nchini Taiwan kutokana na huruma yake aliamua kuyamaliza maisha ya mkewe mgonjwa wa kansa kwa kuizamisha bisibisi kwenye kichwa chake.
Kabla ya kufanya mauaji hayo, Babu Wang aliandika kwenye blogu yake kuwa hali ya mkewe imezidi kuwa mbaya na amepoteza hamu ya kuendelea kuishi duniani.
Babu Wang alimpa mkewe dawa za usingi na alipopitiwa na usingizi alimuua kwa kuizamisha bisibisi kwenye fuvu lake la kichwa.
Kwa mujibu wa magazeti ya Taiwan, Wang alipiga simu polisi kuwapa taarifa kuwa amemuua mkewe na alikaa nje ya nyumba yake akiwasubiri polisi wafike.
"Kwanini nimemuua mke wangu?, majibu yote yapo kwenye blogu yangu", alisema Wang akiwaambia waandishi wa habari wakati akiingizwa kwenye karandinga la polisi.
Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa, Wang alikubaliana na mkewe miaka kumi iliyopita kuwa kila mmoja wao afariki kwa amani muda utakapofika.
Katika makubaliano hayo, Wang alimwambia mkewe, "Muda utakapofika nitakuua".
Kumekuwa na mjadala mkubwa nchini Taiwan kuhusiana na haki ya mtu aliyechoka kuishi kusitisha maisha yake.
Mwezi juni mwaka huu, baraza la kutunga sheria la Taiwan lilipitisha sheria ya kuwaruhusu wagonjwa na ndugu wa mgonjwa aliyekuwa mahututi kwa magonjwa yaliyofikia kikomo, kusitisha kuwapa dawa au huduma za kurefusha maisha yao ili kuwaepusha na mateso wanayopata.
source nifahamishe
Jela Miaka Mitano Kwa Kusoma Email ya Mkewe
Mwanaume mmoja wa nchini Marekani ambaye alifungua email ya mkewe na kugundua kuwa mkewe alikuwa akifanya mapenzi nje ya ndoa, anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela.
Leon Walker mwenye umri wa miaka 33 mkazi wa Michigan nchini Marekani anakabiliwa na kifungo cha miaka mitano jela kwa kufungua na kusoma email za mkewe.
Leon alifungua email ya mkewe, Clara Walker, kwa kutumia kompyuta waliyokuwa wakiitumia pamoja nyumbani kwao.
Kwa kutumia password yake, Leon alifungua akaunti ya Gmail ya mkewe na alisoma email zake ambapo aligundua kuwa mkewe alikuwa akitembea nje ya ndoa.
Mkewe alikasirika baada ya siri hiyo kufichuka na aliamua kufungua kesi ya madai ya talaka ambapo pia alimfungulia Leon mashtaka ya kusoma email zake.
"Hii ni kesi ya kustaajabisha, hakuna sheria inayoweka wazi suala kama hili", alisema mwanasheria Frederick Lane.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hii ni mara ya kwanza sheria dhidi ya wizi wa nyaraka za siri kwenye masuala ya kibiashara inatumika kwenye masuala ya kifamilia.
Baadhi ya wanasheria wanasema kuwa huenda Leon akahukumiwa kwenda jela miaka mitano iwapo atapatikana na hatia ya kutumia password ya mkewe kusoma email zake.
Leon akiongea na waandishi wa habari alisema kuwa alichungulia email za mkewe ili aweze kujua chanzo cha mkewe kuwatelekeza watoto wao.
Kesi ya Leon itaanza kusikilizwa februari 7 mwakani.
source nifahamishe
SIRI ZA MTANDAO WA WIKILEAKS: aliyemhoji Dk Hoseah ni jasusi aliyebobea
WAKATI wananchi wakimkosoa mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah kupinga taarifa ya Wikileaks iliyovujisha mazungumzo yake na ofisa wa ubalozi wa Marekani, imebainika kuwa Mmarekani huyo amepikwa "kijasusi" katika masuala ya usalama wa taifa, uhusiano wa kimataifa, jeshi na ni ofisa mwandamizi.
Ofisa huyo, D. Purnell Delly alipeleka taarifa ya mazungumzo nchini Marekani akiripoti kuwa DK Hoseah amemwambia kuwa Rais Jakaya Kikwete hayuko tayari kuachia sheria ichukue mkondo wake katika kuwashtaki vigogo wanaojihusisha na rushwa.
Dk Hoseah, ambaye kwenye taarifa hiyo anadai kutishiwa maisha kiasi cha kufikiria kuikimbia nchi, amekiri kuongea na ofisa huyo lakini akadai kuwa ofisa huyo alimkariri tofauti na alivyosema.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Dk Hoseah amefafanua kuwa alichokisema ni kwamba Rais Kikwete hayuko tayari kuidhinisha vigogo wanaojihusisha na rushwa kufikishwa mahakamani bila ya kuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yao.
Ubalozi wa Marekani umekataa kuzungumzia taarifa hizo za mawasiliano zilizovujishwa na mtandao wa Wikileaks ukisema kuwa hauna maelezo yoyote, kwa mujibu wa mkurugenzi wa kitengo cha mahusiano ya jamii cha ubalozi huo, Ilya D. Levin.
Ikulu ya Dar es salaam nayo haikutaka kuzungumzia suala hilo baada ya Mwananchi kuwasiliana na mwandishi wake, Premmy Kibanga.
Lakini Mwananchi imebaini kuwa ofisa huyo ni mzoefu katika kazi na amepitia mafunzo mbalimbali kiasi cha kumfanya aaminiwe na taifa hilo kubwa kufanya kazi hiyo inayofanana na ya kijasusi kwenye nchi tofauti, baadhi zikiwa ni zile zenye matatizo ya amani.
Taarifa ya Delly kwenda Ikulu ya Marekani ilivujishwa na mtandao wa wikileaks ambao umepata umaarufu mkubwa kwa kutoa siri za serikali mbalimbali duniani.
D. Delly alikuwa mkuu wa ujumbe wa wanadiplomasia wa Marekani kwenye Ofisi za ubalozi jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 9, mwaka 2005.
Kabla ya kuja Dar es Salaam kufanya kazi hiyo ya diplomasia, alikuwa msaidizi maalumu wa katibu msaidizi wa masuala ya Afrika kwenye Idara ya Serikali ya Marekani jijini Washington. Alipata nafasi hiyo baada ya kutumikia cheo cha naibu mkuu wa ujumbe wa Marekani jijini Khartoum, Sudan.
Delly alijiunga na idara hiyo mwaka 1983. Awali alikuwa mshauri wa mambo ya siasa na uchumi wa Copenhagen; naibu mshauri wa masuala ya Uchumi jijini Ankara, Uturuki na ofisa katika dawati maalumu nchini Sri Lanka.
Pia alifanya kazi hizo katika miji ya Edinburgh na El Salvador wakati wa vita na akajizolea heshima kubwa na hivyo kutunukiwa tuzo ya ujasiri na utumishi uliotukuka.
Dk Hoseah alieleza kuwa alikaririwa vibaya na ofisa huyo, lakini taarifa zinaonyesha kuwa Delly, ambaye anatokea Jimbo la Virginia, ni mtaalamu wa lugha akiwa amepata shahada yake ya kwanza katika Fasihi ya Lugha ya Kirusi kwenye Chuo Kikuu cha Dartmouth na shahada ya uzamili ya fasihi katika Chuo Kikuu cha Chicago.
Pia Mmarekani huyo alisomea Sheria za Kimataifa kwenye Chuo cha William na Mary, na shahada ya Uzamili ya Usalama wa Kimataifa na Uandaaji wa Mikakati ya Kijeshi katika chuo cha Newport, Rhode Island ambako wanafundishwa askari wa majini.
Chuo cha US Naval alichosomea Delly, ambaye alikuwa mwanachama na mwalimu wa vikosi vya ulinzi vya mwambao wa Marekani, kina kazi ya kuzalisha viongozi wa kuandaa Mikakati ya kijeshi na namna ya kuitekeleza.
Chuo hicho hutoa programu za fani za kijeshi zinazokwenda na wakati, usahihi, mahususi na zinazotekelezeka kwa idadi kubwa ya maofisa wa kijeshi wa Marekani, askari waajiriwa wa majini, waajiriwa raia ndani ya serikali ya Marekani na hata katika taasisi zisizo za kiserikali (NGOs), pamoja na maofisa wa kimataifa.
Chuo hicho hutarajia kupata kundi la viongozi wenye sifa ya uaminifu na kujiamini katika kila jukumu lao na wenye akili za kiutendaji na kimkakati, wenye tafakuri tunduwizi, uwezo mkubwa katika kuunganisha mambo na wapiganaji katika vita.
Mtaala wa chuo umegawika katika kozi kuu tatu za masomo; mikakati na sera, usalama wa taifa katika kufanya maamuzi na namna ya kuunganisha operesheni za kijeshi.
Kozi ya Mikakati na Sera imewekwa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi kufikiria kulingana na mikakati kuhusu nadharia za kijeshi kuanzia mwanzo wa vita katika bahari kati ya Athens na Sparta hadi sasa. Lengo ni kuweka uhusiano kati ya Malengo ya Taifa kisiasa na namna ambayo mbinu zake za jeshi zinakuwa mahususi kutumika ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa (Ushindi).
Kozi ya pili ya Usalama wa Taifa katika Maamuzi imewekwa kwa ajili ya kuwasaidia watendaji wakuu katika jeshi na wananchi kukabiliana na hoja za kisiasa, kiuchumi, na kijeshi katika kufanya maamuzi sahihi kwenye masuala ya Usalama wa Taifa.
Kozi ya tatu ya kuunganisha operesheni za kijeshi inawasaidia wakuu wa taasisi za kijeshi kutafsiri mikakati ya kijeshi na hasa ya kikanda katika vita vya majini.
Karibu nusu ya wanafunzi wanaotoka Marekani ni maofisa kutoka jeshi, vikosi vya anga, majini, ulinzi wa mwambao na katika meli na kampuni na wakala wa ulinzi binafsi.
Uzoefu huo wa kazi na elimu kubwa ya ofisa huyo wa Marekani ulimfanya mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim Lipumba kutokuwa na wasiwasi na ripoti ya Delly kwenda Ikulu ya Marekani.
“Delly hana sababu ya kumzulia Hoseah. Ni mzoefu na anajiamini katika kazi zake; haya ya kusema kwamba nimenukuliwa vibaya, ni ujanja ujanja wa kulindana tu,” alisema Profesa Lipumba ambaye alisomea shahada yake ya uzamili, akijikita katika uchumi kwenye Chuo Kikuu cha nchini Marekani.
“Yale yaliyoandikwa katika mtandao wa Wikileaks na baadaye kuchapishwa katika gazeti la The Guardian la Uingereza ni ya kweli ya Dk Hoseah na yale ya kukanusha ni ya kulindana.”
Prof Lipumba alidai kuwa ni kweli Rais Kikwete hayuko tayari hata siku moja kuona rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa au waziri mkuu wake, Frederick Sumaye wakisimamishwa mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi.
Alisema mambo hayo yanafanana kabisa na yaliyoandikwa katika gazeti hilo mwaka 2007 kwamba Hoseah anatembea na mlinzi mwenye silaha kutokana na kuhofia usalama wake.
“Jambo la msingi ambalo tunaliona hapa ni kwamba tuna udhaifu mkubwa katika uongozi na viongozi hawana utashi na ujasiri wa kupambana na rushwa... Hoseah na hata Kikwete hawawezi kupambana,” alisemai.
“Fedha ile (dola 12.4 milioni alizolipwa Shailesh Vithlani katika ununuzi wa rada) haina mjadala kuwa ni rushwa, ni rushwa ambayo alilipwa Vithlani kifisadi kufanikisha zabuni ya uuzaji wa rada kwa serikali ya Tanzania.”
Wakili wa siku nyingi nchini, Profesa Abdallah Safari alisema kuna uwezekano mkubwa kuwa taarifa iliyotolewa na mtandao huo ni ukweli.
"Kuamini utetezi wa Dk Hoseah ni vigumu kutokana na mwenendo wake," alisema Profesa Safari. "Alijaribu kumsafisha (mwanasheria na mbunge wa Bariadi Magharibi) Andrew Chenge katika kashfa ya rada.
“Amekuwa akitofautiana na ripoti mbalimbali mpaka za bunge kama ile ya Richmond. Kwa hiyo CCM ni watu wasioaminika na serikali yao... wana mambo yao bwana.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alitazama suala hilo katika sura tatu, akielezea sura ya kwqanza kuwa ni nchi za Kiafrika kuanzisha taasisi zisizo huru na zinazoendeshwa kwa kutegemea msaada wa wahisani, akitoa mfano wa Takukuru.
“Hata ukisoma hiyo taarifa kwa umakini kwenye mtandao, utona kabisa kuwa Dk Hoseah alikuwa anajipendekeza kwa ajili ya kulinda ufadhili,” alisema Bashiru.
Alisema endapo Takukuru ingekuwa ni taasisi huru na inayojitegemea kwa kila kitu, basi kusingekuwa na sababu ya mkurugenzi wake kuzungumza na Wamarekani.
Katika mtazamo wake wa pili, Bashiru alisema wasomi, wanahabari na wanasiasa wana kazi kubwa ya kuangalia lengo la mtandao huo kufichua habari kama hizo zinzolihusu bara la Afrika na Asia.
“Lazima tujiulize kwa nini hizi siri zinafichuliwa wakati huu/ kwa nini Marekani na nchi kama Uganda, Iraq na Tanzania; kwa nini hakuna siri za Marekani na nchi nyingine tajiri kusema ni jinsi gani wanavyopanga kutugandamiza,” alisema Bashiru.
Kwa sura ya tatu, Bashiru alisema inakuwa vigumu kwa sasa kuangalia hatima ya mapambano ya rushwa, akisema ni lazima mtu ajitoe mhanga katika vita ya rushwa na kwamba kama hakuna dhamira ya kweli, huwezi kupambana.
“Dk Hoseah amekanusha baadhi ya mambo kwa hiyo labda tusubiri wamarekani wenyewe watuambie kama wamemlisha maneno, lakini kweli kwenye mapambano ya rushwa lazima mambo ya kutishiana maisha yawepo kwa sababu yanahusu watu wazito,” alisema Bashiru.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya kukuza demokrasia nchini Agenda Participation 2000, Moses Kulaba alisema mtandao huo umefungua macho ya Watanzania.
Alisema siri zilizofichuliwa zimekuwa uthibitisho wa masuala ambayo Watanzania walikuwa wakiyawaza kwa muda mrefu.
“Mimi mwenyewe nimeusoma ule mtandao, bado kuna mengi ni mapema mno kwa Dk Hoseah kuanza kukanusha,” alisema Kulaba.
Hussein Kauli
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitivo cha Uchumi, Adolf Mkenda alimtaka Dk Hoseah ajiuzulu iwapo ni kweli alimuelezea Rais Kikwete kuwa hapendi vita dhidi ya rushwa.
Mkenda alisema kitendo cha Dk Hoseah kueleza mambo ya ndani kwa maofisa wa ubalozi wa Marekani wakati anajua yeye anawajibika kwa serikali ni ukiukwaji wa maadili ya kazi yake na hivyo anapaswa kuwajibika kwa kujiuzulu.
“Ni jambo la ajabu sana kwa Dk Hoseah kufanya kitendo hicho, kama taarifa hizi ni za kweli inabidi ajiuzulu mwenyewe kwani hafai kuendelea kuiongoza Takukuru” alisema Mkenda na kuongeza kuwa iwapo atajiwajibisha, serikali haina budi kumchukulia hatua.
Mkenda pia alieleza kuwa kama Rais Kikwete hapendi sheria ichukue mkondo wake katika vita dhidi ya rushwa, amekiuka katiba.
source mwananchi
Thamani ya Shilingi ya Tanzania imepanda mfululizo kwa muda wote wa wiki mbili zilizopita tokea Desemba 3 Mwaka huu ukilinganisha na Dola ya Kimarekani.
Kwa mujibu wa takwimu zinazotolewa kila siku na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kiwango cha kubadilisha fedha Desemba 2, kilikuwa Shilingi 1,487.55 kwa Dola moja, lakini Desemba 3, kilishuka na kufikia Shilingi1,485.23 upungufu wa shilingi 2.32.
Hadi kufikia Desemba 10, Dola ilibadilishwa kwa shilingi 1,477.22, pungufu kwa shilingi 8.01 ikilinganishwa na kiwango cha ubadilishanaji wa shilingi kwa dola wa Desemba 3 uliokuwa shilingi 1,485.23.
Kuanzia Desemba 13 hadi jana thamani ya Shilingi ilipanda kwa kasi kubwa ambapo Desemba 13 dola ya Kimarekani ilibadilishwa kwa Shilingi1,466.23, Desemba 14 ilibadilishwa kwa Shilingi 1,455.72, Desemba 15 ilibadilishwa kwa Shilingi 1,443.39 na jana dola ilibadilishwa kwa Shilingi1,432.42.
Hivyo takwimu hizi za Bot zinamaanisha kuwa thamani ya fedha yetu imeimarika ukilinganisha na dola ya Kimarekani kwa kipindi hiki cha wiki mbili zilizopita.
Kupanda huku kwa thamani ya shilingi mfululizo unakinzana na namna ilivyoporomoka kwa haraka mwanzoni mwa Agosti wakati harakati za uchaguzi zilipoanza hadi kura zilipopigwa na kuendelea hivyo hadi mwanzoni mwa mwezi huu.
source nipashe