Ukiwa Mchungaji Kanisani Nigeria, Utajiri Nje Nje

Thursday, June 23, 2011 / Posted by ishak / comments (0)



Mchungaji tajiri kuliko wote Nigeria, Mchungaji David Oyedepo

Uchunguzi uliofanywa nchini Nigeria umebaini kuwa wachunga kondoo wa Bwana nchini humo mbali ya kuhubiri neno la bwana wanatengeneza pesa ya maana kiasi cha kwamba baadhi yao wanamiliki ndege, hoteli na biashara kubwa.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Muandishi wa Nigeria wa jarida la Marekani la masuala ya uchumi, Forbes, wahubiri wa neno la bwana nchini Nigeria wanatengeneza pesa sana kutokana na uchungaji kiasi cha kufanananishwa na matajiri wa biashara ya mafuta.

Mfonobong Nsehe akitoa ripori ya uchunguzi wake alisema kuwa wachungaji wa Nigeria wanaishi maisha ya kifahari na wana miradi mikubwa ya kibiashara.

"Kuhubiri ni biashara inayolipa sana, sawa sawa na biashara ya mafuta", alisema Nsehe.

Utajiri wa wachungaji watano maarufu nchini Nigeria unakadiriwa kufikia dola milioni 200, alisema Nsehe.

Makanisa mengi yameibuka nchini Nigeria na waumini wamekuwa wakiongezeka.

Nsehe alisema kuwa mchungaji tajiri kuliko wote ni Mchungaji David Oyedepo wa kanisa la Living Faith World Outreach Ministry, ambaye utajiri wake ni dola milioni 150.

Mchungaji Oyedepo ndiye anayeshika nafasi ya pili akimiliki ndege nne, kampuni ya uchapishaji, chuo kikuu na shule moja na majumba ya kifahari jijini London na Marekani.

Mchungaji Chris Oyakhilome wa kanisa la Loveworld Ministries ana utajiri unaokadiriwa kuwa kati ya dola milioni 30 na 50. Mchugaji Oyakhilome anamiliki kampuni ya magazeti na majarida, stesheni ya televisheni, hoteli na kampuni ya majumba.

"Wachungaji hawa wanaishi maisha ya kifahari utawaona kwenye ndege zao binafsi na magari ya kifahari", alisema Nsehe.

Wachungaji wengine walioingia kwenye listi ya utajiri ni mchungaji Temitope Joshua Matthew mwenye utajiri kati ya dola milioni 10 na 15, Mchungaji Matthew Ashimolowo dola milioni 6-10, na mchungaji Chris Okotie mwenye utajiri kati ya dola milioni 3-10.

Nsehe aliongeza kuwa wawakilishi wa wachungaji wote isipokuwa mchungaji Ashimolowo, wamethibitisha taarifa ya umiliki wa mali za wachungaji hao.


source nifahamishe

Mfanyabiashara maarufu Zanzibar atinga kizimbani

Sunday, June 19, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Mfanyabiashara maarufu mjini Zanzibar Suleyum Mbarak Salim (35) amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuiibia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Sh bilioni 2.7.
Mfanyabiashara huyo, maarufu kama Morgan alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu, Amisa Suleima Hemed wa Mahakama ya mkoa mjini Magharibi Unguja jana.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Maullid Mkame alisema mshtakiwa huyo anadaiwa kuiibia benki ya watu wa Zanzibar kati ya Machi 12 na Mei 11, 2009.
Alisema kwamba mstakiwa aliiba dola za Marekani 122,000 sawa na sh bilioni 2.7, ikiwa ni mali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kitendo ambacho ni kinyume na sheria namba 6 kifungu namba 124 (1) (4) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004. Mshtakiwa alikana shtaka hilo ambapo wakili anayemtetea Suleiman Salum aliomba mteja wake kupatiwa dhamana kwa vile shtaka alilofunguliwa ni miongoni mwa makosa yenye dhamana na haki yake kwa mujibu wa katiba.
Salum alisema kwamba mshtakiwa hajawahi kuhusishwa na mashtaka yoyote au kutiwa hatiani kwa kosa lolote na kuomba hakimu kumpatia dhamana mteja wake kwa vile ana mali zisizohamishika.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka, Maulid Makame alisema kwamba kwa muda mrefu, mshtakiwa huyo alikuwa akisakwa baada ya kuhusishwa na kesi namba 115 inayohusu wizi katika benki hiyo ya Zanzibar iliyofunguiliwa mwaka 2009 na kuwahusisha wafanyakazi wawili wa benki hiyo.
Alisema kitendo cha kumpa dhamana kinaweza kuathiri upelelezi hasa kwa kuzingatia uchunguzi wa suala hilo haujakamilika na mshtakiwa alikuwa anasakwa muda mrefu.
Hata hivyo, Hakimu Amisa alisema atatoa uamuzi juu ya ombi la dhamana Juni 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena katika mahakama ya Vuga mjini Zanzibar.



source ippmedia

UZURI WA KUMSAMEHE MPENZI WAKO............

Sunday, June 12, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Ni vizuri kusamehe na kusahau ili uweze kuishi maisha ya furaha na amani.

Katika maisha inapotokea kuna mtu amekukera inawezekana akawa ni mwenza wako lakini baadaye akakuomba msamaha kwa kile alichokosea kama kweli umeamua kumsamehe basi ni vizuri kujiepusha kuwa na kinyongo yaani ile hali ya kusamehe huku bado moyoni kile kitu unacho kinakusumbua na wakati mwingine labda unayo nia ya kulipiza kisasi au bado unapenda kuzungumzia makosa ya zamani wakati ulishasamehe haipendezi kuwa na tabia ya kutosahau baada ya kusamehe kwani hata wewe mwenyewe binafsi unakuwa hujitendei haki kwani unajidanganya na pia utaendelea kuuumia kutokana na kushindwa kusahau naamini huwa inakuwa ni vigumu kusahau kulingana na uzito wa kosa lakini kama umeamua kusamehe basi samehe kwa moyo wako wote ili uweze kuwa huru na yule umpendaye .

MAZINGIRA USIYOTAKIWA KABISA KUANZISHA UHUSIANO KIMAPENZI

Tuesday, June 07, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Wengi kati ya watu ambao hukumbwa na majuto ya “ningejua nisingemkubali” ni wale wanaoanzisha uhusiano wa kimapenzi kwenye mazingita yasiyostahili.
Wataalamu wa mapenzi wanasema, penzi sahihi lazima liambatane na wakati muafaka wa kufanya hivyo. Ukikosea katika kupima mazingira unakuwa kwenye asilimia 80 za kuchagua mtu asiyekufaa maishani mwako.
Leo kwa kutambua umuhimu wa mada hii nimeona niwaletee mazingira ambayo hayafai mtu kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, lengo langu likiwa ni kuweka umakini katika kuchagua na kuondoa, kupunguza majuto ya kuumizwa na mapenzi.


KWENYE MGOGORO
Uchunguzi unaonesha kuwa asilimia 60 -70 ya wapenzi huanzisha uhusiano mpya wa kimapenzi nyakati za migogoro baina ya wapendanao kwa lengo la kupoza maumivu.
Msomaji wangu, ni jambo la hatari sana kuanzisha uhusiano kwenye mazingira ya mgogoro kwani utakapofanya hivyo utapoteza umakini na hivyo kujikuta ukijiingiza kwenye uhusiano usiokuwa na faida ya baadaye kwako.

UKIWA NA HISIA KALI
Kama binadamu kamili kuna wakati tunakuwa kwenye msukumo mkubwa wa hisia za kimapenzi, kila umuonaye anaweza kukushawishi si kwa sababu anakufaa lakini njaa ya penzi isiyohitaji kuchagua itakuwa inakusukuma kujishibisha hata kwa maganda.
Epuka kabisa kusukumwa na mhemko wa mwili, usikubali kuwa mtumwa wa hisia kwani utajikuta umempa penzi mtu ambaye hata wenzako watashangaa jinsi ulivyoangukia pua.

UNAPOKUWA UMELEWA
Mazingira ya ulevi ni hatari sana, watu wengi hufanya ngono zembe bila kuangalia madhara yake wakati wakiwa wamelewa. Nashauri kwamba, unapokwenda baa jambo la kwanza kabisa unalotakiwa kulihifadhi kwenye akili yako ni kutojiingiza kwenye uhusiano mpya wa kimapenzi.

Katika maisha yangu ya ushauri nimekutana na watu wengi sana wakikiri kuambukizwa magonjwa ya zinaa walipokuwa wamelewa.
Nakushauri msomaji wangu kwamba, usikubaliane kabisa ulevi ukuingize kwenye masuala la kimapenzi. Acha starehe ya pombe pekee ikifurahishe, ukitaka vyote utaamka umefanya jambo la ajabu litakalokuhuzunisha maisha yako yote.

SIKU ZA UPWEKE
Nafahamu kuwa, harakati za kimaisha huwatengenisha wapenzi na kujikuta wakiwa wapweke kwa muda. Kipindi hiki kinaweza kuwa cha mwenza kwenda masomoni au safari ya kikazi. Ni kipindi cha kujaribiwa imani.

Jambo baya kabisa ni kuona, eti wapenzi waliotenganishwa na changamoto za kimaisha kujiona wapweke na kuamua kutafuta wachezaji wa nje wawasaidie kumaliza upweke.
Wapenzi wengi walijikuta kwenye majuto baada ya kujiingiza kwenye uhusiano na watu ambao kimsingi hawaendani nao ila kwa lengo moja tu la kuwaondolea upweke, matokeo yake kufumaniwa na jamii kuwashangaa kwa kutokuwa wavumilivu.

MSUKUMO WA MKUMBO
Ninaposema msukumo wa mkumbo namaanisha nyakati ambazo rafiki zako watakupitia kwenda disko, mkifika huko bila kupanga kila mtu anakuwa na wake, wewe unajikuta peke yako unalazimika kumkubali aliyebaki nawe kwa lengo la kuogopa kuonekana huna mtu wa kujirusha naye. Baadaye unajikuta kwenye majuto makubwa.


source globalpublishers

Dawa ya Babu inawezekana kuwa katika mfumo wa vidonge -WHO

Thursday, May 05, 2011 / Posted by ishak / comments (1)


Foleni ya kupewa kikombe cha babu

UTAFITI unaoendelea kufanyika wa dawa ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile wa kijiji cha Samunge umebainika kuwa dawa inatibu maradhi sugu na Shirika la Afya Duniani [who] Kuikubali dawa hiyo
Hayo yamebainishwa na Askofu wa Kanisa la KKKT na kubainisha kuwa shirika hilo limekubali kuwa dawa hiyo inatibu maradhi sugu kama ilivyobainishwa awali katika utafiti wa kina walioufanya.

Imesemekana kuwa dawa hiyo inawezekana kuwa katika mfumo wa vidonge na chupa.

Shirika la Afya Duniani WHO ambalo lilituma wataalamu wake kuichunguza dawa ya babu, limebainisha hilo na kulifanyia kazi mikakati hiyo ya kuweka dawa hiyo katika mifumo hiyo na si kikombe pekee kama ilivyozoeleka, alisema Askofu huyo.

Pia dawa hiyo imethibitishwa na taasisi ya TMF na kubainisha kuwa dawa hiyo inatibu maradhi sugu.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa TMF, Marwa Gonzaga jijini Dar es Salaam.

Alisema wakati wakiendelea na utafiti huo walibaini kuwa tiba hiyo ni mchanganyiko wa mizizi ya miti shamba ya aina mbili ambayo ni kisayansi unafahamika kama Carissa Spinarum na mti wa Ntuntwa.

Tayari dawa ya babu imeshajizolea sifa ndani na nje ya nchi ambapo watu wameendelea kumiminika kijijini hapo kunywa dawa hiyo.

Hata hivyo taarifa zilizopatikana baadae zimesema kuwa babu amekataa dawa yake kufanyiwa mabadiliko yoyote kwakuwa Mungu hapendi.

Babu alisema kuwa kwakuwa dawa hiyo ni ya miujiza alioteshwa na Mungu, masharti aliyopewa na mungu kwenye ndoto yake hayaruhusu dawa hiyo ifanyiwe mabadiliko yoyote yale. Labda kama ataoteshwa ndoto nyingine ya kupewa ruhusa kufanya hivyo.

source nifahamishe

Wakristo Wamsalie Osama

Thursday, May 05, 2011 / Posted by ishak / comments (0)



Kardinali Albert Vanhoye

Wakristo inabidi wasali kumuombea makazi mema peponi Osama bin Laden ingawa alikuwa ni adui wao kwakuwa kutoa msamaha ndio mafundisho ya biblia.
Ingawa Osama alikuwa ni adui wa wakristo, wakristo inabidi wasimame kusali na kumuombea makazi mema Osama bin Laden.

Hayo yalisemwa na kardinali Albert Vanhoye mwenye umri wa miaka 87 wa kanisa katoliki nchini Italia ambaye alisema kuwa mafundisho ya biblia yanafundisha kusameheana.

"Mimi nimeusalia mwili wa Osama bin Laden, inatubidi tumuombee dua njema kama tulivyowaombea wahanga wa shambulio la septemba 11, hivyo ndivyo Yesu anavyowafundisha wakristo", alisema Kardinali Vanhoye.

"Yesu ametutaka tuwasamahe maadui zetu, tunaposali huwa tunasema "Baba, tusamehe kwa yale tuliyoyatenda kama vile tulivyowasamehe watu kwa yale waliyotutendea".

"Sala hii haiwezi kukubalika kama bado tutaendelea kuweka chuki kwa maadui zatu", alisema Kardinali Vanhoye, ambaye alichaguliwa kuwa Kardinali na Pope Benedict XVI mwaka 2006.

Kardinali Vanhoye anatambulika sana kwa mafundisho yake kuhusiana na biblia.


source nifahamishe

Binti wa Osama bin Laden Akiri Baba Yake Ameuliwa

Thursday, May 05, 2011 / Posted by ishak / comments (0)


Osama bin Laden

Mtoto wa kike wa Osama bin Laden amesema kuwa baba yake alikamatwa akiwa hai kabla ya kuuliwa kwa kupigwa risasi mbele yake na wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani.
Televisheni ya Al-Arabiya iliwanukuu maafisa usalama wa ngazi za juu wa Pakistan wakisema kuwa binti huyo wa Osama mwenye umri wa miaka 12, aliwaambia kuwa baba yake aliuliwa mbele ya familia yake na kisha mwili wake kuburuzwa hadi kwenye helikopta ya Marekani.

Mwili wa mtoto wa kiume wa Osama nao ulichukuliwa na wanajeshi wa Marekani na kupakizwa kwenye helikopta.

Televisheni ya Al-Arabiya iliwanukuu maafisa usalama wa Pakistan wakisema kuwa watoto sita wa Osama bin Laden, mmoja wa wake zake na mwanamke mmoja toka Yemen ambaye inasemekana alikuwa daktari wake walisafirishwa hadi kwenye mji wa Rawalpindi karibu na mji wa Islamabad, kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya jeshi.

"Hivi sasa wanapatiwa matibabu kwenye hospitali ya jeshi ya Rawalpindi" alisema mmoja wa Maafisa usalama wa Pakistan na kuongeza kuwa mke wa Osama bin Laden aliwaambia kuwa wamekuwa wakiishi Abbottabad kwenye nyumba hiyo kwa miezi sita sasa.

Afisa mwingine wa ngazi za juu wa Pakistan alisema kuwa baadhi ya taarifa zilizotolewa na Marekani kuhusiana na kukamatwa na kuuliwa kwa Osama hazina ukweli ndani yake.

"Hakuna hata risasi moja iliyopigwa toka kwenye nyumba ya Osama, ndege yao ya kivita ilipata matatizo ya kiufundi angani na ilianguka kwenye eneo la tukio".

Maafisa usalama wa Pakistan walisema kuwa hawakukuta silaha yoyote wala mabomu wakati walipofanya msako wa nguvu ndani ya nyumba ya Osama baada ya maiti yake kuchukuliwa na Marekani.

Uchunguzi wa kwanza ulifanyika jumatatu na jumanne walirudia kufanya msako kwenye nyumba hiyo yenye vyumba 13. Walichokuta ndani ya nyumba ya Osama ni nyati wawili, ng'ombe mmoja na kuku wapatao 150.

"Kulikuwa hakuna handaki wala sehemu maalumu ya kujificha ndani ya nyumba hiyo, ndio maana sielewi kwanini mtu anayetafutwa kuliko watu wote duniani alienda kuishi pale", alisema afisa huyo wa Usalama wa Pakistan.


source nifahamishe