Mabaki ya Binadamu Yakutwa Kwenye Tairi la Ndege

Sunday, July 11, 2010 / Posted by ishak /


Mabaki ya mwili wa binadamu yamekutwa kwenye matairi ya ndege ya Saudi Arabia iliyokuwa ikitoka Lebanon kuelekea Saudi Arabia.
Mabaki ya mwili wa binadamu yamekutwa kwenye matairi ya ndege ya shirika la ndege la Saudia, Nas Air wakati ndege hiyo ilipotua kwenye uwanja wa ndege wa Riyadh.

Maafisa wa Lebanon walisema kuwa mabaki hayo ni ya mwanaume aliyejaribu kusafiri bure toka Lebanon kwa kujificha kwenye sehemu ya matairi ya ndege.

"Mwanaume ambaye hakutambulika jina lake alifanikiwa kujificha kwenye sehemu ya matairi ya ndege bila ya waongozaji wa ndege mjini Beirut kumuona", alisema afisa mmoja wa Lebanon.

Ndege ya Nas Air namba XY 720 ilipaa toka uwanja wa ndege wa Beirut ijumaa usiku na ilitua Riyadh siku ya jumamosi asubuhi.

Mabaki ya mwili wa mwanaume huyo yalionekana wakati wa ndege hiyo ilipokuwa ikifanyiwa marekebisho baada ya kutua.

Shirika la habari la Lebanon NNA lilisema kuwa baadhi ya abiria walimuona mwanaume huyo aliyekuwa amebeba kibegi kidogo mgongoni akijificha kwenye sehemu ya matairi ya ndege wakati ndege hiyo ikijiandaa kuanza safari.

"Abiria walimpa taarifa rubani lakini hakuchukua hatua yoyote na alianza kuiendesha ndege kujiandaa kupaa bila ya kuwataarifu waongoza ndege", lilisema shirika hilo la habari.

Mwanaume huyo alipondwa pondwa na matairi ya ndege na mabaki ya mwili wake yalibaki yamegandia kwenye matairi ndege ilipotua.

Maafisa wa Nas Air walisema kuwa wanasubiri taarifa ya mamlaka ya anga ya Saudia kabla ya kusema chochote kuhusiana na suala hilo.

source nifahamishe