Picha ya Maiti ya Mandela Yazua Mzozo Afrika Kusini

Saturday, July 10, 2010 / Posted by ishak /


Msanii ambaye amechora picha ya rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela akiwa amefariki maiti yake ikifanyiwa uchunguzi ameingia kwenye mzozo mkubwa na chama tawala cha ANC.
Chama tawala nchini Afrika Kusini, African National Congress (ANC) kimelaani picha hiyo ambayo imetengezwa na msanii wa nchini humo na kuwekwa kwenye shopping centre mjini Johannesburg.

ANC imesema kuwa picha hiyo inamvunjia heshima mzee Mandela kwa kuzivunja haki zake.

Picha hiyo inauonyesha mwili wa Mandela ukiwa umepasuliwa huku viongozi wakuu wa Afrika Kusini wakiwa wameuzunguka.

Katika picha hiyo, maiti ya Mandela inaonekana ikiwa imelazwa kwenye meza huku mwanaharakati wa kupambana na ukimwi, Nkosi Johnson, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 12, anaonekana akiifanyia uchunguzi maiti ya Mandela.

Desmond Tutu, rais wa zamani wa Afrika Kusini, FW de Klerk, Thabo Mbeki na wanasiasa wengine wanaonekana wakiwa pembeni wakiangalia kinachoendelea.

Pamoja na tuhuma zote, msanii Yiull Damaso aliyechora picha hiyo amesema kuwa nia yake kubwa ni kuwakumbusha watu juu ya kifo.

"Nelson Mandela ni mtu mkubwa sana, lakini ni mtu kama watu wengine.. kifo cha Mandela ni kitu ambacho kitatokea na sote kwa pamoja kama taifa itatubidi tukipokee", alisema Damaso alipokuwa akiongea na shirika la habari la Uingereza la BBC.

Kuongelea kifo cha Mandela mwenye umri wa miaka 91 kunaonekana kama ni uchuro na huonekana kama kumvunjia heshima mzee Mandela.

Mwandishi wa habari wa BBC alisema kuwa wananchi wa Afrika Kusini hawazungumzii kabisa kifo cha Mandela kwa kuhofia ukweli kuwa siku moja wataamka mzee Mandela akiwa hayupo tena.

Uongozi wa Hyde Park Mall ambako picha hiyo imewekwa kama maonyesho, umesema kuwa umepokea malalamiko mengi kuhusiana na picha hiyo kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo ndugu wa Mandela.

Hata hivyo uongozi huo umesema utaendelea kuunga mkono Uhuru wa Kujieleza kwenye Sanaa.


source nifahamishe