Afariki Baada ya Kulipukiwa na Simu ya Nokia

Thursday, August 19, 2010 / Posted by ishak /


Mwanaume mmoja nchini India amefariki dunia baada ya simu yake aina ya Nokia kumlipukia wakati akiwasiliana na mtu mwingine kwa kutumia simu hiyo.
Mwanaume huyo aliyetajwa kwa jina la Gopal Gujjar, mwenye umri wa miaka 23, alifariki dunia baada ya kupata majeraha makubwa shingoni, mabegani na masikioni.

Taarifa zinasema kuwa Gujjar mkazi wa jimbo la Rajasthan nchini India alikuwa akiwasiliana na mtu mwingine kwa kutumia simu yake aina ya Nokia wakati mlipuko mkubwa ulipotokea.

Mwili wake ulikutwa pembeni ya mabaki ya simu yake kwenye shamba lake lililopo kwenye kijiji cha Banda, limeripoti gazeti la The Times of India.

Polisi walithibitisha kupatikana kwa mabaki ya simu aina ya Nokia 1209 ya mwaka 2008.

Gazeti la The Times of India limesema kuwa tukio hili huenda likawa tukio la kwanza nchini humo kwa mtu kulipukiwa na simu ambayo haipo kwenye umeme ikichajiwa.

Mwezi januari mwaka huu, mwanamke mmoja nchini India mwenye umri wa miaka 27 alifariki dunia baada ya kulipukiwa na simu iliyotengenezwa China wakati akiongea huku akiichaji simu hiyo kwenye umeme.

Vifo vya watu kulipukiwa na simu vimekuwa vikiripotiwa mara nyingi nchini China, Korea Kusini na Nepal.

source nifahamishe