Mwanamke Mwenye Matumbo Mawili ya Uzazi Azaa Mapacha wa Mimba Mbili Tofauti

Wednesday, August 10, 2011 / Posted by ishak /

Madaktari wanasema kwamba hali kama hii humtokea mwanamke mmoja tu katika wanawake milioni 50 lakini pamoja na uwezekano huo mdogo sana mwanamke mmoja nchini India aliyekuwa na matumbo mawili ya uzazi alipata mimba mbili kwa wakati tofauti na amejifungua watoto wawili mapacha kwa wakati mmoja.
NewsImages/5874618.jpgRinku Devi alikuwa akijua kuwa ana mimba ya watoto mapacha lakini alikuwa hajui kwamba alikuwa ana matumbo mawili ya uzazi na watoto wake mapacha walikuwa katika matumbo tofauti kutokana na ujauzito ulioingia kwa nyakati tofauti.

Madaktari waliielezea hali aliyo nayo Rinku kuwa inajulikana kama kama "uterus didelphys" au "double uterus" na hutokea kwa mwanamke mmoja tu kati ya wanawake milioni 50.

Rinku ambaye ni mke wa afisa wa jeshi, alijifungua watoto wake mapacha kwenye hospitali iliyopo kaskazini mwa India kwenye mji wa Patna.

Hali aliyokuwa nayo Rinku iligundulika wakati Rinku alipoingia leba baada ya kuzidiwa na uchungu wa uzazi.

Madaktari waligundua kuwa Rinku alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha ambao ujauzito wao ulipishana kwa mwezi mmoja.

"Niligundua kuwa nina matumbo mawili ya uzazi wakati nilipokuwa kwenye uchungu wa leba", alisema Rinku mwenye umri wa miaka 28.

Rinku aliwahi kujifungua mtoto wa kiume miaka minne iliyopita na hakukumbana na tatizo lolote.

"Sikujua cha kufanya, nilikuwa kwenye maumivu makali huku nikiogopa, sijawahi kusikia kitu kama hichi", aliendelea kusema Rinku.

Rinku alijifungua watoto wake mapacha kwa njia ya upasuaji kabla ya watoto hao kutimiza miezi tisa. Watoto hao walikuwa na uzito wa kilo mbili na kilo 1.5.

"Kutoka na ripoti za hospitali nilijua alikuwa na mimba ya watoto mapacha lakini nilipogundua ana matumbo mawili tofauti ya uzazi nilishtuka sana, sikuwahi kukutana na hali kama hii", alisema daktari wa Rinku.

Mimba kama hizi huwa ni hatari kwa maisha ya mama na mtoto, huwa kuna uwezekano mkubwa wa mimba kuharibika au watoto kuzaliwa kabla ya muda wao au watoto kuzaliwa wakiwa na uzito mdogo sana, alisema daktari huyo.


source nifahamishe