Wanajeshi Wa Kikosi Kilichomuua Osama bin Laden Wauliwa

Wednesday, August 10, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

NewsImages/5870762.jpg

Wanajeshi wa Marekani wapatao 22 toka kikosi cha Seal Team Six kilichotumika kumuua Osama bin Laden wamefariki dunia baada helikopta waliyokuwemo kutunguliwa na makombora ya Taliban nchini Afghanistan.
Jeshi la Marekani limepata pigo kubwa sana la mwaka baada ya kupoteza jumla ya wanajeshi 31 wakiwemo wanajeshi 22 toka kikosi maalumu cha Seal Team Six ambacho wanajeshi wake walitumika katika shambulio la kumuua kiongozi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden.

Seal Team Six ni kikosi maalumu cha makomandoo wa Marekani ambacho ndicho kilichotumika kuivamia nyumba ya Osama bin Laden nchini Pakistan na kumuua kiongozi huyo wa Al-Qaeda.

Taarifa iliyotolewa ilisema kwamba helikopta ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa imewabeba wanajeshi 31 wa Marekani pamoja na makomandoo saba wa Afghanistan ilitunguliwa na makombora ya wanamgambo wa Taliban.

Kuuliwa kwa wanajeshi wengi wa Marekani ndani ya siku moja ni pigo kubwa sana kwa jeshi la Marekani katika vita hivyo vya Afghanistan ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa takribani miaka 10 sasa.

Mmoja wa maafisa wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba helikopta hiyo ya kijeshi ya Marekani ilitunguliwa na Taliban kwenye mji wa Wardak usiku wa siku ya ijumaa.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba helikopta hiyo ilitunguliwa wakati ilipokuwa ikifanya shambulizi kwenye maeneo yanayotawaliwa na Taliban kwenye mji wa Wardak.

"Tulikuwa nyumbani usiku wakati tulipoona helikopta ikitua juu ya paa la jumba la kamanda wa Taliban na mara risasi zilianza kuvurumishwa toka pande zote mbili", alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Mohammad Saber.

Saber aliongeza kuwa helikopta hiyo iliamua kuondoka toka eneo hilo lakini ghafla ilidondoka chini na kulipuka.

Msemaji wa Taliban, Zabiullah Mujahid alisema kwamba wanamgambo wa Taliban ndio waliyoiangusha helikopta hiyo kwa kombora.

Pia Mujahid alibainisha kuwa wanamgambo wanane wa Taliban waliuliwa wakati wa shambulio hilo.


source nifahamishe

Mwanamke Mwenye Matumbo Mawili ya Uzazi Azaa Mapacha wa Mimba Mbili Tofauti

Wednesday, August 10, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Madaktari wanasema kwamba hali kama hii humtokea mwanamke mmoja tu katika wanawake milioni 50 lakini pamoja na uwezekano huo mdogo sana mwanamke mmoja nchini India aliyekuwa na matumbo mawili ya uzazi alipata mimba mbili kwa wakati tofauti na amejifungua watoto wawili mapacha kwa wakati mmoja.
NewsImages/5874618.jpgRinku Devi alikuwa akijua kuwa ana mimba ya watoto mapacha lakini alikuwa hajui kwamba alikuwa ana matumbo mawili ya uzazi na watoto wake mapacha walikuwa katika matumbo tofauti kutokana na ujauzito ulioingia kwa nyakati tofauti.

Madaktari waliielezea hali aliyo nayo Rinku kuwa inajulikana kama kama "uterus didelphys" au "double uterus" na hutokea kwa mwanamke mmoja tu kati ya wanawake milioni 50.

Rinku ambaye ni mke wa afisa wa jeshi, alijifungua watoto wake mapacha kwenye hospitali iliyopo kaskazini mwa India kwenye mji wa Patna.

Hali aliyokuwa nayo Rinku iligundulika wakati Rinku alipoingia leba baada ya kuzidiwa na uchungu wa uzazi.

Madaktari waligundua kuwa Rinku alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha ambao ujauzito wao ulipishana kwa mwezi mmoja.

"Niligundua kuwa nina matumbo mawili ya uzazi wakati nilipokuwa kwenye uchungu wa leba", alisema Rinku mwenye umri wa miaka 28.

Rinku aliwahi kujifungua mtoto wa kiume miaka minne iliyopita na hakukumbana na tatizo lolote.

"Sikujua cha kufanya, nilikuwa kwenye maumivu makali huku nikiogopa, sijawahi kusikia kitu kama hichi", aliendelea kusema Rinku.

Rinku alijifungua watoto wake mapacha kwa njia ya upasuaji kabla ya watoto hao kutimiza miezi tisa. Watoto hao walikuwa na uzito wa kilo mbili na kilo 1.5.

"Kutoka na ripoti za hospitali nilijua alikuwa na mimba ya watoto mapacha lakini nilipogundua ana matumbo mawili tofauti ya uzazi nilishtuka sana, sikuwahi kukutana na hali kama hii", alisema daktari wa Rinku.

Mimba kama hizi huwa ni hatari kwa maisha ya mama na mtoto, huwa kuna uwezekano mkubwa wa mimba kuharibika au watoto kuzaliwa kabla ya muda wao au watoto kuzaliwa wakiwa na uzito mdogo sana, alisema daktari huyo.


source nifahamishe

Ajaribu Kumtorosha Mfungwa Kwa Kutumia Begi

Tuesday, July 05, 2011 / Posted by ishak / comments (0)




Mfungwa Juan Ramirez Tijerina akiwa amejificha ndani ya begi akijaribu kutoroka jela Tuesday, July 05, 2011 6:54 PM
Mwanamke mmoja wa nchini Mexico ameingia matatani baada ya jaribio lake la kumtorosha mumewe toka jela kwa kumdumbukiza ndani ya begi na kisha kujaribu kulikokota begi hilo kutokana nalo nje ya jela.
Maafisa jela katika jela ya Chetumal nchini Mexico jana walipigwa na bumbuwazi baada ya kumkamata mwanamke akijaribu kumtorosha mumewe toka jela kwa kumficha ndani ya begi.

Walinzi wa jela hiyo walimuona Maria del Mar Arjona mwenye umri wa miaka 19, akionekana mwenye wasiwasi wakati akitoka nje ya jela huku akilikokota begi ambalo lilionekana limetuna sana.

Walipomsimamisha na kulichunguza begi hilo hawakuamini macho yao walipomuona mfungwa Juan Ramirez Tijerina akiwa amejikunja kama vile mtoto akiwa tumboni mwa mama yake.

Maria aliingia na begi hilo jela wakati alipopewa nafasi ya kumtembelea Juan ambaye anatumikia kifungo chake ndani ya jela hiyo.

Juan alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutupwa jela mwaka 2007 alipopatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Maria alitiwa mbaroni wakati akisubiri kufikishwa mahakamani.



source nifahamishe

SEMINA YA VITAMBULISHO KWA WAWAKILSHI

Sunday, July 03, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifungua semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Utambuzi wa usajili na Vitambulisho vya Taifa,katika ukumbi wa Ocean View Hotel Kilimani Zanzibar jana,(kulia) Makamo wa Pili wa Rais Balozi Sei Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifungua semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Utambuzi wa usajili na Vitambulisho vya Taifa,katika ukumbi wa Ocean View Hotel Kilimani Zanzibar jana,(kulia) Makamo wa Pili wa Rais Balozi Sei Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya utambuzi na usajili wa Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maina,akizungumza akitoa taarifa kuhusiana na mamlaka ya vitambulisho wakati wa ufunguzi wa Semina kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein
Baadhi ya watendaji wa Mamlaka ya utambuzi na usajili wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) wakisikiliza kwa makini hotuba iliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akifungua semina ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Utambuzi wa usajili wa Vitmbulisho vya Taifa,katika ukumbi wa Ocean View Hotel Kilimani Zanzibar jana
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,wakimsikiliza Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akitoa hotuba yake katika ufunguzi wa Semina ya wajumbe hao inayohusu usajili wa vitambulisho vya Taifa,iliyoandaliwa na Mamlaka ya Utambuzi na Usajili vitambulisho vya Taifa,(NIDA) katika ukumbi wa Ocean View Hoteli Kilimani Zanzibar


source othman mapara blog

Radi Yaua Wanafunzi 18 Shuleni Uganda

Saturday, July 02, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Radi iliyopiga kwenye shule moja ya msingi nchini Uganda, imewaua watoto 18 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 50.
Radi hiyo iliyopiga kwenye shule ya msingi ya Runyanya katika wilaya ya Kiryandongo magharibi wa jiji la Kampala, imepelekea vifo vya wanafunzi 15 wa kike na watatu wa kiume.

Msemaji wa polisi, Judith Nabakooba alisema kuwa zaidi ya wanafunzi wengine 50 walijeruhiwa na radi hiyo.

“Baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa waliwahishwa hospitali za karibu lakini wanafunzi 15 waliojeruhiwa vibaya sana waliwahishwa kwenye hospitali kuu ya wilaya”, alisema Nabakooba.

Magazeti ya kila siku ya Uganda yaliripoti kuwa wanafunzi wengine 21 katika shule nyingine iliyopo kwenye wilaya ya Zombo, nao walijeruhiwa vibaya baada ya kuunguzwa na radi.

Wakati gazeti la The Daily Monitor likiripoti jumla ya wanafunzi 28 wameishafariki kutokana na radi tangu wiki iliyopita, msemaji wa polisi hakutoa idadi kamili ya wanafunzi waliofariki kutokana na radi katika msimu huu wa mvua zilizoambatana na radi



source nifahamishe

Ukiwa Mchungaji Kanisani Nigeria, Utajiri Nje Nje

Thursday, June 23, 2011 / Posted by ishak / comments (0)



Mchungaji tajiri kuliko wote Nigeria, Mchungaji David Oyedepo

Uchunguzi uliofanywa nchini Nigeria umebaini kuwa wachunga kondoo wa Bwana nchini humo mbali ya kuhubiri neno la bwana wanatengeneza pesa ya maana kiasi cha kwamba baadhi yao wanamiliki ndege, hoteli na biashara kubwa.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Muandishi wa Nigeria wa jarida la Marekani la masuala ya uchumi, Forbes, wahubiri wa neno la bwana nchini Nigeria wanatengeneza pesa sana kutokana na uchungaji kiasi cha kufanananishwa na matajiri wa biashara ya mafuta.

Mfonobong Nsehe akitoa ripori ya uchunguzi wake alisema kuwa wachungaji wa Nigeria wanaishi maisha ya kifahari na wana miradi mikubwa ya kibiashara.

"Kuhubiri ni biashara inayolipa sana, sawa sawa na biashara ya mafuta", alisema Nsehe.

Utajiri wa wachungaji watano maarufu nchini Nigeria unakadiriwa kufikia dola milioni 200, alisema Nsehe.

Makanisa mengi yameibuka nchini Nigeria na waumini wamekuwa wakiongezeka.

Nsehe alisema kuwa mchungaji tajiri kuliko wote ni Mchungaji David Oyedepo wa kanisa la Living Faith World Outreach Ministry, ambaye utajiri wake ni dola milioni 150.

Mchungaji Oyedepo ndiye anayeshika nafasi ya pili akimiliki ndege nne, kampuni ya uchapishaji, chuo kikuu na shule moja na majumba ya kifahari jijini London na Marekani.

Mchungaji Chris Oyakhilome wa kanisa la Loveworld Ministries ana utajiri unaokadiriwa kuwa kati ya dola milioni 30 na 50. Mchugaji Oyakhilome anamiliki kampuni ya magazeti na majarida, stesheni ya televisheni, hoteli na kampuni ya majumba.

"Wachungaji hawa wanaishi maisha ya kifahari utawaona kwenye ndege zao binafsi na magari ya kifahari", alisema Nsehe.

Wachungaji wengine walioingia kwenye listi ya utajiri ni mchungaji Temitope Joshua Matthew mwenye utajiri kati ya dola milioni 10 na 15, Mchungaji Matthew Ashimolowo dola milioni 6-10, na mchungaji Chris Okotie mwenye utajiri kati ya dola milioni 3-10.

Nsehe aliongeza kuwa wawakilishi wa wachungaji wote isipokuwa mchungaji Ashimolowo, wamethibitisha taarifa ya umiliki wa mali za wachungaji hao.


source nifahamishe

Mfanyabiashara maarufu Zanzibar atinga kizimbani

Sunday, June 19, 2011 / Posted by ishak / comments (0)

Mfanyabiashara maarufu mjini Zanzibar Suleyum Mbarak Salim (35) amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuiibia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Sh bilioni 2.7.
Mfanyabiashara huyo, maarufu kama Morgan alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu, Amisa Suleima Hemed wa Mahakama ya mkoa mjini Magharibi Unguja jana.
Mwendesha mashtaka wa serikali, Maullid Mkame alisema mshtakiwa huyo anadaiwa kuiibia benki ya watu wa Zanzibar kati ya Machi 12 na Mei 11, 2009.
Alisema kwamba mstakiwa aliiba dola za Marekani 122,000 sawa na sh bilioni 2.7, ikiwa ni mali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kitendo ambacho ni kinyume na sheria namba 6 kifungu namba 124 (1) (4) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004. Mshtakiwa alikana shtaka hilo ambapo wakili anayemtetea Suleiman Salum aliomba mteja wake kupatiwa dhamana kwa vile shtaka alilofunguliwa ni miongoni mwa makosa yenye dhamana na haki yake kwa mujibu wa katiba.
Salum alisema kwamba mshtakiwa hajawahi kuhusishwa na mashtaka yoyote au kutiwa hatiani kwa kosa lolote na kuomba hakimu kumpatia dhamana mteja wake kwa vile ana mali zisizohamishika.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka, Maulid Makame alisema kwamba kwa muda mrefu, mshtakiwa huyo alikuwa akisakwa baada ya kuhusishwa na kesi namba 115 inayohusu wizi katika benki hiyo ya Zanzibar iliyofunguiliwa mwaka 2009 na kuwahusisha wafanyakazi wawili wa benki hiyo.
Alisema kitendo cha kumpa dhamana kinaweza kuathiri upelelezi hasa kwa kuzingatia uchunguzi wa suala hilo haujakamilika na mshtakiwa alikuwa anasakwa muda mrefu.
Hata hivyo, Hakimu Amisa alisema atatoa uamuzi juu ya ombi la dhamana Juni 23, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena katika mahakama ya Vuga mjini Zanzibar.



source ippmedia