Katibu mkuu wa chama kikuu cha upinzani katika siasa za visiwa vya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alitangaza jana kumtambua rais Karume kama rais halali wa Zanzibar na kusababisha hasira toka kwa wafuasi wa CUF ambao almanusura wamshushie kipigo wakidai viongozi wa CUF wamewasaliti.
Akiongea katika mkutano wa hadhara katika uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti, Maalim Seif Hamad alizomewa na kulazimika kushuka toka kwenye jukwaa akiwa chini ya ulinzi mkali baada ya kutangaza kuwa CUF imeamua kumtambua Rais Amani Abeid Karume.
Akiongea katika mkutano huo, Maalim Seif Hamad alisema kwamba baraza kuu la uongozi wa CUF limefanya kikao na kuamua kumtambua rais Amani Abeid Karume kama rais halali wa Zanzibar ili kumaliza msukosuko wa kisiasa katika visiwa hivyo.
Tamko hilo la Maalim Seif limefuatia kikao chake na rais Karume ndani ya ikulu ya Zanzibar na kisha kufuatiwa na mkutano wa baraza la kamati kuu ya chama hicho.
Maalim Seif alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa ni mgumu kufanywa kwa vile chama hicho kimekuwa kikiibiwa kura zake katika uchaguzi kila uchaguzi unapofanyika visiwani humo.
Uamuzi huo wa Maalim Seif kumtambua rais Karume uliamsha hasira za wafuasi wa CUF ambao walianza kumzomea huku wakipiga kelele "hatukubali hatukubali".
Kutokana na vurugu iliyoanza kuzuka kwenye mkutano huo ambapo baadhi ya wafuasi wa CUF walianza kutembea kuelekea kwenye jukwaa hilo, ilibidi Maalim Seif alazimike kushuka jukwaani na kupewa ulinzi mkali kunusuru maisha yake na kwenda kukaa kwenye jukwaa la viongozi wa CUF.
Baada ya hapo mwenyekiti wa chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba alipanda jukwaani kujaribu kuwatuliza wafuasi wenye hasira ambao waliwaona viongozi wao kama wasaliti na wengine kuangua kilio.
Hata hivyo hali haikutulia na wafuasi wa chama hicho walianza kupiga kelele za kuwataka viongozi wa chama hicho wajiuzulu.
Wafuasi hao walilalamika kuwa baadhi yao na ndugu zao wamepoteza maisha na wengine kuwa vilema kwa sababu ya kutetea siasa za chama hicho na matokeo yake chama hicho kimewasaliti.
Chama cha CUF kwa miaka kadhaa sasa katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, na 2005 kimekuwa kikigoma kuitambua serikali na baadhi ya nyakati wajumbe wake wa baraza la wawakilishi waligoma kuingia vikaoni.
Miongoni mwa mazungumzo ya kutafuta muafaka yaliyofanyika mwezi Februari mwaka huu, yalikwama baada ya CUF kukataa kumtambua rais Karume kama rais halali wa Zanzibar na kwa upande wake rais Karume aligoma kuwachagua wajumbe wawili wa CUF kuingia katika baraza la wawakilishi kwa sababu hiyo hiyo.
Ukiwa ni mwaka mmoja tu umebakia kufanyika kwa uchaguzi mwingine mkuu visiwani humo, baadhi ya wataalamu wa siasa za Zanzibar wanadhani CUF itapita katika kipindi kigumu huku wengine wakiamini kuwa uamuzi wa kusamehe dhuluma wanzodai kufanyiwa unaweza kukifanya chama hicho kuwa imara zaidi visiwani humo.
source.nifahamishe.com
CUF yamtambua Rais Karume, Maalim Seif Hamad Nusura Ashushiwe Kipigo
Sunday, November 08, 2009
/
Posted by
ishak
/
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment