Matumaini ya Mkenya Kumuoa Mtoto wa Clinton Yaota Mbawa

Tuesday, December 01, 2009 / Posted by ishak /


Chelsea Clinton, mtoto wa rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton amekubali posa ya mpenzi wake wa muda mrefu na hivyo kuyafuta kabisa matumaini ya raia wa Kenya ambaye alituma posa ya kumuoa akiahidi kutoa ng'ombe 20 na mbuzi 40.
Awali Mkenya huyo Godwin Kipkemoi Chepkurgor mwenye umri wa miaka 40 alituma posa ya kumuoa Chelsea Clinton, binti wa rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton mwaka 2000 na aliahidi kutoa ng'ombe 20 na mbuzi 40 kama mahari.

Kipkemoi alikumbushia nia yake ya kumuoa Chelsea, wakati mama yake Chelsea ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, alipofanya ziara yake nchini Kenya mwaka huu miezi michache iliyopita.

Hillary alimjibu Kipkemoi kuwa Chelsea ni mtu mzima na ana maamuzi yake lakini atamfikishia ujumbe huo.

Matumaini ya Kipkemoi kumuoa Chelsea yamefutika baada ya Chelsea kukubali kuchumbiwa na mpenzi wake wa muda mrefu Marc Mezvinsky.

Mezvinsky ambaye ni mfanyakazi wa benki ya Goldman Sachs alikuwa rafiki wa karibu wa Chelsea tangia utotoni.

Msemaji wa familia ya Clinton alitoa taarifa wiki hii kuwa Chelsea na Mezvinsky walivalishana pete ya uchumba wiki iliyopita.

Kama Chelsea angekubali kuolewa na Kipkemoi angekuwa mke wa pili wa Kipemoi ambaye alifunga ndoa na mwanamke mwingine raia wa Kenya mwaka 2006 baada ya kusubiria majibu ya posa yake ya kumuoa Chelsea kwa miaka sita.

Kipkemoi alidai kuwa mkewe yuko radhi kushea nyumba moja Chelsea Clinton.

Kwa mujibu wa sheria za Kenya, mwanaume anaruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja.


source.nifahamishe.com