Brazili Kupimana Ubavu na Tanzania Juni 7

Friday, May 28, 2010 / Posted by ishak /


Timu ya soka ya Brazili ikiwa na mastaa wake wote watakaoshiriki kombe la dunia nchini Afrika Kusini, itashuka dimbani kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kupimana ubavu na Tanzania.
Mabingwa wa dunia mara tano, Brazili wametua nchini Afrika Kusini tayari kwaajili ya kombe la dunia litakaloanza kutimua vumbi juni 11.

Wazee wa samba Brazili wakiwa na mastaa wao wote watawasili Tanzania juni 5 na mechi yao dhidi ya Tanzania itafanyika juni 7. Bila shaka hiyo itakuwa mechi ambayo kila mpenzi wa soka Tanzania hatapenda kuikosa.

Brazili katika mechi zake mbili za maandalizi kabla ya kuanza kwa kombe la dunia itacheza na Zimbabwe mjini Harare juni 2 kabla ya kucheza na Tanzania juni 7 jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo ili kufanikisha mechi hizo Tanzania na Zimbabwe zitailipa Brazili mshiko mnene ambao haukuwekwa bayana ingawa inasemekana ni mamilioni ya dola.

Mashirikisho ya soka ya Tanzania na Brazili yamethibitisha kuwepo kwa mechi hiyo juni 7.

Mechi hiyo itakuwa ni fursa pekee ambayo haijawahi kutokea kwa wapenzi wa soka Tanzania kuwaona live mastaa wa Brazili kama vile Kaka, Robinho, Maicon, Lucio, Dani Alves, Elano, Kleberson, Fabiano na wengineo.

Brazili ambayo inajulikana zaidi kwa jina la "Selecao" ipo kwenye kundi la kifo kundi G pamoja na Ureno, Ivory Coast na Korea Kaskazini.

Mechi ya kwanza ya Brazili itakuwa juni 15 ambapo itakiputa na Korea Kaskazini wakati Ivory Coast itachuana na Ureno siku hiyo hiyo.


source nifahamishe

0 comments:

Post a Comment